Habari za Punde

MBETO: AFANYA ZIARA YA KUTEMBELEA MASOKO ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Khamis Mbeto Khamis,akisikiliza changamoto za mfanyabishara wa soko la Welezo Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ Unguja.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.                                                                                          

Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kimeridhishwa na hali ya upatikanaji wa chakula katika mwezi mtukufu wa ramadhani pamoja na bei za bidhaa zinazoingizwa katika masoko mbalimbali yaliyopo katika Mkoa wa Mjini Magharibi na maeneo jirani.

 

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalumya NEC, idara ya itikadi na uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,katika ziara yake ya kutembelea mazoko yaliyopo katika mkoa wa mjini magharibi.

 

Alieleza kwamba kupitia ziara hiyo amejiridhisha kuwa chakula nchini kipo na kinapatikana kwa bei elekezi ya Serika ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Aliwapongeza wafanyabishara nchini kwa kufuata maelekezo ya Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi, aliyewasihi kuhakikisha wanaleta chakula na kuuza kwa bei halali iliyowekwa na serikali.

 

Katika maelekezo yake Katibu huyo Mbeto, alisisitiza kuwa hali hiyo ya upatikanaji wa chakula nchini iwe endelevu kwani wananchi wanahitaji chakula wakati wote.

 

“Tunawapongeza wafanyabishara wote nchini kwa uzalendo wenu wa kuhakikisha chakula kinapatikana kwa wingi nchini na bei zake zina unafuu kwa wananchi wa hali ya kawaida, nasaha zangu ni kuwa endeleeni kutoa huduma hii ya kuuza vyakula vya aina zote isiishie katika mwezi huu wa ramadhani tu kwani kila siku wananchi wanahitaji kula.

 

changamoto ya zamu ya upigaji mnada kwa masoko yote hiyo naichukua nitaenda kukaa na viongozi wa Chama na Serikali tujadili na baada ya maamuzi ya vikao tutapata suluhisho hivi karibuni.”, alisema Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi Mbeto.

 

Alieleza kuwa Zanzibar  kuna chakula cha kutosha cha miezi mitatu mbele hivyo amewaomba wafanyabiashara kuendelea kufata bei elekezi ili kuona wananchi wanyonge wanamudu gharama za kununua chakula hicho.

 

Alifafanua kuwa mbali na bidhaa hizo pia meli ya bidhaa ya tende tayari imefika Zanzibar na imeanza kushusha mzigo huo kwa ajili ya kutumika katika mwezi mtukufu wa ramadhani. 

 

Pamoja na hayo aliwapongeza Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi, kwa juhudi zao za kupambana na tatizo la mfumoko wa bei duniani huku nchi zao mbili zikiwa na chakula cha kutosha kinachokidhi mahitaji ya wananchi.

 

Alichukua nafasi hiyo pia kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar ndg.Nahaat Mohamed Mahfoudh, kwa kutekeleza maagizo ya Chama Cha Mapinduzi ya kuhakikisha meli zote za chakula zinashusha bidhaa hizo kwa wakati ili wananchi mitaani wapate huduma hiyo.

 

Pamoja na hayo alitoa ufafanuzi juu ya changamoto ya ushuru kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kutoka Pemba amesema Chama cha Mapinduzi kikiwa ni msimamizi mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kitawaelekeza viongozi wa mkoa, wilaya, manispaa na bandari kukaa pamoja na wafanyabiashara wa masoko kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.

 

Kupitia ziara hiyo Mbeto, amewataka madiwani nchini kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kufanya usafi katika maeneo  mbalimbali hususani katika masoko na mitaro ili kuepuka mafuriko katika kipindi hiuki cha mvua za masika.

 

Kwa upande wake katibu wa kamati maalumu ya NEC,Idara ya mambo ya siasa na  Uhusiano wa Kimataifa Khadija Salum Ali,amewasihi    wafanyabiashara hao kuendeleza ushirikiano ili serikali iweze kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili.

 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mjini Zanzibar Rashid Simai Msaraka alisema suala la upatikanaji wa chakula nchini limetafutiwa ufumbuzi wa kudumu na kwa sasa kinapatikna kwa bei halali za serikali.

 

DC.Msaraka, aliwahakikishia wafanyabiashara wa soko la kibandamaiti kuwa soko hilo litaongezewa nguvu ili kuwa kubwa kuliko masoko yote yaliyowepo mkoa wa mjini magharibi.

 

Nao wafanyabiashara wa masoko mbalimbali wameiomba serikali kutoa maamuzi sahihi wapi mnada unatakiwa ufanyike ili kuepusha kuwatia hasara ya kuharibika kwa bidhaa zao. 

 

Pia wafanyabiashara hao waliomba serikali kushusha ushuru kwa bidhaa zinazotoka pemba ili kutoa unafuu kwa wananchi hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa ramadhani ili kuepusha kupanda kwa bei za bidhaa.


Katibu huyo Mbeto,alitembelea masoko ya Jumbi,Mwanakwerekwe ''C'',Mombasa,Welezo,Kibandamaiti,Darajani,soko la samaki malindi na katika gati ya badari ya kushusha mizigo malindi.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.