SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar imesema inajukumu kubwa la kuzifanyia kazi takwimu za Sensa ya watu
na makaazi ya mwaka 2022, ili kujipanga na utekelezaji wa mipango ya maendeleo,
kiuchumi na kijamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar
alipopokea ripoti ya Kamati ya Sensa ya watu na makaazi iliyofanyika mwaka
jana.
Rais Dk. Mwinyi
alisema sensa hiyo imetoa mambo mengi ambayo lazima yafanyiwe kazi kabla ya
kukamilika kwa mpango wa Maendeleo 2025 - 2050 kuelekea mwisho wa Dira ya
Maendeleo ambako mwaka 2030 alieleza Zanzibar itakadiriwa kuwa na idadi kubwa
zaidi ya watu.
Alisema ripoti hiyo
na nyengine zitakazofuata lazima zitafutiwe namna nzuri ya kufanyiwa kazi kwa
undani ili serikali ijipange katika masuala mazima ya maendeleo ya nchi.
“Ripoti kama hii na
nyengine zitakazokuja lazima tutafute namna nzuri ya kujipanga jinsi ya
kuzifanyia kazi kwa undani ili serikali iweze kujipanga sasa kwa masuala mazima
ya maendeleo ya nchi kwa kipindi cha muda mfupi, muda wakati na mrefu” alifafanua
Rais, Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk.
Mwinyi aliipongeza Kamati ya ushauri wa sensa Kitaifa kwa kazi nzuri
waliyoikamilisha.
“Tulidhani tukishapata
idadi ya watu na makazi basi kazi imekwisha, kumbe bado kuna kazi kubwa
yakufanya, kwa kweli mnaendelea kuifanya kwa ufanisi mkubwa” Rais Dk. Mwinyi
aliipongeza kamati hiyo.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah
aliwaahidi Rais Dk. Mwinyi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Samia Suluhu Hassan kwamba kamati yao ya ushauri wa sensa Kitaifa, itajitahidi
kuendeleza sehemu ndogo iliyobaki ili kulikamilkisha kwa vitendo zoezi hilo.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, aliwashuruku
Rais Dk. Mwinyi na Rais Samia kwa kuiamini kamati hiyo katika kukamilisha zoezi
zima la sensa kitaifa.
Naye, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema matokeo ya sensa
yanadhihirisha wazi kwamba ifikapo mwaka 2025 wakati wa kuhitimisha Dira ya
Maendeleo ya Tanzania, Zanzibar pekee itakua na idadi ya watu wapatao milioni
mbili na elfu nane na dunia itakapohitimisha maendeleo endelevu mwaka 2030,
Zanzibar inakadiriwa kuwa na idadi ya watu wasiopungua 2,440,000 na mwaka 2050
Zanzibar inakisiwa kuwa na idadi ya watu wasiopungua 4,630,000.
Dk. Mkuya alieleza
kwa mujibu wa viashiria hivyo vya idadi kubwa ya watu wa Zanzibar kwa wakati
huo, Serikali haina budi kuangalia upya sera ya idadi ya watu nchini pamoja na
kuzifanyia mabadiliko sera nyengine ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi na
jamii kwa wakati husika.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment