Habari za Punde

DKT.DIMWA - ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO JIMBO LA KWAHANI

Na.Mwandishi Wetu  Zanzibar..

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, amesema mshikamano,umoja na upendo ndiyo msingi wa maendeleo ya kufanikisha ushindi mkubwa wa Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.


Hayo ameyasema wakati akihutubia Wana CCM katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo la Kwahani kwa ajili ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka mwaka 2020/2025, uliofanyika Tawi la CCM la Muungano huko Unguja.


Dkt.Dimwa,alisema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwa na nguvu na imara endapo wanachama wake watakuwa wamoja na wenye msimamo usioyumba katika kulinda na kusimamia maslahi ya Chama.


Alisema kila mwanachama kwa sasa anakiwa kujiandaa kikamilifu kutekeleza kwa vitendo ibara ya tano(5) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 inayoelekeleza kupatikana kwa ushindi wa ngazi zote kwa Zanzibar na Tanzania bara kwa ujumla.


 “Tunapoelekea katika kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 lazima tuwe  na Jeshi moja lenye nguvu ya kupambana kikamilifu vita ya kisiasa na kuhakikisha tunashinda na kupata majimbo yote na Viti vyote vya Urais kwa Zanzibar na Tanzania bara.


Tukiwa wamoja hata wapinzania na makundi mengine ya watu wasiyoitakia mema CCM na nchini kwa ujumla watashindwa kutugawa kwani tutakuwa imara zaidi na hakuna wa kupenya wala kuingilia mikakati yetu”, alisema Dkt.Dimwa.


Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo,aliwapongeza viongozi wa Jimbo la Kwahani ambao ni Mwakilishi,Mbunge na Madiwani kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa ahadi walizotoa katika Jimbo hilo zinazoendana na mahitaji ya wananchi.


Kupitia mkutano huo alihimiza ubunifu,uchapakazi na utamaduni wa kufanyika kwa vikao vya kikanuni kuanzia ngazi za Mashina hadi Jimbo kwa lengo la kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali ya Changamoto na mafaniko ili kufikia maamuzi ya pamoja katika kumarisha Chama na Jumiya zake.


Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar Dkt.Dimwa,aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ambayo ndio kibali cha kuiletea ushindi wa kishindo CCM katika uchaguzi Mkuu ujao.


Pamoja na mambo mengine Dkt.Dimwa,kwa niaba ya Viongozi wa Jimbo aligawa sadaka ya futari kwa wanachama na wananchi wa Jimbo hilo zikiwemo mchele,mafuta ya kula,tende,unga wa ngano,mayai na sukari ili viwasaidie katika mfungo wa mwezi huu wa Ramadhan.


Mapema akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Talib Ali Talib, alieleza kuwa Jimbo hilo ni mfano wa kuigwa kwani viongozi wake wamekuwa wabunifu katika kutatua changamoto za wananchi.


Naye Mbunge wa Jimbo la Kwahani Mhe. Ahmada Yahya Abdulwakil,alisema ametumia zaidi ya shilingi milioni 354 katika kufanikisha masuala mbalimbali ya kijamii na uimarishaji wa miradi ya CCM ndani ya Jimbo hilo.


Pamoja na hayo alisema kwa ushirikiano wa viongozi wote wa jimbo hilo wanatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Jengo la ghorofa moja litakalotoa huduma mbali mbali zikiwemo Kituo cha Kisasa cha Mafunzo ya ujasiriamali kitakachogharimu kiasi cha milioni 450 hadi kukamilika kwake.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe. Yahya Rashid Abdulla, alisema ametumia zaidi ya milioni 200 katika kutatua changamoto za wananchi pamoja na kuimarisha miradi ya Chama ya ukarabati wa Ofisi za Matawi,Maskani na Ofisi ya Jimbo ili ziendane na hadhi ya Chama Cha Mapinduzi.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.