Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Amejumuika na Wananchi Katika Ibada ya Sala ya Ijumaa Masjid Mushawar Muembeshauri Zanzibar

                                         

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia Waumini wa Masjid MUSHAWWAR uliopo Muembe Shauri Wilaya ya Mjini mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanawavalisha watoto wao mavazi yenye stara yanayoendana na mila za kizanzibari kwa kipindi chote cha skukuu na siku nyengine ili kuwaepusha na udhalilishaji kutoka kwa watu wasio na nia njema kwao na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati alipokuwa akiwasalimia Waumini wa Masjid MUSHAWWAR uliopo Muembe Shauri Wilaya ya Mjini mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha anamvisha mtoto wake mavazi yanayoendana na maadili ya kizanzibari na kuwa waangalifu kwa watoto wao wakati wanapowapeleka sehemu za matembezi hasa katika kipindi hiki cha skukuu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa matendo mengi maovu yakiwemo ya udhalilishaji kwa watoto hutokea wakati wa skukuu hivyo ni lazima kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawasimamia vyema vijana wao ili waendelee kuwa salama wakati wote wa skukuu na baada ya skukuu.

Alhajj Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kupambana na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji ambapo amewataka wananchi kuuungana  na Serikali katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji hasa wa watoto ambao ndio nguvu kazi ya Taifa  hapo baadae.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewashukuru  wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kuitunza na kuidumisha amani na utulivu iliyopo nchini inayopelekea kufanya ibada kwa utulivu pamoja na shuhuli nyengine za kimaendele ambayo chanzo chake ni kuwepo kwa anani na utulivu nchini.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi kuendelea kuwaombea dua waumini walioko nchini Makka wanaendelea na ibada ya Hijja kuweza kufanya ibada hio kwa amani huku wakitarajia kupata ujira ulio bora  kutoka kwa Allah (S.W) sambamba na kuwataka walio na uwezo kujiandaa kwenda kufanya Ibada ya Hijja mwakani panapo majaaliwa.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Ustadh ALI  ABDUL- RAHMAN amewataka waumini wa dini ya Kiislam kuhakikisha wanakisirisha kufanya ibada kwa wingi hasa katika masiku kumi (10) bora ya mfungo Tatu (3) huku wakitarajia kupata fadhila nyingi kutoka wa Allah (S.W)

Amesema kuwa kumekuwa na kutofautiana katika suala la funga ya sunna ya Arafa hivyo amewataka waumini kuisoma dini  pamoja na kufuata maneno ya wanazuoni ili kuondosha tofauti zao hasa katika masuala mbali mbali ya dini ikiwemo kuandama kwa mwezi.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.