Bismillahi Rahmani Rahim!
Mheshimiwa Othman Masoud Othman; Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar,
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla; Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar,
Mheshimiwa Sheikh Saleh Omar Kaabi; Mufti Mkuu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume; Rais Mstaafu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein; Rais Mstaafu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid; Spika wa Baraza la
Wawakilishi,
Mheshimiwa Khamis Ramadhan Abdalla; Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Sheikh Hassan Othman Ngwali; Kadhi Mkuu wa
Zanzibar,
Mheshimiwa Mwalimu Dkt. Haroun Ali Suleiman; Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora,
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri,
Mhandisi Zena Ahmed Said; Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,
Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya siasa,
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,
Ndugu Wanahabari,
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu Aleikum Warahamtullahi Wabarakatuh
Iddi Mubarak!
Ndugu Wananchi,
Shukurani zote za waja anastahiki Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataala, Mola na Viumbe vyote kwa kutujaalia neema ya uhai na kutuwezesha kuifikia siku hii ambapo Waislamu na Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla tunaungana na Waislamu na Mataifa mbali mbali duniani katika kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitri. Sikukuu hii ni neema kutoka kwa Mola wetu Mtukufu baada ya kukamilisha kwa salama mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na ibada nyengine tulizozifanya katika mwezi tulioukamilisha jana.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu azikubali ibada zetu zote tulizoifanya na atulipe malipo mema ya kutuingiza katika Pepo yake ya Fildaus Yarabil alaminah.
Ndugu Wananchi,
Kwa hakika leo ni siku ya furaha ya
kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kutakiana kheri ya sikukuu,
kula pamoja, kupeana zawadi, kutembeleana na kwenda kuwakagua wagonjwa, kuiombea
dua nchi yetu na kujiombea wenyewe na kupeana nasaha zenye lengo la kuongeza
ustawi wa jamii yetu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunaishukuru neema hii
aliyoturuzuku Mwenyezi Mungu na tunaendeleza mila na desturi walizotuachia
wazee wetu.
Sambamba na hayo, tuna utamaduni wa kuwa na Baraza la Iddi ambayo ni fursa nyengine ya kuungana pamoja katika kusherehekea Sikukuu ya Iddi kupeana nasaha na kuiombea dua nchi yetu tuzidi kupata mafanikio.
Napenda kutumia fursa kutoa salamu zangu za Iddi kwenu mliohudhuria Baraza hili la Iddi, kwa waislamu na wananchi wote wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakutakieni nyote na familia zenu sikukuu njema yenye kheri na baraka nyingi kwa utukufu wa siku ya leo.
Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
tulioukamilisha jana, tuliweza kujifunza mambo mbali mbali ya kheri ambayo kwa
kiasi kikubwa yaliweza kuhuisha imani zetu na ucha Mungu. Hivyo basi ni wajibu
wetu kuendeleza mwendo huo mwema katika miezi iliyobakia ikiwa ni namna bora ya
kunufaika na mafunzo yanayotokana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Bila ya shaka,
Mwenyezi Mungu ametuwekea Mwezi wa Ramadhani kuwa ni kipindi maalum cha
kujifunza kuwa wacha Mungu kwa kufanya mambo mema anayoyaridhia na kujiepusha
na makatazo yake, ili tuweze kupata mafanikio hapa duniani na kesho mbele ya
haki. Tumuombe Mwenyezi Mungu atuwezeshe kudumu katika mwendo huo mwema. Amiin.
Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa mambo ya msingi ambayo
tuliyapa kipaumbele ni kuoneshana moyo wa mapenzi, huruma na hisani kwa kutoa
sadaka ili kuwasaidia watu mbali mbali wenye uwezo mdogo wa kukidhi mahitaji
yao wakiwemo wazee, wajane, watu wenye ulemavu na Watoto yatima. Ni
dhahiri kuwa sadaka walizopata wenzetu hawa ziliwasaidia sana
kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa futari na daku,na kuwawezesha kutekeleza
ibada ya funga bila ya kuwa na wasiwasi wa kupata mahitaji yao muhimu.
Nasaha zangu ni kwamba tuendelee na mwendo huu mwema wa kusaidia watu wenye mahitaji mbali mbali katika maisha yetu ya kila siku. Hakika utoaji wa zaka na sadaka ni mambo yanayohimizwa katika Uislamu kutokana na faida zake katika jamii. Tunafundishwa kuwa miongoni mwao ni kuitakasa nafsi ya mtoaji na kuleta upole na huruma. Aidha, husaidia kuondoa chuki na husda na kujenga jamii yenye umoja, mapenzi na mshikamano na kuimarisha ustawi na uchumi. Hakika haya ni mambo ya msingi ambayo jamii yetu inayahitaji ili tuzidi kupiga hatua za mafanikio.
