Habari za Punde

Waumini wa Dini ya Kiislam Watakiwa Kuendelea na Mema Waliyokuwa Wakiyafanya Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akimsalimia na kumjulia hali yake Sheha wa Shehia ya Muungano Mhe. Kitwana Mustafa  alipofika nyumbani kwake eneo la mtaa wa muungano

Waumini wa dini ya kiislamu wametakiwa kuyaendeleza mema waliyokuwa wakiyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuendelea kupata radhi za Allah (S.W) na kupata fadhila katika maisha yao yote watakayoishi hapa duniani.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid MBUYUNI uliopo MALINDI Wilaya ya Mjini  mara baada ya kumaliza  Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Alhajj Hemed amesema ni wajibu wa kila muislamu kuhimizana katika kufanya Ibada  na kukatazana maovu katika miezi yote ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu sambamba na kuzijenga jamii zetu katika kufanyiana wema na kusaidiana kwa kila hali.

Aidha Alhajj,Hemed amewasisitiza wazazi na walezi kutimiza wajibu wao katika kuzilea familia zao ili kuwakinga na matendo maovu na machafu yakiwemo matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto jambo ambalo linaiathiri jamii ya kizanzibari.

Sambamba na hayo  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla kuzidi kudumisha Amani na Utulivu uliopo nchini ili kuzidi kupata maendeleo na kuiwezesha Serikali kutekeleza waliyoyaahidi kwa wananchi wake kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.

Aidha amewataka waumini kuzidi kuwaombea dua viongozi wakuu wa nchi pamoja na kuiombea nchi iweze kupata maendeleo pamoja na kujikinga na mabalaa mbali mbali ambayo yanadumaza upatikanaji wa maendeleleo nchini.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Imamu Mkuu wa Mskiti wa Mbuyuni Shekh FARIDI HADI AHMED  amewataka waumini wa Dini ya Kiislam kuendeleza kufanya amali njema walizokuwa wakizifanya ndani ya  mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuachana na  maovu yanayomkirihisha ALLAH (S.W).

Amesema kuwa waislamu ni lazima kufanya matendo mema kwa taqwa huku wakitarajia kupata fadhila kutoka kwa Mwenyezi mungu (S.W) sambamba na kuacha kujiingiza katika matendo maovu ili kujakupata hasara hapa duniani na kesho Akhera.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed amefika nyumbani kwa Sheha wa Shehia ya Muungano Mzee Kitwana Mustafa na kumjuulia hali pamoja na kumuombea dua kwa Mwenyezimungu amjaalie apone haraka ili aweze kuendelea na majukumu ya kikazi na kifamilia.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.