Habari za Punde

Waandishi wa Habari Wajengewa Uwezo Uandishi wa Habari za Usawa wa Jinsia na Michezo

Na Fauzia Mussa- Habari Maelezo 15,mei,2024

WAANDISHI wa habari wameshauriwa kuandika habari zitakazowashajiisha madaktari na wauguzi kusomea pia elimu ya tiba ya michezo ili kuwezesha wanamichezo wanawake kuhudumiwa na wataalamu wa jinsia sawa ili kulinda heshima yao.

Akitoa somo kuhusu uandishi na jinsia katika warsha ya mafunzo kwa wanahabari inayofanyika katika ofisi za TAMWA Zanzibar huko Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, muwezeshaji Salum Vuai, alisema uhaba wa madaktari wanawake katika sekta ya michezo, kunaweza kuleta athari pale wachezaji wanapoumia na kutibiwa na wanaume wasiokuwa waaminifu na waadilifu.

Alisema kupatikana kwa idadi kubwa ya madaktari wanawake michezoni, kutawajengea imani wanamichezo wa jinsia hiyo na hivyo kushiriki bila ya hofu na wasiwasi wa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

“Hili ni jambo la msingi kwani dunia sasa imebadilika, ni wanaume wachache wenye moyo wa kuhudumia wanamichezo wanawake kwa dhati. Iko haja kuongezeka madaktari wanawake katika tiba ya michezo ambayo pia ni taaluma inayipaswa kusomewa,” alifaahamisha.

Alisema jamii imekuwa na hofu kubwa kuwaruhusu watoto au ndugu zao wa kike kushiriki michezo wakishindwa kuwaamini walimu na hata madaktari wanaume, na kuongeza kuwa ni muhimu kulinda mila, silka, desturi na tamaduni za Mzanzibari.

Kwa upande mwengine, alishauri kuanzishwa au kufufuliwa kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo, ili kuibua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo ambazo zimekosa jukwaa la kuzibainisha ili zipatiwe ufumbuzi.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kujitokeza vitendo viovu wanavyofanyiwa wanamichezo na baadhi ya wanajamii ikiwemo kauli za kuwakejeli waamuzi wanawake wanaoamua kujifunza uchezeshaji.

Aidha alisisitiza waandishi kuzieleza wazi changamoto zinazowakabili wanamichezo wa timu za watu wenye ulemavu, ambao wanakosa usimamizi na jamii kuwaficha ndani hali inayowapa wajione wanatengwa.

Mtaalamu wa masuala ya michezo wa shirika la maendeleo ya michezo kutoka Ujerumani (GIZ) Makame Amir Mgeni, ameeleza kuwa faida zinazopatikana katika sekta ya michezo ni kumkuza mchezaji kiafya na kuimarisha uwezo wake wa kiakili na masomo.

Alisema umefika wakati kwa waandishi wa habari kujipangiai agenda ya kumuwezesha mwanamke kufika mbali kimichezo.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo Bi. Hawra Shamte, akielezea tathmini ya michezo na hali ya jinsia, alisema Serikali inaizingatia sekta hiyo ikijua umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi.

Alisema Serikali inaendelea kuweka mikakati katika kushughulikia tofauti za kijinsia, hivyo aliwashauri waandishi kuwahamaisha wanawake kushiriki katika michezo kwa maendeleo.

Aliitaja Sera ya Michezo ya mwaka 2018 kuwa miongoni mwa hatua za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,katika kutekeleza mikakati na mabadiliko yanayohusu michezo.

Aidha aliwataka waandishi kushajiisha wanawake wanaoshiriki michezo kujilinda na kujiheshimu Ili kulinda hadhi yao mbele ya jamii.

Mradi wa michezo na maendeleo umepangwa kuchukua mwaka mmoja ukilenga kukuza usawa wa jinsia katika sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.