Habari za Punde

Kukamilika kwa Ujenzi wa Bandari ya Abiria Maruhubi na Bandari Kavu ya Mpigaduri Kutaifungua Zaidi Nchi Kiuchumi

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kukamilika kwa ujenzi wa bandari ya abiria Maruhubi na bandari kavu ya Mpigaduri, kutaifungua zaidi nchi kiuchumi, sambamba na kuondoa changamoto kwenye sekta ya usafiri hapa nchini.

Mhe. Hemed ameyaeleza hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo inayoendela na ujenzi katika Mkoa wa Mjini Magharib.

Amesema bandari ndio lango la kiuchumi kwa nchi za visiwa kama Zanzibar, hivyo kukamilika kwa miradi hiyo, kunakwenda kuifungua nchi kiuchumi na kuimarika kwa sekta ya biashara na usafirishaji wa biadhaa.

Sambamba na hayo, Mhe. Hemed amesema changamoto iliyopo hivi sasa ya msongamano wa makontena pamoja na meli kukaa nangani kwa muda mrefu katika Bandari ya Malindi, nayo yanakwenda kufokia mwisho baada ya mradi huo kukamilika.

Amesisitiza kuwa serikali itahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, huku akiliagiza Shirika la Bandari Zanzibar kuharakisha ulipaji wa fidia kwa wananchi walioondoka katika eneo hilo kupisha ujenzi wa bandari hizo.

Makamu wa Pili wa Rais, amewahimiza wazanzibari wenye uwezo kutumia fursa ya kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayojengwa nchini, hasa ikizingatiwa kuwa kipaumbele cha serikali ni kuwapa fursa wazawa kwenye uwekezaji.

Amewataka wananchi wa Chumbuni na maeneo jirani kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wa ujenzi wa bandari hizo ili waweze kukamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Shirika la Bandari Zanzibar Akif Ali Khamis, amesema ujenzi wa bandari ya abiria ya Maruhubi hadi kukamilia kwake utagharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 400.

Amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa jengo la abiria, eneo la vyombo vya majini, sehemu ya kutulia ndege, kituo cha mabasi na kuruhusu meli nne kushusha na kupakia kwa wakati mmoja.

Akif amesema bandari hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa abiria zaidi ya milioni tano kwa mwaka na itakakuwa na uwezo wa kuzalisha nishati, jambo litakalosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Amesema bandari hiyo itakuwa miongoni mwa bandari kubwa Barani Afrika ambayo inajengwa kwa makubaliano kati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kampuni ya ZF Devco itakayojenga na kuiendesha bandari hiyo kwa muda wa miaka 33.

Ujenzi wa bandari ya abiria awamu ya kwanza Maruhubi,m na  ujenzi wa bandari kavu zinatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu na ujenzi wa bandari ya abiria awamu ya pili kwa ajili ya boti za mwendo kazi unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.

Wakati huo huo, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar alikagua ujenzi dakhalia inayojengwa katika skuli ya sekondari Lumumba na kuridhishwa na maendeleo ujenzi huo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Amesema wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inachukua juhudi mbali mbali katika kuhakikisha inatatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwa pamoja na kujenga skuli za kisasa, dakhalia na miradi mengineyo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Utawala Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khalid Massoud Waziri, alisema dakhalia hiyo itatumiwa na wanafunzi wanojianda na kufanya mitihani ya kidato cha nne na kidato cha sita.

Amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi kwa kuwekeza na kuipa kipaombele sekta ya elimu jambo linachangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua ujenzi mradi wa kituo cha Afya Mtoni, ujenzi wa skuli ya sekondari Mbuzini, ujenzi wa kituo cha afya Sebleni, ujenzi wa nyumba ya Sanaa Mwanakwerekwe na ukarabati wa hospitali ya wagonjwa wa Akili Kidongo Chekundu.

Miradi mingine aliyokagua ni ujenzi wa soko la Mboga Mombasa, ujenzi wa jengo la makaazi Kiembe Samaki, kukagua miradi inayojengwa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, ujenzi wa kiwanja cha michezo cha Kilimani Breeze na ukarabati wa Mahkama Kuu Vuga.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 22.07.2025
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.