Habari za Punde

Simamieni Maadili ya Jamii

 

Na Koplo Issa Mwadangala-Polisi Songwe.

Wazee wa mila na waganga wa tiba asili Kata ya Saza Wilaya na Mkoa wa Songwe wametakiwa kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika usimamizi wa maadili na sio uvunjifu wa maadili unaopelekea jamii kujiingiza katika uhalifu kama ubakaji, mauaji, na imani za kishirikina jambo ambalo linaleta ukosefu wa amani katika jamii.

Hayo yamesemwa Machi 25, 2024 na Polisi Kata wa Kata ya Saza Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mussa Masumbuko wakati alipoongea na wazee wa mila na waganga wa tiba asili wa Kata hiyo ili kuwajengea uelewa wa namna gani wataendesha majukumu yao pasipo kuvunja sheria za nchi yetu.

"Nyinyi ndio mnaoweza kuitengeneza jamii yetu ikawa na muamko mzuri katika kupiga vita imani potofu za kishirikina pamoja na kuondokana na mawazo hasi ya kuamini kuwa kupitia kuziamini nguvu za giza ndio njia pekee ya kupata mafanikio ya haraka" alisema mkaguzi huyo.

Pia amewataka wazee hao wa jadi na waganga wa tiba asili kutotoa huduma zao kupitia njia zinazovunja sheria za nchi yetu.

Kauli hii imekuja baada ya kuonekana makosa mengi ya udhalilishaji na mauaji yanayoripotiwa kituo kidogo cha Polisi cha Saza kuonekana mengi yanahusishwa na imani za kishirikina.

"Tumieni njia zisizoleta uvunjifu wa sheria pia msiwape wateja wenu masharti ambayo yanaenda kupelekea uvunjifu wa sheria, mfano si mmeona tukio la juzi la mtoto mdogo kubakwa mwenye umri wa miaka 04 kweli hapo hakuna imani potofu? niwaulize nyie wazee wa mila, hebu ifike mahali muwe na utaratibu mzuri wa kuendana na wakati na usasa katika tiba zenu ili jamii ipate kuelimika na kuondokana na imani hizi mbaya na potofu" alisisitiza mkaguzi huyo.

Baada ya Elimu hiyo wazee wa mila na waganga wa tiba asili walionesha hamasa na nia ya kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa wengine wa maeneo mbali mbali ili waweze kutoa tiba kwa njia iliyo bora zaidi na isiyovunja amani na sheria za nchi zetu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.