Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Atembelea Ujenzi wa Mradi wa Mabanda ya Maonesho Nyamazi Wilaya ya Magharibi "B" Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla akizungumza wakati wa ziara yake kukagua Mradi wa ujenzi wa Mabanda ya Maonesho ya Biashara Nyamazi Wilaya ya Magharibi "B" Unguja na (kulia kwake) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shaban na (kushoto kwake) Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Kitwana Mustafa.
Mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa mabanda ya maonesho Nyamazi Kanal Makame Abdalla Daima kutoka Jeshi la kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) amesema changamoto kubwa anayokabiliana nayo katika ujenzi huo ni kutokamilika kwa michoro na kukosekana kwa wakati mshauri elekezi wa Mradi, hata hivyo  amemuahidi Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa mwishoni mwa mwezi wa Kumi anatarajia kukabidhi kazi hiyo endapo changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Muonekano wa Eneo linalojengwa mabanda ya Maonesho Nyamazi Wilaya ya Magharibi "B" Unguja Mkoa wa Mjini Magaribi Unguja.  

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amewaagiza viongozi na watendaji wa wizara ya Biashara na Viwanda  kuhakikisha wanasimia vyema Mradi wa ujenzi wa Viwanja vya Maonesho ya Biashara eneo la Nyamanzi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kiwango kilichikusudiwa.                       

Akitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo huko Nyamanzi Wilaya ya Magharibi "B" Mhe. Hemed ameutaka Uongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa na kuwasisitiza kuwa  Maafisa watakaokwenda China kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa vya ujenzi wa mradi huo wana utaalamu na utambuzi wa Vifaa vyenye  ubora na Viwango vya hali ya juu ambavyo  vitadumu kwa muda mrefu.

Aidha amewaelekeza Mkandarasi na Mshauri elekezi wa mradi huo kuhakikisha  shughuli za ujenzi zinaendelea katika kipindi ambacho wanasubiri baadhi ya Vifaa vikamilike na kumtaka mshauri elekezi kuwepo katika eneo la ujenzi kwa muda wote ambao harakati za ujenzi zinaendelea ili kutoa ushauri atakapohitajika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amempongeza na kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussen Ali Mwinyi kwa maono na maamuzi yake ya kujenga Mabanda ya Maonesho ya Bishara katika Viwanja vya Nyamanzi ili kutoa fursa kwa Wafanyabiashara kufanya biashara zao katika mazingira mazuri yenye hadhi na mnasaba wa maonesho hayo.

Amesema Mabanda hayo yatakapomalizika yatotoa nafasi kwa wafanyabiashara kutangaza biashara zao kwa muda mrefu ikiwezekana  hata baada ya Sherehe za Mapinduzi maonesho hayo yaweze kuendelea.

Sambamba na hayo Mhe.Hemed amempongeza  Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa Viwanja vya Maonesho ya Biashara Nyamanzi ambae ni Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kwa kufanya kazi kwa uzalendo na kujitolea licha ya changacmoto mbali mbali zinazojitokeza katika ujenzi huo bado Mkandarasi  anafanya kazi kwa uharaka na ufanisi wa hali ya juu .

Nae Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban amesema Serikali kupitia Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imeamua kujenga Mabanda ya maonesho Nyamanzi ili kuboresha mazingira ya maonesho hayo,  kuwapa fursa wafanyabiashara  kuweza kujitangaza  na kuyafikia masoko ndani na nje ya nchi.

Amesema Wizara imejipanga kutatua changamoto yoyote itakayojitokeza ili kuhakikisha Mradi huo unamalizika kabla ya  mwezi Januari 2024 ili kutoa nafasi kwa maonesho ya kuadhimisha Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar  kufanyika katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo Kanal Makame Abdalla Daima kutoka Jeshi la kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) amesema changamoto kubwa anayokabiliana nayo katika ujenzi huo ni kutokamilika kwa michoro na kukosekana kwa wakati mshauri elekezi wa Mradi huo, hata hivyo  amemuahidi Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa mwishoni mwa mwezi wa Kumi anatarajia kukabidhi kazi hiyo endapo changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Kanal Daima Amesema dhamana ya ujenzi wa magazebo aliyopewa atahakikisha unamalizika kwa wakati na kuwaomba watendaji wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kufanya haraka kwa upatikanaji wa mantenti ili kurahisisha umalizikaji wa ujenzi wa mradi huo.

Mradi wa mabanda ya maonesho ya Biashara Nyamanzi utajumuisha Matenti kumi na mbili (12)  pamoja na vibanda vidogo vidogo Vya Biashara, Mahema ya wadhamini, Ukumbi wa wageni mashuhuri (VIP) na Tenti  kubwa la Ukumbi wa Mikutano litakalochukua watu zaidi ya 1500 ambalo litatumika kwa shughuli mbali mbali.

Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)

Trh. 02.10.2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.