RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewapongeza na
kuwashukuru madaktari kutoka hospitali ya MIOT ya India kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kuwahudumia Wazanzibari hasa wagonjwa wa moyo, saratani na
kiharusi.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar
alipozungumza na uongozi wa hospitali hiyo ya MIOT ya Chinnai, India
wakiongozwa na mwenyeji wao Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui na watendaji
wakuu wa Wizara ya Afya, Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi amepongeza pia uhusiano mzuri uliopo
baina ya hospitali hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya
Afya na kueleza kuwa kuwepo kwao kumeongeza tija kubwa kwa jamii ya Wazanzibar
wenye mahitaji ya huduma zao.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameleeza kuwa Serikali imekua
ikitumia gharama kubwa kufuata baadhi ya matibabu nje ya nchi hasa kwa wagonjwa
wa moyo jambo alilolieleza haliathiri tuu wagonjwa bali na jamaa wa wagonjwa
hao wanaoambatana nao wakati wa matibabu.
Ameeleza kuwepo kwa madaktari hao nchini, ni fursa
nzuri kwa wataalamu wa ndani kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo, utaalamu
pia kupunguza gharama kubwa kwa wagonjwa wanaopata matibabu kutoka taasisi
hiyo.
Naye, Mkurugenzi wa hospitali hiyo ya MIOT, Dk.
Prithvi Manawng Mohandas amemueleza Rais Dk. Mwinyi huduma wanazozitoa kwa
wagonjwa wa Zanzibar hasa kwa maradhi ya saratani ni tiba za mionzi (Redio
therapy), matibabu ya kikemia (Chemical Therapy) na tiba ya kulenga eneo maalum (targeted therapy) pamoja na matibu ya moyo.
Akizungumzia ugonjwa wa kiharusi Dk. Prithvi
amemueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba wanawatibu wagonjwa wa maradhi hayo hasa kwa
kuwasaidia kuimarisha na kurejesha uwezo wa viungo vyao kwa kutembea na kufanya
shughuli zao za kawaida kwa maisha yao ya kila siku.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment