RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesifu mafanikio
makubwa ya hati safi zilizowasilishwa kwa serikali, kufuatia taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, (CAG) na kuzitaka taasisi na
Mashirika ya Umma zenye hati zzilizo na dosari kujitathmini na kuzifanyia kazi
ili mapungufu yasiendelee kujirejea.
Rais Dk. Mwinyi ameyaeleza hayo
alipozungumza kwenye viwanja vya Ikulu, Zanzibar baada ya kuwasilishwa kwa
taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, (CAG), Dk.
Othman Abbas Ali.
Alisema, pamoja na
mapungufu na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa kuchukuliwa hatua
mbalimbali ili kufaya vizuri zaidi siku za usoni, alisifu hati za ukaguzi safi
kwa serikali, kwa kufikia kiwango cha asilimia 95.4 na kueleza kuwa ni
mafanikio makubwa kwa Serikali.
Akizungumzia
mapungufu yaliyojitokeza kwenye ripoti hiyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza baadhi
yao ni ya kiutawala na mengine ya kiutendaji yanayohitaji ufumbuzi wa
kiutawala.
Hivyo, amemuagiza Katibu
Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Ahmeid Said
kuunda Kamati maalumu itakayoshughulikia kasoro hizo ili kuzifanyia kazi.
Alisema, sio kila
kasoro zilizomo kwenye Ripoti ya CAG ni za kijinai, nyengine zipo za Kiutendaji
zinahitaji ufumbuzi wa Serikali na zile za kijinai zitakabidhiwa kwa Mamlaka ya
Kudhibiti na Kuhujumu Uchumi, Zanzibar (ZAECA) kwa hatua za kisheria.
Dk. Mwinyi, alizionya
baadhi ya taasisi za Serikali kuingia kwenye mikataba ya utekelezaji wa miradi
ya Serikali bila kuishirikisha Ofisi ya Mwanashiria Mkuu wa Serikali jambo
alilolieleza kuwa ni kosa kisheria.
Hata hivyo, aliwataka
viongozi wa Serikali wa ngazi zote, kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Zanzibar panapokua na
wajibu wa kufanya hiyo.
Mapema, akiwasilisha
ripoti yake, CAG Dk. Othman Abbas Ali, aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kuwa na mifumo michache itakayodhibiti siri za serikali pamoja na
mapato ya serikali yasipotee.
Akizungumzia kasoro
za baadfhi ya Mashirika ya Umma na kampuni zinazoendelea kujiendesha kwa hasara
kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, Dk. Abass alisema mashirika hayo huathiri
mitaji ya Serikali iliyoekezwa pamoja na kuwa na mitaji hasi hali
inayosababisha taasisi hizo kutegemea mikopo na ruzuku kutoka serikalini
kwajili ya kujiendesha na kushindwa kulipa gawio kwa serikali.
Dk. Abass, pia alieleza
ukaguzi huo ulibaini kasoro kwa mashirika na kampuni hizo kutokuwa na ufanisi
wa utoa huduma na hayaendani na malengo na mkakkati yaliyojiwekea kwa ushindani
na taasisi nyengine binafsi.
Akiyataja Mashirika
na kampuni hizo Dk. Abass alisema ni pamoja na Shirika la Magazeti ya Serikali
ya Zanzibar (SMS), Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Kampuni ya Maendeleo
ya Uvuvi, Kampuni ya mafuta na Kampuni ya ujenzi Zanzibar.
Aidha, aliishauri
Serikali kuwa na mashirika machache yenye uwezo wa kujiendesha wenyewe na kutoa
gawio kwa Serikali.
Akizungumzia ukaguzi
wa awali wa mafao ya kiinua mgongo na pesheni, Dk. Abass alieleza ripoti hiyo ilibaini
asilimia 28 ya upotevu wa fedha za Umma zilizokokotolewa kwa mafao ya mishahara
ya watumishi waliokwishastaafu.
Alisema kasoro hizo
zilijitokea baada ya mfumo wa “Payroll” kushindwa kuzuia utaratibu wa ugawaji
wa mishahara hiyo na kuendelea kuitia hasara Serikali kwa upotevu wa fedha za
Umma kwa baadhi ya watumishi hao kushindwa kuwekewa kizuizi cha mishahara na
kuendelea kupokea mishahara wakati tayari walishahtaafu, miongoni mwa dosari
hizo Dk. Abbasi alisema zilitokea kwa Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar, Chuo cha Mafunzo, Kikosi cha cha Kuzuia Magendo
KMKM, Kikosi cha Zimamoto na uokozi pamoja na Wizara Nchi Tawala za Mikoa na
Vikosi Maalum vya SMZ..
Hivyo, CAG, aliishauri
serikali kuwana mifumo michache itakayokuwa na tija kwao kuliko kuwa na mifumo
mengi inayoitia hasara serikali sambamba na kuacha kubuni mifumo mipya
isiyokuwa na uwezo wa utatuzi wa changamoto za kimifumo juu ya changamoto za
serikali.
Jumla ya ripoti nane zilikabidhiwa
Serikali ikiwemo ya Serikali Kuu (Mawizara na taasisi zote).
Kifungu cha 112 (5)
kinamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, awasilishe
taarifa yote aliyoikagua na aikabidhi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi kwa hatua nyengine na baadae Rais Dk. Mwinyi alimkabidhi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun
Ali Suleiman ambae nae ataikabidhi kwa Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa
takwa la kikatiba kwaajili ya kujadiliwa.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment