Habari za Punde

CCM YAKIRI UMUHIMU WA RIPOTI YA APRM KWA WANANCHI NA SERIKALI

 


Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Mhe. Mohammed Said Mohammed (DIMWA) amesema kuwa mpango wa APRM Tanzania kuitathmini Serikali kwa vigezo vya Utawala Bora ni mzuri na unahitajika sana kuungwa mkono kwavile unalenga moja kwa moja kubaini changamoto zilizopo katika jamii na kuzitafutia suluhisho lake ili Serikali iweze kuleta ustawi mzuri kwa wananchi.

Hayo ameyasema leo hii wakati alipokutana na viongozi wa APRM Tanzania waliofika Ofisini kwake Kiswandui kwa lengo la kujitambulisha pamoja na kuelezea mikakati ya kuelekea Ripoti ya Pili ya Tathmini ya masuala ya Utawala Bora Tanzania.

Mhe. Dimwa amesema kuwa utaratibu wa kujitathmini unatumika pia katika Chama cha Mapinduzi kuangalia kwa namna gani wameweza kutekeleza Ilani ya Chama hivyo Ripoti ya Tathmini ya Utawala Bora ya APRM itawasaidia pia kunadi sera zao hususan katika uchaguzi mkuu wa 2025.

Ameongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi kipo tayari kufanya kazi kwa karibu na APRM Tanzania, hivyo itatoa mashirikiano makubwa katika kuhakikisha kuwa Tathmini hiyo inafanikiwa na kusisitiza kuwa suala la elimu kwa wananchi kuhusu APRM na Ripoti ya Pili lipewe kipaombele zaidi ili wananchi waweze kuhamasika na kutoa ushirikiano unaotakiwa pamoja na kuhakikisha kuwa Tathmini hizo zinafanyika mara kwa mara ili Serikali ielewe inaendaje katika suala la Utawala Bora.

Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Lamau Mpolo amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 43 za Afrika kati ya nchi 54 ambazo zimeridhia kuingia katika mpango wa hiyari wa kujitathmini kwa vigezo vya utawala bora, hivyo APRM Tanzania inawaomba wadau wote kutoa mashirikiano ya kila aina katika kuhakikisha kuwa Ripoti ya Pili ya Tathmini inafanikiwa na Tanzania iendelee kuwa kinara wa masuala ya Utawala Bora.

Aidha amesisitiza kuwa,dhumuni kuu la APRM ni kuhakikisha kuwa inaharakisha mpango wa maendeleo kwa wananchi hivyo ushiriki wao ni muhimu kwa vile mpango huu unaipa nchi yetu fursa ya kuwaonyesha kwa uwazi zaidi wabia wetu wa maendeleo na wawekezaji jitihada zetu za kujikwamua kiuchumi na kijamii na kuvutia uwekezaji na kundeleza heshima ya nchi yetu katika uso wa dunia.

Nae mratibu wa eneo la Uchumi Jamii APRM Tanzania Balozi Hemedi Mgaza amesema kuwa APRM imefarijika sana kuona kuwa Chama cha Mapinduzi kipo tayari kutoa ushirikiano mkubwa lakini pia ameahidi APRM Tanzania itahakikisha pia inasoma Ilani ya Chama hicho ili pia iweze kuitathmini.

Meneja Habari na mawasiliano APRM Badria Masoud amesisitiza kuwa suala la elimu kwa wananchi ni kipaombele cha APRM kwasasa kwani elimu itakapowafikia kwa wakati na kwa wananchi waliowengi itasaidia kuwashajihisha na kuweza kutoa ushirikiano wa kutoa maoni yanayostahiki ili waweze kuitathmini Serikali yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.