Na Khadija Khamis – Maelezo 02- 08-2023.
Kamishna wa Bima Tanzania Baghayo Abdalla Saquare amewataka watoa huduma ya kusajili na kutoa leseni kwa vyombo vya moto, kutekeleza vizuri majukumu yao ili kuondosha usumbufu kwa wateja.
Kauli hiyo imetolewa huko Mamlaka ya Bima TIRA, Kilimani wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiana na kugundulika kwa baadhi ya wakala kutokuwa waaminifu.
Alisema kuwa hali hiyo imejitokeza baada ya kufanyika ukaguzi wa vyombo vya moto katika Barabara za Unguja kuanzia tarehe 24 hadi 31 ,2023 kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Mhe. Rashid Msaraka, Mashirika ya bima, Jeshi la Polisi pamoja na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alifahamisha kuwa katika zoezi hilo la ukaguzi kumegundulika kwamba wakala wa Bima wa Tabasamu Centra Agency Company LTD ana hatia ya udanganyifu kwa kutoa huduma za bima kinyume na taratibu .
Aidha alisema wakala wa bima TABASAMU ni wakala halali na anafanya kazi na Makampuni matatu ya bima ambayo ni heritage, ZIC, na Srategis ambayo yote yana matawi yake Zanzibar.
Kamishana huyo alibainisha makosa ya wakala huyo ni kutowasilisha malipo ya ada ya bima kwenye kampuni ya bima jambo ambalo linaleta usumbufu kwa wateja ambao wameshalipia na taarifa zao hazipo kwenye mfumo wa TIRAMIS.
Alieleza kuwa ilibainika kuwa sampuli tisa kati ya 15 zilizokaguliwa hazikuwasilishwa katika kampuni ya bima ya Heritage licha ya ada zake kupokelewa na wakala tabasamu.
Aidha alifahamisha kuwa madhara ya kutowasilisha ada ya bima katika kampuni kunasababisha upotevu wa mapato kwa kampuni husika , tozo zinazotolewa na ada ya bima kuwa na upotoshaji kwenye takwimu ya ada ya bima zinazoandikishwa kwenye soko pamoja na kuleta taswira mbaya kwenye sekta ya bima nchini.
Nae Naibu Kamishna wa Bima Khadija Issa Said alisema kuwa zoezi hilo la ukaguzi litaendela kwa muda wa mwezi mmoja ili kuhakikisha wanawapata wale wananchi ambao wanaoendesha vyombo vya moto bila ya kukata bima .
Aidha amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa mashirikiana yake ya pamoja katika kampeni hiyo ili kuhakikisha inafanikiwa kwa kukagua uhai na mwenendo wa kutoa huduma .
Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “KATA BIMA BILA YA SHURUTI “
No comments:
Post a Comment