Habari za Punde

KAMATI YA MAKATIBU WAKUU YARIDHISHWA NA UJENZI WA UWANJA MPYA WA MPIRA JIJINI ARUSHA

Kamati ya Makatibu Wakuu inayoongozwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, imekagua na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa mpira wa miguu katika eneo la Olmoti, jijini Arusha. Uwanja huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vitakavyotumika kwenye mashindano ya AFCON 2027.

Dkt. Yonazi amesema maendeleo ya mradi huo ni ya kuridhisha na uwanja huo utakuwa si tu kituo cha michezo, bali pia kivutio cha utalii na maendeleo ya uchumi kwa wakazi wa Arusha.

“Tunaamini uwanja huu utakuwa fursa kwa wananchi kuwekeza kibiashara. Ujenzi huu unapaswa kutazamwa kama chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya michezo.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema uwanja huo utaongeza idadi ya matukio ya kimataifa nchini, Kutakuza vipaji vya ndani, na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia michezo.

Ujenzi wa uwanja huo ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuandaa mashindano ya AFCON 2027, kwa ushirikiano na Kenya na Uganda








No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.