Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Ajumuika na Wananchi Katika Ibada ya Sala ya Ijumaa Masjid Noor Kwa Hajitumbo Wilaya ya Mjini Unguja

Waumini wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kujipanga kwa kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum wakiwemo mayatima, wajane na watu wasiojiweza hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhan unaotarajiwa kuwafikia hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid NOOR kwa HAJI TUMBO  mara baada ya kumaliza  Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema ni lazima wazanzibari na waumini wa dini ya kiislamu kuendeleza utamaduni wa kusaidiana pamoja na  kuwasaidia watu wasio na uwezo ili kuweka usawa baina yao hasa katika mwezi mtukufu wa ramadhani mwezi ambao una fadhila nyingi sana ndani yake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza kuwa mwezi wa Ramadhani umeshakaribia hivyo ni wajibu kwa waumini wa dini ya kiisalmu na wazanzibari kwa ujumla kuuendeleza yale yote ambayo waliokuwa wakiyafanya miezi yote kumi na moja (11) ambayo yanamfurahisha mwenyezimungu ikiwemo kutoa kile ambacho wameruzukiwa na Allah (S.W) kwa wanao hitaji ili kupata fadhila zake.

Alhajj Hemed amewataka waumini na  Wazanzibari kuzidisha imani kwa viongozi wao ambao wanawaongoza na kuahidi kuwa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwaenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kutatua changamoto zote zinazowakabili wananchi wake.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewashukuru waumini na wazanzibari wote kwa ujumla kwa kuendelea kuishi kwa amani na utulivu jambo ambalo ndio dira ya maendeleo ya Taifa kwani kufanya hivyo ndio kunakopelekea Serikali kufanya yale yote iliyoyaahidi kwa wanachi wake kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Ustadh, TWAHIR ALI  amewataka waumini wa Dini ya Kiislam kuamini kuwa kila anachokifanya mwanadamu atalitwa kulingana na matendo yake hivyo ni lazima kuzidisha Ibada hasa katika kipindi hichi Cha kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Ustadh Twahir amewasisitiza waumini kuwa na subra kwa kila jambo ambalo muumini linamtokea kwani kufanya hivyo ndio kufata nyayo za mitume wote ambalo walioletwa kuja kuitangaza dini ya mwenyezi mungu sambamba  na kuyaacha yale yote ambayo yanamkirihisha Allah (S.W)

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe..16.02.2024

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.