Napenda kutumia fursa hii kwa mara nyengine kutoa shukurani kwa watu wote waliotoa sadaka zao kwa madhumuni ya kuwasaidia wenzetu wenye mahitaji mbali mbali katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awalipe kila la kheri, awaongezee baraka katika shughuli zao na wapate mafanikio zaidi.
Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutudumisha katika hali ya amani na tukaweza kuitekeleza ibada ya
saumu na ibada nyengine tulizozitekeleza katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa
utulivu. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru ndugu zetu wasiokuwa waislamu kwa
ushirikiano mkubwa waliouonesha kwa ndugu zao waislamu wakati wakitekeleza
ibada ya saumu. Hakika ushirikiano wao ni muhimu na kigezo cha kustahamiliana
kwa wananchi wanaoamini madhehebu tafauti ya Dini kama ilivyo katika nchi yetu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atudumishe katika umoja na ushirikiano kwa manufaa na ustawi wa Taifa letu. Kwa baraka ya siku ya leo, tunamuomba Mola wetu Mlezi atujaalie kuweza kuilinda na kuidumisha neema hii ya amani tuliyonayo, hususan katika mwaka huu ambapo nchi yetu inakabiliana na Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba. Atuepushe kupita mtihani huo kwa salama na kubaki tukiwa tukiwa wamoja kwa faida ya vizazi vya sasa na wale watakaokuja baada ya sisi. Kila mmoja wetu kwa imani yake tuendelee kuiombea dua nchi yetu ili Mwenyezi Mungu atuvushe salama
Kwa lengo la kuhakikisha
tunasherehekea sikukuu hii kwa amani na furaha, napenda kuzihimiza mamlaka
zinazohusika kusimamia usalama katika viwanja vya sikukuu na katika barabara
zetu. Kwa kawaida katika kipindi cha sikukuu kunakuwa na harakati nyingi za
matumizi ya barabara. Lazima tuhakikishe sheria za usalama barabarani zinazingatiwa ili kuepusha ajali
zinazoweza kuepukika. Aidha, tuna wajibu wa kuhakikisha watoto wetu na wananchi
kwa jumla katika viwanja vyote vya sikukukuu wanakuwa salama dhidi ya vitendo vinavyoweza
kuharibu amani na furaha yao.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuwatakia kheri
na maandalizi mema ya Waislamu wenzetu wanaojiandaa kwenda kutekeleza Ibada ya
Hijja mwaka huu huko nchini Saudi Arabia. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie
wenzetu hao matayarisho mmema na wape afya njema ili wafanikiwe kwenda
kuitekeleza Ibada hiyo.
Tunawaombea safari njema na Mwenyezi Mungu azikubali ibada zao zote na kisha awarudishe nyumbani kwa salama.
Ndugu Wananchi,
Nahitimisha hotuba yangu kwa
kukutakieni nyote sikukuu njema ya Idd el-Fitri yenye furaha na amani. Napenda
kutoa shukurani kwa Kamati ya Kitaifa ya Sherehe na Mabaraza ya Iddi kwa
maandalizi mazuri ya shughuli hii. Shukurani maalum nazitoa kwa vijana wetu wa
Qasida kwa kusherehesha na kutupa ujumbe wenye mnasaba na shughuli hii. Aidha,
nalishukuru Jeshi la Polisi kwa kufanikisha sherehe hizi kwa paredi maalum.
Nakushukuruni tena nyote mliohudhuria katika Baraza hili la Idd el Fitri na
wale wanaofuatilia kupitia vyombo mbali mbali vya habari.
Kwa baraka ya siku ya leo, tunamuomba Mwenyezi Mungu awape shifaa wagonjwa wetu walioko hospitali na majumbani. Mwenyezi Mungu awarehemu wazee, masheikh na walimu wetu, ndugu, jamaa, marafiki na waislamu wote waliotangulia mbele ya haki. Awape malazi mema Peponi na sisi tulio hai atupe khatma njema. Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu neema na baraka ili tuzidi kupiga hatua za maendeleo.
IDDI MUBARAK
WAKULUU AAM
WAANTUM BIKHEIR
Ahsanteni kwa
kunisikiliza
No comments:
Post a Comment