Na.Maulid Yussuf -- Zanzibar
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto Mhe Anna Athanas Paul, amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga Nyumba Maalum ya kulelea Watoto ili kuwasaidia kulelewa katika mazingira salama.
Mhe Anna ameyasema hayo wakati mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania ndugu Dogo Iddi Mabrouk, kufika katika Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja kwa kumuangalia mtoto aliyeokotwa hivi karibuni katika maeneo ya Fuoni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesma ni vyema jamii inapokuwa na changamoto kuhusu watoto wasisite kuwapeleka katika nyumba hizo ili kuepusha athari za kuwatupa kwani hali hiyo inawakosesha haki zao za msingi ikiwemo malezi bora.
Amesema, Wizara imekuwa ikiweka bajeti mbalimbali za kuwatunza watoto hao na kuiaka jamii kuacha tabia ya kutupa watoto wasiokuwa na hatia.
"Musitupe watoto maana munapowaweka kwenye dastbin, kwenye vichaka watakula uchafu na hatimae kupoteza maisha, hili sio jambo la kiungwana jamii tuweni na utaratibu wa kulea watoto wetu na tukishindwa tuwafikishe katika nyumba zetu" amesisitiza Mhe Anna.
Hata hivyo, amewataka wanajamii kutumia Kinga maalumu za kutopata ujauzito ikiwa hayupo tayari kupata mtoto ili kuondokana na athari ya kutupa watoto wasiokuwa.
Mhe Anna ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja chini ya Madaktari wa kitengo cha Mtoto kwa kumshughulikia mtoto huyo tokea afikishwe hapo huku afya ya mtoto huyo ikiwa inaendelea vizuri.
Hata hivyo, amekishukuru chama cha Mapinduzi kupitia Jumuiya zake kwa kumtembelea mtoto huyo na kumpatia zawadi mbalimbali ambapo wamemfariji mtoto huyo.
Nae, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, ndugu Dogo Iddi Mabrouk ameiomba Serikali kuendelea na uchunguzi wa kumbaini mama mzazi wa mtoto huyo ili hatua za kisheria zichukuliwe kutokana na kitendo alichokifanya ni ukiukwaji wa haki za kibinaadamu.
"mtoto ni hidaya kutoka kwa Allah, si vyema kuwatupa watoto, kwani kuna watu wanatumia gharama kubwa kutafuta watoto, naomba wanawake wenzangu tuache tabia ya kuwatupa watoto" amesema ndugu Dogo.
Imetolewa na kitengo cha Uhusiano Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar.
No comments:
Post a Comment