Habari za Punde

Tanzania Mwenyekiti wa Mkataba wa Nairobi Kuhusu Utunzaji wa Mazingira

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto) akishiriki Mkutano wa 11 wa Nchi za Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Antananarivo, Madagascar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania ulioambatana naye katika Mkutano wa 11 wa Mawaziri wa Mkataba wa Nairobi Convention mara baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi Convention. Mhe. Dkt. Kijaji anashiriki Mkutano huo wa nchi za Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi ambao umeanza tarehe 21 hadi 22 Agosti, 2024 jijini Antananarivo, Madagascar.

Tanzania yachaguliwa Mwenyekiti wa Mkataba wa Nairobi kuhusu utunzaji wa mazingira

Tanzania imechaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi kuhusu utunzaji wa mazingira wakati wa Mkutano wa 11 wa Nchi za Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Antananarivo, Madagascar.

Hatua hiyo itaifanya Tanzania kuwa nchi mwenyeji wa Mkutano wa 12 (COP 12) wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi.

Akihutubia mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji Agosti 22, 2024 ameahidi kuendeleza ushirikiano na nchi zingine wanachama katika kuendeleza, kusimamia na kutunza mazingira ya bahari kwa ukanda huo.

Amewashukuru Wanachama wanaoingia Mkataba wa Nairobi kwa kuichagua Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Ofisi ya Mkataba wa Nairobi na kusema kuwa hiyo ni heshima kubwa ambayo itaenziwa.

Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji ametoa shukurani kwa kufanyika kwa Mkutano wa Nairobi na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa Mkutano wa COP 11 ulioandaliwa na kuratibiwa vyema.

“Hii ni COP yangu ya kwanza (tangu nilipoteuliwa) lakini ninahisi kama nimekuwepo kwa muda mrefu kwasababu ya kukaribishwa na ninyi nyote na namna mada ngumu zimefanywa rahisi na kueleweka kwa wasio wataalam,” amesema.

Halikadhalika, ameahidi kuwa Tanzania itafanya chochote kilicho ndani ya uwezo ili kuhakikisha uamuzi uliopitishwa katika COP 11 unatekelezwa kwa mafanikio na Sekretarieti inafanya kazi kwa ufanisi.

Waziri Dkt. Kijaji ambaye aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, amesema kupitia uzoefu wa mkutano huo, Tanzania itahakikisha inakuwa na mkutano wa COP12 bora zaidi.                                

Mkutano wa Mkataba wa Nairobi ulifunguliwa Agosti 20 hadi 22, 2024 ambapo Mhe. Dkt. Kijaji alifanya mikutano ya pembezoni na viongozi mbalimbali kujadili mikakati ya mazingira. 

Miongoni mwa washiriki aliofanya nao mazungumzo kwa nyakati tofauti ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi. Elizabeth Mrema, Mshauri wa Kiuchumi wa Mradi wa Western India Ocean Initiative Bi. Brenda Kibiki na Msimamizi wa Programu ya Lead Blue Economy – Western India Ocean (WIO) kupitia Mradi wa The Nature Conservancy (TNC) Dkt. Tuqa Jirmo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.