Na Mwandish wetu, Dar es Salaam.
CHAMA cha Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) kimeshukuru uamuzi wa serikali ya kuwapatia mafunzo maalumu ya kunoa weledi na uzalendo wa wanachama wake kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Mabloga zaidi ya 200 wakiwemo wa diaspora walioanzisha Mtandao huo mwaka 2015 watapata mafunzo hayo.
“Tumekuwa na mazungumzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao kimsingi ndio wasimamizi wakuu wa maudhui na wametuthibitishia kwamba wapo hatua za mwisho za kutekeleza maagizo ya serikali ya kutoa mafunzo kwa mabloga wote nchini,” alisema Mwenyekiti wa TBN , Beda Msimbe.
Akifafanua kuhusu mafunzo hayo, Msimbe alisema kwamba lengo kuu la mafunzo ni kuwajengea mabloga weledi, uzalendo, na umakini katika kutambua na kupambana na habari feki, huku wakiwezesha usambazaji wa taarifa sahihi zitakazowawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu ujao.
“ Tunahitaji kukumbushana kuhusu nchi hii, katiba yetu, amani na umuhimu wa uchaguzi katika demokrasia ya aina yetu.Uamuzi huu wa serikali wa kutupiga msasa ni muhimu sana” alifafanua.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mwenyekiti huyo wa TBN, Beda Msimbe, alieleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na serikali kufanikisha mafunzo. Alisema wameomba mafunzo hayo kipindi cha sasa kwa kuwa wapo wanablogu ambao ni mara ya kwanza kuelekea katika uchaguzi mkuu, na kurejea ombi lao tena wakati wa mkutano wa wadau ulioandaliwa na Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo.
Alisema kwamba uongozi wa TBN kwa sasa unafanya kazi kwa karibu na serikali kuhakikisha kuwa zaidi ya wanachama 150 wa chama hicho waliotawanyika nchini kote wanafaidika kikamilifu na mafunzo haya muhimu.
Msimbe aliwataka mabloga wote nchini kuhakikisha wanawasiliana na Mratibu wa TBN, Bw. Gadiola Emanuel ili kuthibitisha anwani zao na kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi kwa ajili ya ushiriki. Pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wale wote ambao bado hawajajiunga na TBN kufanya hivyo sasa ili waweze kunufaika na fursa hii muhimu ya mafunzo.
Chama cha Mabloga Tanzania (TBN) kinajumuisha mabloga wanaotengeneza aina mbalimbali za maudhui, ikiwemo michezo, habari za siasa, afya, uchumi, na habari mchanganyiko. Mafunzo haya yanatarajiwa kuimarisha uwezo wao wa kutoa taarifa zenye ukweli na uhakika, hivyo kuchangia katika mazingira ya uchaguzi yenye uwazi na uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment