RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema suala la
kuimarisha utawala bora ni jambo la msingi kuleta maendeleo ya nchi, hivyo
amewasihi watumishi wa umma na binafsi kuongeza juhudi, uzalendo na uadilifu
katika kulitumikia Taifa.
Dk. Mwinyi
amesema, wajibu wa kuimarisha Utawala Bora hasa kwa matumizi
ya rasilimali za umma si wa Serikali na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
hesabu za Serikali pekee bali ni kwa kila mtumishi.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo, ukumbi
wa Ziwani Polisi Zanzibar kwenye maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Ukaguzi ya
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Zanzibar.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza
juhudi za kuijengea mazingira mazuri Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali ili itekeleze vizuri kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni,
na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa na kwenda sambamba na mabadiliko ya
mara kwa mara ya ukaguzi duniani.
Dk.
Mwinyi amebainisha kuwa, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali, imefanikiwa kuisaidia Serikali kutekeleza kwa ufanisi malengo na
mipango yake, na kuongeza kuwa Maendeleo makubwa yaliyofikiwa Serikalini
yanatokana na mchango wa udhibiti na ukaguzi bora wenye kuzingatia uwajibikaji,
nidhamu na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma nchini.
Aidha,
Rais Dk. Mwinyi amesema, miongoni mwa faida zinazopatikana kwenye Ofisi ya CAG
ni pamoja na kusaidia kuongeza Pato la Serikali ambapo, Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali kupitia ripoti yake ya kila mwaka, huishauri
Serikali juu ya mbinu bora za kuziba mianya ya upotevu wa makusanyo ya mapato
ya Serikali, kuibua vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuwepo kwa usimamizi bora
wa rasilimali za umma.
Ameeleza,
ufanisi unaotokana na utekelezaji wa kazi za ukaguzi una mchango mkubwa kwa
serikali hasa kuimarisha uchumi wa Zanzibar, ambapo hadi kufikia mwaka 2023 kasi ya ukuaji wa uchumi umefikia wastani wa
7.4% ikilinganishwa na 1.3% ya mwaka 2020.
Dk.
Mwinyi ameongeza kuwa, mafanikio ya kazi za ukaguzi wa rasilimali za umma,
yameimarisha utoaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji safi na
salama, nishati ya umeme na huduma nyengine.
Pia
Rais Dk. Mwinyi ameongeza kuwa, kazi za ukaguzi wa rasilimali fedha na
rasilimali nyegine zimeimarisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu
ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, viwanja
vya Michezo na masoko.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa sana na udhibiti
na ukaguzi bora wa rasilimali za umma, ambapo Serikali hupokea na kuzifanyia
kazi hoja, ushauri na mapendekezo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kupitia ripoti zake za kila mwaka.
Pia Dk. Mwinyi ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kuendelea
kufanikisha malengo na mipango ya sasa na baadae ya Ofisi hiyo kwa kadri hali
ya uchumi itakavyoruhusu.
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi
amepongeza ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar na Ofisi ya Taifa ya
Ukaguzi ya Tanzania kwa kufanikisha kazi za ukaguzi wa hesabu za Serikali
nchini.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi Ofisi ya Rais Sheria,
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amepongeza juhudi za rais Dk. Mwinyi za
kuimarisha Umoja, amani na maendeleo na mshikamao kumeifanya Zanzibar kuwa nchi
ya mfano kwa kasi ya Maendeleo yanayowashangaza wageni kutoka mataifa
mbalimbali.
Amekiri kuwepo kwa mabadiliko makubwa kwenye Ofisi ya CAG kwa kipindi
hiki cha Serikali ya awamu ya nane ambayo yamekuwa kielelezo cha mafanikio ya
miradi mbalimbali katika sekta tofauti.
Naye, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG), Dk.
Othman Abbas Ali amebainisha kuwa maadhimisho hay oni fursa adhimu kwa taasisi
za Umma kuwatumia wataalamu wao kuongeza uwajibikaji kubadilishana uzoefu na
kujifunza mbinu bora za kukabiliana na uhujumu wa Uchumi, kuongeza uwazi na
uwajibikaji pamoja na kutoa nafasi kwa watendaji wa Ofisi ya CAG kuwafikia
walengwa na kuwafariji katika makundi mbalimbali wakiwemo wazee wasiojiweza,
yatima, na wenye watu wenye mahitaji maalumu.
Ameongoza kuwa kujadiliwa kwa tipoti za CAG kila mwaka katika Baraza la
Wawakilishi kumbeendelea kuleta tija ya usimamizi wa rasilimali na matuimizi ya
fedha za umma kwa taasisi mbalimbali na kujenga uelewa kwa wananchi juu ya
utendaji wa Ofisi hiyo.
Maadhimisho ya Wiki ya Ukaguzi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali, Zanzibar kwa mwaka 2024, yenye kauli mbiu isemayo, “Kuimarika kwa Ukaguzi wa Rasilimali za Umma
Kunaongeza Ufanisi na Kuleta Tija Nchini.” yalianza rasmi tangu Disemba, 12 kufikia kilele
chake Disemba 18 mwaka huu kwa kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo kutoa
elimu ya ukaguzi kwa jamii, kuwatembelea na kuwafariji watoto waliolazwa katika
hospitali ya Kitogani, Unguja na Vitongoji kwa Pemba, kuwatembelea na
kuwafariji wazee wetu waliopo Sebleni, Unguja na Limbani Wete Pemba,
Kuwatembelea na kuwafariji Wanafunzi wenye mahitaji Maalum katika Skuli ya
Pujini, Pemba na Jendele kwa Upande wa Unguja, kuwatembelea na kuwafariji
Watoto yatima waliopo katika Kituo cha Mazizini pamoja na Kuwatembelea na
kuwafariji watumishi na wastaafu wagonjwa wa Afisi hii ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment