Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kufuata Maelekezo Yanayotolewa na Wataalamu Juu ya Tahadhari za Mapema Kuhusiana na Mvua za Masika

Na Khadija Khamis Maelezo Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Salhina Mwita Ameir amewataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu juu ya tahadhari za mapema kuhusiana na mvua za masika .

Amesema tunaelewa kuwa ni vigumu kuepukana  na majanga ya kimaumbile lakini tunanafasi kubwa ya kujikinga na kujiepusha kutokana  na visababishi vya majanga hayo .

Akizungumza wakati wa kikao cha kujadili mwenendo  wa mvua za masika na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Taasisi mbali mbali katika ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi .

Alieleza kuwa kutokana na taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) juu mwenendo wa mvua za masika kuwa za wastani na juu ya wastani hivyo iko haja ya watu wanaoishi mabondeni na njia za maji kuondoka mapema kabla ya athari kutokea.

Aidha alizitaka Taasisi za kukabiliana na maafa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbali mbali za mawasiliano kwa kutoa taarifa sahihi ambazo zitawasaidia kupunguza athari juu ya watu na mali zao.

“Taarifa ni vyanzo vya msingi kwa jamii kwa kujitayarisha kuchukua hatua za mapema na kupunguza athari, ”alisema Naibu Katibu huyo .

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kukabiliana na Maafa Makame Khatibu Makame amesema mjumuisho wa sekta mbali mbali za kukabiliana na maafa zina nafasi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa kila sekta ili kupunguza  athari za majanga  ,

Amefahamisha kuwa kikao hicho cha kujadili mwenendo wa mvua za masika, kupanga mikakati na kuona changamoto zilizopo na kuzijadili pamoja na kuchukuwa  hatua za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza .

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Masuod Makame Faki amesema mwenendo wa mvua za masika unaonyesha kuwa wilaya ya kusini Unguja na kati  kutakuwa na mvua za wastani  juu ya wastani na kwa upande wa Kisiwa Pemba zitakuwa ni za wastani chini ya wastani .

Aidha amesema mwenendo wa mvua hizo kwa  kipindi cha mwezi wa Mei inategemewa kuwa na mvua kubwa na za kawaida na kuongezeka hadi Aprili na Juni.

Mkuu wa Devisheni ya  Mawasiliano na Tahadhari za Mapema, Omari Mohamed Ali akiwasilisha mada juu ya maeneo hatarishi yaliyopo katika makaazi ya watu ambayo yanaviashiria vya kupata mafuriko ikiwemo kisiwa maboga pamoja na maeneo mbali mbali yaliyokuwa na makaazi ya watu katika njia za maji ya mvua .

Alisema kuwa katika kipindi cha mvua ya masika majanga mengi yanaweza kujitokeza katika jamii ikiwemo mafuriko maradhi ya mripuko,upepo mkali ,radi ajali za barabarani, baharini ,kuanguka nguzo za umeme,  kukatika madaraja,kupasuka mabomba ya maji,kuanguka nyumba za maakaazi uharibifu wa mazingira pamoja na upotevu wa watu na mali zao .

Alieleza kuwa jamii isiwe inapuuza taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa kwani kufanya hivyo kutahatarisha usalama wa maisha yao.

Nao wajumbe hao wameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa kushauriana na viongozi wakuu wa Wizara ya Elimu wakati wa muelekeo wa mvua kubwa za masika ili kuwazuwia wanafunzi wasitoke majumbani mwao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.