Na.Abdulrahim Khamis -OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaweka mazingira mazuri kwa Skuli zote ili kukuza ufaulu nchini.
Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati akikabidhi futari kwa wanafunzi wanaokaa Dakhalia Skuli ya Sekondari Lumumba Mkoa wa Mjini Magharibi na Skuli ya Sekondari ya Hasnuu Makame Kibuteni.
Amesema ni vyema kwa wanafunzi hao kuendeleza juhudi hizo kwa kusoma kwa bidii ili kuendeleza Mapinduzi katika Sekta ya elimu.
Aidha Mhe. Hemed amewapongeza walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wa elimu Mkoa wa Kusini Unguja kwa kukuza ufaulu katika Mkoa huo hatua inayoonesha utayari wao katika kukuza sekta hiyo.
Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameungana na waumini wa Mskiti wa Mtegani Kusini Unguja katika Ibada ya Sala ya Ijumaa na kuwataka wazazi na walezi kusimamia malezi ya vijana kupitia maelekezo ya Kitabu kitukufu cha Qur-ani pamoja na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W)
Aidha amesema ni vyema kudumisha mila, silka na Tamaduni za Kizanzibari ili kuilinda jamii na janga lililoikumba jamii ya Kizanzibari na Tanzania kwa ujumla.
Wakati wa Mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefika Shehia ya Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajali ya kukabidhi vifaa kwa wananchi walioathirika na upepo uliotokea tarehe Mosi na tarehe Saba Aprili ikiwa ni ahadi aliyoitoa mwanzoni mwa Wiki hii.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua jitihada hizo kwa kufuata maelekezo ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili wananchi warudi katika makazi yao kabla ya kukamilika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar Ndugu Makame Khatib Makame amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa miongozo yake juu ya kukabiliana na Maafa nchini.
Amesema Kamisheni kwa kusaidiana na Serikali ya Mkoa wa Kaskazini imefanya tathmini ya mahitaji yanayohitajika katika kurudisha hali ya wananchi
Jumla ya Mabati 2094, Saruji Mifuko 50, Matofali 2335 Boriti na mbao za kuezekea vimekabidhiwa kwa wananchi hao ikiwa ni ahadi aliyoitoa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyoitoa mwanzoni mwa wiki hii alipopita kuwafariji waathirika hao.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/04/2023
No comments:
Post a Comment