Habari za Punde

TUZO kwa Waandishi wa Habari za Takwimu za Wanawake na Uongozi Zanzibar (Champion Data Journalism Award in Zanzibar)

 CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAZELA) na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) kupitia   mradi  wa kuinua  Wanawake na Uongozi,  wanatangaza tunzo maalum ya uandishi wa habari za Takwimu za wanawake na uongozi ikiwa ni katika maadhimisho   ya   kuelekea  siku  ya wanawake   duniani  ambayo   kitaifa  huadhimishwa   kila   ifikapo    machi   8  duniani  kote.

Tunzo  hizo   ni  muendelezo       wa  shughuli  zinazofanywa    na  mradi  wa  kuinua  wanawake  na uongozi   kufikia   50/50  katika   ngazi  zote  kupitia   tasnia   ya  habari, kwa  kuwashajiisha   waandishi   wa habari   kutoka  vyombo    mbali  mbali   vya  habari  ikiwa na lengo la kutumia vyombo vya habari katika kushajiisha masula ya wanawake na uongozi na kutanabahisha jamii na Taifa kwa ujumla umuhimu wa wanawake kuwemo katika nafasi za uongozi ili kukuza na kuimarisha demokrasia.

Tunzo hii itahusisha kazi zilizotolewa katika vyombo vya habari vya aina nne (4) kama ifuatavyo:

Uandishi wa habari za Makala katika magazeti (feature articles)

Uandishi wa habari wa vipindi katika redio (radio program)

Uandishi wa habari katika Televisheni (TV program)

Uandishi wa habari wa makala katika mitandao ya kijamii (feature articles in social media story).

Hivyo, TAMWA ZNZ na washirika wake  inawaalika waandishi wa habari kukusanya kazi zao au kuandika katika eneo hilo na  kuziwasilisha kwa wakati.

Vigezo muhimu vya kuzingatia wakati wa kuandaa au kuwasilisha habari ni:

Ubora wa kazi iliyowasilishwa

Upekee wa mada

Umuhimu wa kuzingatia uwiano sawa wa jinsia.

Vyanzo vingi vya habari vilivyojitawanya.

Ubunifu wa mada husika.

Matokeo baada ya kutoka habari au kipindi hicho (impact)

Uwasilishaji wa mada husika

Mpangilio wa mada

Ufasaha na mtiririko wa lugha

Kuzingatia maadili ya uandishi wa habari

Uweledi na matumizi ya TAKWIMU.

Kipindi cha Redio na Television kisizidi dakika 30 na pia sauti na picha ziwe katika ubora unaostahiki.

Kipindi au makala iliyochapishwa au kurushwa HEWANI katika vyombo mbali mbali vya habari vikiwemo magazeti, runinga, redio na mitandao ya kijamii katika kipindi cha kuanzia Januari 1  hadi Disemba 31, 2023.

Kazi ziwasilishwe katika ofisi ya Chama cha ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) Tunguu karibu na IPA na Kwa Pemba kazi ziwasilishwe katika ofisi ya Tamwa Chake chake  Pemba.

Hii  ni  mara   ya   tatu   kufanyika  tunzo ya aina hii ambapo   mwaka   jana   jumla   ya  waandishi   kumi   walishinda  tunzo za  umahiri   kwa   upande  wa  magazeti   na    mitandao  ya jamii.

Hata hivyo imebainika kuwa katika kufanyika kwa tunzo hio kuna changamoto na mafanikio kadhaa yaliyojitokeza.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:

Waandishi kuzingatia zaidi kuandika makala na vipindi ambavyo ni vya matukio ambavyo vimekuwa vinawalenga zaidi viongozi au matokeo ya semina na mikutano.

Kuandika makala au vipindi  ambavyo havikuwa na vyanzo tofauti vya habari na hivyo kukosa maoni ya watu wengi zaidi.

Makala hazikuwa na mvuto au mtiririko maridhawa na hivyo kukosa ubunifu na kuzifanya hazivutii.

Makala na vipindi havikuzingatia makundi mengine ya pembezoni wakiwemo walemavu, wanawake na wale wanaoishi vijijini.

Uwepo na ushiriki mdogo sana katika vipindi vya Televisheni.

Makala na vipindi vya habari vya uchunguzi wa kina vilikuwa navyo ni vichache sana.

Picha na sauti katika vipindi vya redio na Televisheni havikuwa katika ubora na baadhi vilikuwa havifunguki.

Hata hivyo pamoja na changamoto hizo bado kulikuwa na mafanikio:

Kuibua vipaji vya waandishi chipukizi na kuonekana ni kwa jinsi gani waandishi hao wamejitahidi katika kuweza kufikia viwango vinavyotakiwa.

Ushiriki wa waandishi wengi zaidi ambao wako katika rika tofauti chipukizi na wazoefu.

Mashirikiano ya pamoja kwa wadau wa habari na kuzifanya tunzo hizi kuwa na mvuto na kuzitangaza kwa kina.

Mwisho katika kuimarisha kada ya habari tunatoa wito maalum kwa wanahabari kujiendeleza zaidi katika fani na pia kutoa wito maalum kwa taasisi za habari pamoja na vyombo vya habari kuimarisha mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa waandishi wa habari.

Waandishi wa habari tufahamu kuwa kazi hii ni kusaidia jamii na hivyo ni muhimu kutumia kalamu na vipaaza sauti katika kuelimisha na kuibua kero na sauti za wasio na sauti.

Ni muhimu kwa waandishi na wahariri kuimarisha kada hii kwa kufuata kwa vitendo maadili ya habari lakini wito kwa wahariri kuwasaidia waandishi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Natoa shukuran kwa waandishi kwa kuendelea na majukumu yao na kutoa wito kwa ushiriki zaidi katika mashindano haya kwa lengo la kuimarisha kada ya habari lakini pia katika kuandika habari za takwimu za wanawake na uongozi.

“KALAMU YANGU MCHANGO WANGU KWA WANAWAKE”.

Imetolewa na:

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ)

 Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA)

 Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.