Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley (kushoto) wakisaini Mkataba wenye thamani ya dola ya Marekani 161.47 (sawa na shilingi 374.9 bilioni), kwa ajili ya mradi wa Umeme wa maporomoko ya maji wa Kakono (MW 88), mkoani Kagera, utakao ongeza Megawati 87.8 za umeme kwenye gridi ya Taifa, wakishuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum. (kulia), jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia N. Laverley (kushoto) wakionesha Hati za Mkataba wenye thamani ya dola ya Marekani 161.47 (sawa na shilingi 374.9 bilioni), kwa ajili ya mradi wa Umeme wa maji wa Kakono, wakishuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum. (kulia), jijini Dar es Salaam. Mradi huo utaongeza Megawati 87.8 kwenye gridi ya taifa na kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika mkoa wa Kagera, mikoa Jirani na nchi Jirani ya Uganda.Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (watatu kulia), Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley (katikati), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum. (wapili kulia), Naibu Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Bw. Axel-David Guillon (wa tatu kushoto), Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Céline Robert (wapili kushoto), Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil (wa kwanza kushoto) na Msemaji wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya nchini Bw. Cedric Merel (wa kwanza kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania, AfDB, AFD na Umoja wa Ulaya baada ya kusaini Mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 161.47 (sawa na shilingi 374.9 bilioni) kutoka AfDB na mwingine kutoka AFD wenye thamani ya Euro milioni 110 (sawa na shilingi 272.6 bilioni) kwa ajili ya mradi wa Umeme wa maji wa Kakono, mkoani Kagera. Tukio hilo limefanyika jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dar es Salaam)
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
WAKAZI wa Mkoa wa Kagera wanatarajia kuondokana na changamoto ya kukosa umeme wa uhakika baada ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kusaini mikataba ya mkopo yenye masharti nafuu ya dola za Marekani milioni 161.47 na euro milioni 110, mtawalia, sawa na shilingi bilioni 647.5 za Tanzania.
Mikataba imesainiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa upande wa Tanzania, Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini Tanzania Dkt. Patricia Laverley na Bi. Celine Robert, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa-AFD.
Dkt. Nchemba alifafanua kuwa kati ya fedha hizo zilizosainiwa, kiasi cha dola milioni 161.47 sawa na shilingi bilioni 374.9 kimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB na kiasi cha euro milioni 110 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 272.6 kimetolewa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa-AFD.
“Katika kutatua changamoto za nishati ya umeme mkoani Kagera, Serikali iliiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kufadhili Mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono, ambapo kwa pamoja - AfDB; AFD kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya; na Serikali ya Tanzania zimekubali kufadhili mradi huu wenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 325 sawa na shilingi 750 bilioni” alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa Serikali imebakiza kusaini mkataba wa msaada kutoka Umoja wa Ulaya wenye thamani ya euro milioni 35 sawa na shilingi 86.7 bilioni na kuuhamasisha Umoja huo wa Ulaya kuharakisha na kukamilisha maandalizi ya ufadhili huo ili mkataba wake usainiwe ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Kanda ya Ziwa ni eneo lenye tija kubwa katika uzalishaji wa madini na samaki wanaouzwa nje, ambapo uhitaji wa nishati ya umeme kwa gharama nafuu na wa uhakika ni muhimu kwa ustawi wa sekta husika lakini kwa muongo mmoja sasa, Kanda ya Ziwa imekuwa na sifa ya matumizi ya mitambo ya kutumia nishati ya dizeli ambayo ni gharama kubwa kuiendesha na kusababisha wakai hao kutokua na umeme wa uhakika na wa kutosha.
“Utekelezaji wa mradi huo utakamilika ndani ya miaka mitano (5) na utahusisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa MW 87.8 na kazi nyingine zikiwemo ujenzi wa shule ya msingi na kituo cha afya pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 28 na hivyo kuboresha hali ya maisha ya jamii ya kanda hiyo. Mradi huu pia unahusisha usambazaji wa umeme na utekelezaji wa mpango wa usimamizi wa mazingira na kijamii” alifafanua Dkt. Nchemba
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Dkt. Patricia Larveley, alisema kuwa mradi huo utakapo kamilika unatarajia kuwahudumia wakazi 210,000, viwanda vidogo na vya kati pamoja na migodi ya madini eneo la Kaskazini Magharibi mwa Tanzania kwa kuwa na nishati bora na ya uhakika pamoja na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ambayo ina athari kwa mazingira.
“Faida za kiuchumi zitakazotokana na uwepo na kukamilika kwa mradi huo, kutasaidia upatikanaji wa nishati yenye gharama nafuu, kuboreshwa kwa maisha ya wakazi wa Kagera, mambo ambayo yatachangia pia ukuaji wa uchumi imara na shindani wa Taifa” alisema Dkt. Laverley.
Alibainisha kuwa kusainiwa kwa mkataba huo, kumeifanya Benki yake kufikisha kiwango cha misaada na mikopo kilichotolewa kwa Tanzania kufikia dola za Marekani bilioni 2.7 ambapo asilimia 86 ya fedha hizo zimeelekezwa kwenye sekta za nishati, usafirishaji, maji na usafi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Bi. Celine Robert, ufadhili wa fedha zilizotolewa na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake utasaidia kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme si tu kwa Tanzania lakini pia nchi jirani ya Uganda ambapo idadi ya wanufaika inakadiriwa kuwa kati ya watu milioni 3 hadi 4.
“Pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa kupata rasilimali fedha takribani dola za Marekani milioni 300, hatua hiyo inaashiria ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Tanzania, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa” alisema Bi. Celine Robert.
Alisema kuwa kwa upande wa Ufaransa, uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili, umewezesha kiwango cha misaada na mikopo kufikia wastani wa euro milioni 150 kila mwaka ambapo mpaka kufikia wakati huu, Ufaransa kupitia Shirika lake, imewekeza zaidi ya euro bilioni 1 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 2.5.
Naye Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, aliwashukuru washirika hao wa Maendeleo, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Umoja wa Ulaya kwa kutoa fedha hizo ambazo zitachangia kuboresha maisha ya wananchi lakini pia kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika maeneo ya mradi na Tanzania kwa ujumla.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imeshuhudiwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa nchi na mashirika ya kimataifa, akiwemo Naibu Balozi wa Ufaransa Mhe. Axel Guillon. Mkuu wa Ushirikiano wa Eu nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Cedric Merel, ujumbe kutoka Mradi wa Umeme Kakono na TANESCO.
No comments:
Post a Comment