Habari za Punde

Mhe Hemed mgeni rasmi kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya kukabiliana na Maafa Duniani


Viongozi na Taasisi mbali mbali zinazohusika na kukabiliana na Maafa wametakiwa kutoa uwelewa kwa jamii juu ya majanga na jinsi ya kutumia rasilimali zilizopo katika kujikinga na maafa ili kunusuru maisha ya Raia na mali zao.

 

Kauli hio imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipowahutubia Viongozi na wananchi katika kilele cha maadhimisho  ya siku ya Kimataifa ya kukabiliana na Maafa Duniani kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar. 

 

Amesema kuwa lengo kuu la kuadhimisha siku ya kukabiliana na Maafa ni kuihamasisha jamii pamoja na Taasisi mbali mbali kutekeleza wajibu wao katika kupunguza uwezekano wa kukumbwa na Maafaa pamoja na kukumbushana wajibu wa kuchukua hatua za kujikinga na majanga yanayosababishwa na binaadamu, kupunguza athari kwa majanga ya kimaumbile sambamba na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali baada ya kutokea maafa.

 

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa kuongezeka kwa matukio mbali mbali ya majanga yakiwemo ya matetemeko ya ardhi, upepo mkali, kuzama kwa meli na ajali za barabarani pamoja na majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika Visiwa vya Zanzibar yanasababisha  kuwepo kwa jamii kubwa tegemezi na yenye uwezo mdogo katika kukabiliana na kurejesha hali wakati na baada ya maafa kutokea.

 

Ametoa wito kwa Taasisi zote zenye miradi ya ujenzi kuhakikisha zinashirikina na Kamisheni ya kukabiliaba na maafa na kikosi cha Zima moto na Uokozi kabla, wakati na baada ya ujenzi ili kuhakikisha uwepo wa mipango na miundombinu ya kukabiliana na majanga .

 

Sambamba na hayo amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima pamoja na Jeshi la Polisi liendelee kusimamia sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka sheria hizo  pamoja na kukata bima  kwa wafanyabiashara, wamiliki wa vyombo vya usafiri na mitambo ili kuweza kurejesha hali pindi maafa yatakapotokea.

 

Aidha amezitaka Serikali ya Mikoa na Wilaya kusimamia ujenzi kwa mipango ili kuepusha ujenzi holela katika jamii hatua ambayo itasaidia kuweza kupambana na majanga yatakapotokea.

 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa Jitihada zao wanazozichukua panapotokea majanga ili kunusuru wananchi na Mali zao.

 

Amewataka wananchi kutumia namba za dharura 114 kwa Kikosi cha zima moto na uokozi na 190 kwa Kamisheni ya kukabiliana na maafa kwa kutoa taarifa zozote za Majanga ili kuzirahisishia Kamati za kukabiliana na Maafa kuweza kufika kwa muda kudhibiti maafa yanapotokea.

 

Kwa upande wake Muwakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Bi Dorothy Temu Usiri ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa unatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha wanakabiliana na Majanga yanapotokea pamoja na juhudi ya kuwa na Mpango wa kukabiliana na Mvua za El nino zinazotabiriwa kunyesha hivi karibuni.

 

Amesema utayari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa maendeleo unaendelea kuimarika ambapo Mashirika ya Umoja wa Mataifa yataendeleza kuunga mkono juhudi hizo ili kukabiliana na majanga ambayo yanachangia kuongezeka kwa umasikini Duniani.

 

Akiwasilisha Mada inayohusiana na ongezeko la majanga ya moto na mikakati ya kupunguza Msaidizi Mrakibu wa Zimamoto na Uokozo A.S.F Makame Omar Moh'd ameeleza kuwa Kikosi cha zimamoto na Uokozi kimeanza kujenga mabomba yatakayosaidia kudhibiti Moto kwa wepesi hatua ambayo itasaidia kurahisisha uzimaji wa moto utakapotokea hivyo, amewataka Wananchi kuilinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu na kuwafaa wengi zaidi.


Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar amefika kukagua Bweni la wasichana la Skuli ya Hasnuu Makame lililopo Kibuteni Mkoa Wa Kusini Unguja ambalo limeungua na Moto tarehe 12 Oktoba mwaka huu.

 

Mhe. Hemed ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha ukarabati wa bweni hilo unakamilika ndani ya miezi mitatu ili Wanafunzi waendelee kulitumia bweni hilo hasa wale ambao wanajiandaa na mitihani ya Taifa.

                

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

16 Oktoba,2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.