Habari za Punde

ZHSF Kuanza Huduma Rasmi Katika Mwaka Mpya wa Fedha 2024/2025

Na.Takdir Ali. Maelezo Zanzibar.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidhi amesema Serikali kupitia Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) unakamilisha taratibu za kimkataba baina ya ZHSF na NHIF ili kuwawezesha wanachama wa ZHSF kupata huduma Tanzania Bara.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Paje Mhe. Dkt. Soud Nahoda Hassan huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi ‘‘B’’.


Amesema iwapo makubaliano ya kimkataba baina ya ZHSF na NHIF yatashindikana ZHSF imepanga kuingia mkataba na vituo vya Afya vya Tanzania Bara ili kuweza kuwapatia huduma wanachama wake walioko huko na watakaokwenda Tanzania Bara kwa kazi maalum au matembezi.


Amefahamisha kuwa Mfuko umejipanga ifikapo mwaka mpya wa fedha 2024/2025 kuanza rasmi matibabu Tanzanisa Bara, kwa kufikia makubaliano na NHIF au kwa kuingia Mkataba na vituo vya Afya.


Aidha amesema Serikali itahakikisha Wafanyakazi wote wanapatiwa huduma hizo kwa mujibu wa mipango ilioandaliwa.


Hata hivyo ametoa taarifa kwamba baadhi ya wafanyakazi hao wanaendelea kupata huduma hizo kupitia NHIF kwa ZHSF kuwalipia michango yao.


Mbali na hayo amesema kwa wale wachache waliokua si wanachama wa NHIF kabla ya kuanzishwa ZHSF tayari mazungumzo yamefanyika na NHIF na mwelekeo ni kwamba watasajiliwa na kuweza kupata huduma huku ZHSF ikijipanga kuanza rasmi kuwapatia huduma wanachama wake Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.