Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia
Wizara ya Maji, imekamilisha zoezi la ulipaji wa fidia yenye jumla ya Shilingi
Milioni 999 kwa wananchi 103 ambao ardhi yao ilitwaliwa katika maeneo ya
Nzuguni, Zuzu Nala, Nala Chihoni na Kibaigwa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi
wa miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Dodoma (DUWASA).
Ulipaji wa fidia hizo, umeongozwa na Wizara ya Maji kwa
kushirikiana na DUWASA, Wizara ya Ardhi na Viongozi wa Serikali za Mitaa wa
maeneo husika, ambapo kwa eneo la Nzuguni, Wananchi 24 wamelipwa fidia ya
Shilingi Milioni 148 tarehe 07 Agosti, 2025, Zuzu Nala Wananchi 51 ambao
wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 594
Agosti 11, 2025, Nala Chihoni Wananchi 7 ambao walilipwa fidia yao ya
Shilingi Milioni 58 tangu mwezi Aprili, 2025 na Kanda ya Kibaigwa Wananchi 23
wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 197 na kukamilisha zoezi hilo Agosti 12,
2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph
ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa
wananchi waliyotoa ardhi yao kupisha utekelezaji wa miradi ya maji.
"DUWASA, kwa niaba ya Wananchi wa maeneo ya Nzuguni,
Zuzu Nala, Nala Chihoni na Kibaigwa, inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na
Wizara ya Maji kwa juhudi zao kubwa na ufanisi katika kuhakikisha ulipaji wa
fidia kwa wakati kwa wananchi wetu," alisema Mhandisi Aron.
"Hatua hii ni muhimu sana kwa maeneo yaliyotekelezwa
na yanayoendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya kimkakati katika Jiji la
Dodoma na Kanda ya Kibaigwa, hii inaonesha dhamira ya Serikali katika kulinda
haki za wananchi wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo." Amesma
Mhandisi Aron.
Kwa upande wa wakazi wa Kibaigwa, Bi. Josephina Paulo
ameishukuru serikali kwa kuwasikiliza na kuwalipa fidia. Ameiomba serikali kwa
kuwaona wanyonge na kuwafikia wengine ambao bado hawajalipwa wanasubiri
kulipwa.
Naye Bwa. Yohana
Mwarabu ameshukuru serikali kwa kumjali na kumlipa kwani sasa ataenda kujenga
nyumba nyingine ili aweze kuishi na familia yake kwani awali hakuwa na
matumaini lakini kwa sasa anaamani.
Fidia hiyo ni sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa miradi
mbalimbali ya maji inayotekelezwa na Serikali kupitia DUWASA iliyokusudiwa
kuboresha upatikanaji wa majisafi na huduma za usafi wa mazingira ka wakazi wa
jiji la Dodoma na maeneo mengine yanayohudumiwa na DUWASA.
No comments:
Post a Comment