Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mh.Daniel Chongolo leo Desemba 12, 2024 aliungana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Naibu Kamishna (DCP) Ramadhani Ng'azi katika Operesheni ya kuzuia na kupambana na ajali katika Mkoa wa Songwe ili kupunguza ajali Mkoani humo.
Akizungumza na madereva wa malori katika eneo la kichangani Kata ya Chapwa Wilaya ya Momba Mh.Chongolo amesema kuwa hapendi kuona ajali zinatokea ndani ya Mkoa wa Songwe kwani zinapelekea madhara makubwa kama vifo na ulemavu na kupunguza nguvu kazi ya Taifa hivyo aliwataka watumiaji wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali hizo.
Katika hatua nyingine, Mh.Chongolo alisema Serikali inafanya jitihada za kujenga miundombinu bora ya barabara ili kuendelea kufanikisha shughuli za usafirishaji kuendelea Mkoani humo, Pia alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camillius Wambura kwa usimamizi mzuri wa kazi na shughuli za Serikali hasa katika kulinda raia na mali zao.
"Nilipongeze Jeshi la Polisi nchini chini ya Mkuu wa Jeshi hilo IGP Camillus Mongoso Wambura pamoja na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini DCP Ramadhan Ng'azi kwa kutoka ofisini kwake na kuja kuongea na madereva wa vyombo vya moto na kujua changamoto zao kisha kuzitatua na kuwapatia majibu hilo ni jambo zuri na linafanya Jeshi la Polisi kuwa karibu na jamii" alisema Mh.Chongolo.
Aidha, Mh.Chongolo alitoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kujiepusha na starehe ambazo zinaweza kuleta madhara kwao na kwa jamii kwani madereva ndio wana jukumu la kuepusha ajali kwa kufuata sheria za usalama barabarani na kutokutumia kilevi wakiwa wanaendesha vyombo vya moto hivyo kila mmoja anatakiwa kujilinda yeye na mwingine ili kuondoa changamoto za ajali ndani ya mkoa wa Songwe ikiwa ni pamoja na kutii sheria za usalama barabarani bila shuruti.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ramadhani Ng'azi aliwataka madereva hao kuwa na leseni zenye sifa zinazoendana na vyombo wanavyoviendesha ikiwa ni pamoja na kufuata sheria za usalama barabarani na kuepuka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kuyapita sehemu zisizo ruhusiwa.
Pia amewataka madereva kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi wapatapo changamoto wakiwa barabarani bali wanatakiwa watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi kwa haraka.
Naye, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Bukombe aliwataka madereva hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili waendelee kuwa salama wanapoendesha na wanapoegesha magari yao ndani ya Mkoa wa Songwe.
John Mwashiuya kwa niaba ya madereva hao alilishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu waliyopata na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuweza kuzuia na kutokomeza ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Katika Operesheni hiyo ya kuzuia na kupambana na ajali Mkoani Songwe, Wadau mbalimbali wa usalama barabarani walishiriki ambao ni Seleman Bishanga Meneja TANROAD Mkoa wa Songwe, Joseph Bulongo Meneja LATRA Mkoa wa Songwe na Ayoub Mimba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduma na waliweza kutoa mada mbalimbali na kujibu maswali na changamoto zilizoibuliwa na madereva hao.
No comments:
Post a Comment