Habari za Punde

Dk.Hussein Ameahidi Kushirikiana na Ofisi ya Haki za Binadamu Katika Kuendeleza Ushirikiano Wao

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwakilishi na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika Bw. Marcel Akpovo, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar na ujumbe wake,mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 10-2-2023

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kushirikiana na  ofisi ya Haki za binadamu katika kuendeleza ushirikiano wao.

Alisema Zanzibar inafurahia kushirikiano uliopo baina yao na kuendeleza masuala mbalimbali ya sheria na haki za binaadamu ili kujenga uelewa mpana kwa jamii.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar  alipozungumza na Mwakilishi na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadam Kanda ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Bw. Marcel Akpovo aliyemtembelea.

Alisema Zanzibar kama sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  ina maeneo mengi inayofanyakazi na kutelekeza haki za binadamu ikiwemo, mahakama, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Jeshi la polisi na taasisi nyengine za sheria.

Alisema ushirikiano baina Serikali na ofisi hiyo ya kimataifa unasadifu adhma ya taasisi za sheria zilizopo nchini.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliiomba taasisi hiyo kuangalia uwezekano wa kuzisaidia taasisi za Serikali zinazofanyakazi na kutekeleza masuala ya sheria kwa kuwajengea uwezo kwenye maeneo wanayoyatumikia ikiwemo mafunzo ya muda mfupi na mrefu, warsha na masuala yatakayowajengea ufanisi na kuwaongezea weledi kwenye majukumu yao ya kila siku.

Alieleza Zanzibar inafanyakazi chini ya mwamvuli wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania licha ya baadhi ya taasisi hizo za Sheria kila moja ikijitegemea kwa mujibu wa maumbile ya upande inakotokea lakini pande zote mbili za Muungano zinashirikiana moja kwa moja kufanikisha wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania wote.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumtaka Mwakilishi huyo kuitumia vyema Zanzibar sio kwa utalii pekee bali kuichagua hata kwa mikutano na makongamano yao ya kimataifa kwani Zanzibar ina kumbi kubwa za mikutano ya kimataifa na vitutio vizuri kwa wageni.

Kwaupande wake Bw. Marcel Akpovo alimuambia Rais Dk. Mwinyi kwamba Ofisi yao inaungamkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwatumikia watu wake na kuwaletea maendeleo makubwa.

Alisema ofisi yao pia ina imani kubwa na Serikali na kwamba ushirikiano wao utaleta mafanikio zaidi kwa watu wa pande zote anazoziwakilisha nakuongeza kuwa, ujio wake kwa Zanzibar mbali na kuonana na Serikali ya awamu ya nane lakini kuimarisha ushirikiano wao.

Marcel ambae ni raia wa Bennin huko Afrika Magharibi, alimuahidi Dk. Mwinyi kwamba taasisi yao watafanyakazi bega kwa bega katika kuiunga mkono Serikali pamoja na kushirikiana kwenye masuala ya sheria na taasisi za sheria zilizopo nchini.

Alieleza taasisi yake itashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoa mafunzo kwa Makahimu, Majaji, Mawakili, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na taasisi za sheria zilizopo Zanzibar.

Alisema moja ya majukumu ya ofisi yao ni kuitangaza na kuungamkono kampeni ya kimataifa ya “Haki za wanawake na masuala ya jinsia” kwa kutekeleza wajibu wa haki za kila mtu kwenye jamii na kuendelea kuhamasisha.

Alisema Tanzaia ni nchi ambayo wameendeleza zaidi urafiki nakueleza kwamba wanaufurahia uhusiano mzuri uliopo baina ya taasisi yao na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao aliusifu ni Muungano wenye baraka na kuimarisha amani, upendo na mafanikio makubwa ya watu wa pande mbili hizo.

“Uhusiano wetu tulionao unaakisi maumbile halisi ya Muungano wa watu wa pande mbili za taifa hili la Tanzania” alisifu mgeni huyo.

Alisema lengo la ujio wao kwa Zaznzibar ni kuona kwa kiasi gani wataungamoko kwenye masuala upatikanaji wa haki kwa Zanzibar na maeneo yanayohusiana na hayo

Bw. Marcel Akpovo anatekeleza wajibu wake kwa mataifa ya Djibuti, Erictria, Ethiopia, Kenya, Sudan, Somali, South Sudan, Tanzania na Uganda.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.