Habari za Punde

Waziri Mhe Makamba Amwakilisha Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan Mkutano wa AWLN

Waziri Makamba amwakilisha Rais Samia AWLN Tanzania inaungana na Viongozi Wanawake Afrika (AWLN) pamoja na Umoja wa Afrika (AU) katika jitihada za kuwainua mabinti na wanawake kwenye nafasi mbalimbali za uongozi Afrika pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa mabinti na wanawake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba ameyasema hayo katika Mkutano wa AWLN Addis Ababa, Ethiopia usiku huu ambapo alimwakilisha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwenye hotuba iliyosomwa na Waziri Makamba, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza AWLN kwa kuingia ubia na Umoja wa Afrika akiamini kuwa ubia huu utachangia katika kutengeneza wanawake wenye ujuzi na uwezo mkubwa katika uongozi ndani na nje ya Bara la Afrika, alieleza Mhe. Makamba. 

Kwa upande wa biashara na uwekezaji, Mhe. Rais Samia anakuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwani anaamini kuwa ni eneo ambalo wanawake na wasichana wana uwezo wa kufanya vyema endapo watawezeshwa. 
 
Tayari Tanzania imewawajumuisha wajasiriamali wanawake katika Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), ambapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kutoa hamasa na kuchangamkia fursa kwa makundi haya muhimu ya jamii. 
 
Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi wengine wakubwa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde, Mhe. Ellen Johnson Sirleaf, Rais Mstaafu wa Liberia na mwanzilishi wa AWLN pamoja na viongozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.