Habari za Punde

THBUB yawashauri wanasheria kubadili sheria za wavuvi wadogo ili kulinda haki zao

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Mohamed Khamis Hamad
 

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Mohamed Khamis Hamad, ameishauri kada  ya Sheria  kuimarisha mifumo ya sheria ikiwemo kubadilisha baadhi ya sheria zake ili kulinda haki za watu.

Mhe. Mohamed ameyasema hayo katika mkutanomaalum  uliowaweka pamoja Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na wadau wengine wa sekta ya uvuvi uliofanyika hoteli ya “Four point”, jijini Dar es Salaam Julai 16, 2025.

Aidha, ameeleza kufanyiwa marekebisho kwa sheria hizo hasa kwa sheria ya uvuvi kutasaidia kulinda haki za wavuvi wadogo wadogo katika kulinda na kutetea ustawi wao.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili wavuvi hao, Mhe. Mohamed alieleza kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutatuliwa kisheria hasa kuijenga uelewa jamii ya wavuvi wadogo pamoja na kuongeza uelewa wa haki za binadamu kwa jamii.

Mhe. Mohamed pia aliishauri Serikali kuwashirikisha wavuvi wadogo hasa wakati wa kupanga mikakati inayolenga kulinda rasilimali za bahari ili kutokiuka haki za binadamu.

Mapema akizungumza kwenye mkutano huo, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Uvuvi, Bi. Agness Meena, Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania, Prof. Mohamed Sheikh alibainisha kuwa haki za wavuvi wadogo ni msingi wa maendeleo endelevu kwenye sekta ya uvuvi nchini.

“Wavuvi wadogo ni muhimili mkubwa katika uchumi wa jamii za pwani na usalama wa chakula nchini. Ni wajibu wetu kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za bahari, wanalindwa dhidi ya unyanyasaji wa mifumo ya kisheria, na wanapewa elimu ya kutosha kuhusu matumizi endelevu ya bahari.” alieleza.

Prof. Mohamed alisisitiza kuwa haki huenda sambamba na wajibu, hivyo zinapoelezewa haki za wavuvi ni vyema pia kukaelezwa na wajibu wa wavuvi.

Mtano huo uliandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Denmark ya Haki za Binadamu kwa lengo la kukuza uelewa wa pamoja juu ya haki za binadamu zinavyohusiana na upatikanaji na usimamizi wa pamoja wa rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo wadogo, kuunda muhtasari wa pamoja wa mijadala ya kitaifa na kubaini mbinu bora na suluhisho za changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo wadogo.

Pia ulijadili haki za wavuvi wadogo katika upatikanaji na usimamizi wa pamoja wa rasilimali za bahari pamoja na kuwaweka pamoja wawakilishi kutoka Serikalini, asasi za kiraia, vyama vya wavuvi, wataalamu wa mazingira ya bahari, na mashirika ya kimataifa yanayoshughulika na maendeleo ya sekta ya uvuvi.






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.