Habari za Punde

Taasisi za kiserikali zatakiwa kupeleka rasimu za mikataba kwa wakati

Kamati ya kudumu ya kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa kitaifa ya Baraza la Wawakilishi inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Machano Othman Said (aliyesimama mwenye Shati la Kitenge) akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Nchi (Ofisi ya Rais), Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora ambapo Kamati hiyo imefanya ziara ya kupokea Taarifa kuhusu utekelezaji wa Robo ya kwanza Mwezi Julai hadi Septemba, 2023 huko Mazizini- Zanzibar

Na Faki Mjaka-AGC ZANZIBAR

 

Kamati ya kudumu ya kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa kitaifa ya Baraza la Wawakilishi imezitaka Wizara na Taasisi za Serikali kuwasilisha kwa wakati Rasimu za Mikataba katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa ajili ya kupatiwa ushauri wa kitaalam.

 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Machano Othman Said ametoa wito huo katika majumuisho ya ziara ya Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa Robo ya kwanza Mwezi Julai hadi Septemba, 2023 kwa Wizara ya Nchi (Ofisi ya Rais), Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora huko Mazizini- Zanzibar

 

Amesema namna mzuri ya kuisaidia Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar ni kuhakikisha Taasisi za Serikali zinapeleka Miswaada hiyo hiyo kwa wakati ili ifanyie kazi kabla ya kufunga Mikataba hiyo kwa faida ya Taasisi hizo na Serikali kwa ujuma.

 

Mh. Machano amesema Miswaada inapochelewa kufika katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu, hupelekea changamoto mbali mbali ikiwemo kuwapa mzigo mzito wa Majukumu Watendaji wanaoipitia Mikataba hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Mikata ni mingi na inahitaji kufanyiwa kazi kwa utulivu.

 

Akiwasilisha Ripoti ya Utekelezaji mbele ya Kamati hiyo Mwanasheria Mkuu Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji amesema, katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2023, Afisi iliandaa jumla ya Miswada Minane (8) ambapo Miswada Saba (7) iliwasilishwa Baraza la Wawakilishi katika kikao cha mwezi wa Septemba, 2023 kwa kusomwa kwa mara ya kwanza.

 

Katika suala la usimamizi wa Mikataba, Mwanasheria Mkuu huyo amesema Katika kipindi hicho, jumla ya Mikataba Mia Mbili Ishirini na Nane (228) imetolewa ushauri kati ya hiyo Mikataba ya Bidhaa na Huduma (138); Mikataba inayohusiana na Ujenzi (42); Mikataba inayohusiana na Ushauri Elekezi (40) na Mikataba inayohusiana na Kodi (Lease) minane (8).

 

Aidha,Dkt. Mwinyi amesema Afisi iliendelea kutoa ushauri wa kisheria katika Hati za Maelewano (MoUs) ambapo jumla ya Hati za Maelewano Sabini na Nane (78) zimetolewa ushauri kwa kipindi cha Julai – Septemba 2023 katika sekta ya Elimu, Uchumi, Usafiri, Utalii, Makaazi, Afya, Ardhi, Ujenzi, Teknolojia, Kilimo, Utamaduni, Sheria, Mazingira na Fedha.

 

Awali Waziri Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais), Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mwalim Haroun Ali Suleiman aliishukuru Kamati hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya huku akiwataka Watendaji wa Wizara yake kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao ili kuihudumia Jamii na kufikia maendeleo wanayoyatarajia.

Awali Kamati hiyo ilifanya ziara katika Taasisi za Wizara ya Nchi (Ofisi ya Rais), Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora ili kupokea Taarifa ya utekelezaji wa Robo ya kwanza Mwezi Julai hadi Septemba, 2023.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.