Habari za Punde

Zanzibar Itaungana na Dunia Kuimarisha Siku ya Wachangiaji Damu Juni 14,2024

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe Nassor Ahmed Mazurui akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu ambayo hufanyika juni 14 duniani kote,hafla iliyofanyika makao makuu ya damu Salama Sebleni Wilaya ya Mjini.

Afisa uhusiano kitengo cha damu salama  Usi Bakar Mohammed akichangia katika mkutano na waandishi wa habari uliohusiana  na maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu ambayo hufanyika juni 14 duniani kote,hafla iliyofanyika makao makuu ya damu Salama Sebleni Wilaya ya Mjini.

Picha na Fauzia Mussa - Maelezo Zanzibar.

Na Fauzia Mussa –Maelezo

Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazurui amewataka wananchi  wenye sifa za kuchangia damu kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu ili kusaidia upatikanaji wa  damu Nchini.

 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na maadhimisho hayo Waziri Mazrui amesema Zanzibar itaadhimsha  siku hiyo  ifikapo juni 14 katika Makao Makuu ya Benki ya Damu Salama, Sebleni Wilaya ya Mjini kama inavyoadhimishwa  Duniani kote kwa lengo la kuwapongeza wachangiaji damu kwa ujasiri wao wa kujitolea kuokoa maisha ya wengine.

 

Amefahamisha kuwa  kila mmoja ni muhitaji wa damu hivyo ni vyema kuweka akiba kabla ya kusubiri dharura kutokezea na kuwaomba wachangiaji kuendelea na mwendo huohuo ili kuhakikisha benki hiyo inakuwa na damu ya kutosha kuweza kukidhi mahitaji .

  

Ameeleza kuwa jumla ya maombi ya damu 38,595, yalipokelewa kutoka Hospitali zinazotoa tiba ya damu ambapo benki ya damu salama iliweza  kusambaza damu 19,785 sawa na asilimia 51 ya maombi, hivyo ni vyema ipo haja ya kuongeza kasi ya uchangiaji ili  kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji tiba ya damu hospitalini.

 

“Sababu kubwa zinazopelekea kuhitaji tiba ya damu ni pamoja na kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua,ajali, tiba ya upasuaji pamoja na upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka 5 wenye kuugua maradhi ya mifupa” alifahamisha mazrui

 

Mapema Waziri Mazrui alisema ili mtu aweze kuchangia damu ni lazima awe na  umri kati ya miaka 18 hadi 65,uzito usiopungua kilo 50,awe na asilimia 85 sawa na gramu 12.5 za wingi wa damu na asiwe ni mwenye maradhi endelevu.

 

Hata hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wafanyakazi wa kitengo cha damu salama pale wanapwafikia katika jamii ili kuhakikisha damu inapatikana wakati wowote.

 

Mpango wa damu salama ambao unazingatia uchangiaji damu kwa hiari umeanzishwa mwaka 2005 visiwani Zanzibar chini ya Wizara ya Afya kwa Ufadhili wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupunguza kasi za maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na kuziwezesha hospital kuwa na akiba za damu za kutosha kwa wakati wote,kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa 2024 ni "KUSHEREHEKEA MIAKA 20 YA UCHANGIAJI;AHSANTENI WACHANGIAJI DAMU"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.