Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Uvuvi Duniani Yaadhimishwa Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipaata maelezo akitembelea mabanda ya maonesho wakati wa kuadhimisha Siku ya Uvuvi Duniani yanayoadhimishwa katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Jijini Zanzibar. akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipaata maelezo kuhusiana na ufugaji wa samaki wa kisasa kutoka kwa mkurugenzi wa (ZAFIRI) Dkt. Zakaria A. Khamis wakati alipotembelea mabanda ya maonesho katika sherehe za siku ya uvuvi duniani kwenye viwanja vya Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussen Ali Mwinyi amesema Serikali zote mbili zitaendelea kutekeleza kikamilifu Dira na Mipangonya Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, pamoja na Sera na Mikakati ya Maendeleo endelevu ya Sekta ya Uvuvi nchini.

Ameyasema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla katika sherehe ya siku ya Uvuvi Duniani iliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar.

Rais Dkt Mwinyi amesema katika kukuza na kuimarisha minyororo ya thamani ya Sekta ya Uvuvi na Mazao ya Baharini, Serikali itaendelea kupiga vita  Uvuvi haramu na kuvitaka  vyombo husika kuendelea kuchukua hatua zinazostahiki katika kupiga vita Uvuvi haramu.

Amesema kuwa uwepo wa siku ya Uvuvi Duniani inatokana na Tamko la Umoja wa Mataifa la kushajihisha Uvuvi endelevu wenye tija kwa wananchi hivyo Serikali zitaendelea kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia elimu, nyenzo, mitaji na masoko ili kuweza kujipatia ajira na kipato  kinachokidhi mahitaji.

Aidha Rais Dkt Mwinyi amesema serikali itaendelea kuwapatia vyombo na nyenzo za kisasa zitakazowawezesha  kuingia katika Uvuvi wa Bahari kuu pamoja na kuwawekea  miundombinu  iliyo bora ikiwemo ujenzi wa madiko ya kisasa, masoko na mitambo ya kuhifadhia samaki.

Sambamba na hayo Dkt Mwinyi amesema katika kuhakikisha sekta ya Uvuvi inafanikiwa zaidi Serikali zimejipanga kujenga viwanda vya kusarifia na kuchakata minofu ya samaki na dagaa pamoja na kuwekeza zaidi kwa  kuwawezesha wavuvi kufuga na kuzalisha samaki katika bahari na maji baridi.

Amesema kuwa kupitia programu ya Ahuweni ya UVIKO 19 ya Uchumi wa Buluu kwa Zanzibar jumla ya Boti 577 za uvuvi zimetolewa, Boti 500 wamepatiwa wakulima wa mwani, vifaa vya uvuvi kama vile mishipi, nyavu, GPS na fish finders, kamba na tai tai kwa wakulima wa mwani pamoja na kujengwa kiwanda cha kisasa cha kusarifia Mwani.

Kwa upande wake waziri wa Mifugo na Uvuvi  wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Abdalla Khamis Olega amesema wizara zote mbili zitahakikisha zinatoa fursa sawa kwa wavuvi wa pande zote mbili  kwa kuwapatia  vitendea kazi ili kuwaweza kuvua kisasa.

Amesema kwa Tanzania bara zaidi ya wavuvi  laki moja na tisiini na saba tayari wameshapatiwa leseni za Uvuvi wa Bahari kuu pamoja na kupatiwaa zana zote ambazo zitawasaidia kuvua kisasa sambamba na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Nae Mkurugenzi Mkaazi kutoka shirika la Chakula Duniani (WFP) Bibi Sara Golden Gipson  amesema WFP imekuwa ikichangia katika shuhuli za maendeo ya Uchumi wa Zanzibar hasa katika Sekta ya Uvuvi sambamba na kuwanyanyua wanawake kiuchumi kwa kuwajengea uwezo pamoja na kuwapatia miradi mbali mbali ya kimaendeleo.

Sara amesema WFP imekuwa ikiwasaidia wanawake katika kuhakikisha wanapiga hatua za maendeleo kwa kuwatatulia changamoto mbali mbali zinazowakabili katika shuhuli zao kama vile uhaba wa vitendea kazi hasa kwa wakulima wa mwani pamoja na kuwapatia maboksi ya kuhifadhia samaki kwa muda refu.

Mwakilishi huyo wa WFP ameishukuru Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaamini na kuwapatia mashirikiano katika kazi zao sambamba na  kuahidi  kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanziabar kwa kasi zaidi ili kuhakikisha malengo mkakati  ya Serikali kupitia Uchumi wa Buluu yanafikiwa.   

Katika sherere hiyo Mhe. Hemed alizindua vitabu mbali mbali kwa niaba ya rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ikiwa ni pamoja na Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar,  Mkakati wa Uchumi wa Buuu Zanzibar, Sera ya Uvuvi Zanzibar, Mkakati wa Uvuvi Zanzibar, Mpango Mkuu wa Uvuvi Zanzibar pamoja na Mpango kazi wa Ukondoishaji wa masuala ya Kijinsia katika Uchumi wa Buluu.

Mapema  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mhe Hemed Suleiman Abdulla   kwa niaba ya rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekagua mabanda ya maonesho ya shuhuli mbali mbali zinazofanywa na Wizara, Taasisi Binafsi na wadau wa Uvuvi katika sherehe ya  siku ya Uvuvi Duniani iliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa ndege  Zanzibar.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.