Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa AICC Bi. Christine G. Mwakatobe alipotembelea moja ya ukumbi wa mkutano ulifanyiwa maboresho.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi akiwa akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa AICC Bi. Christine G. Mwakatobe alipotembelea eneo la ujenzi wa mradi wa ukumbi mpya wa kisasa uliopo mbioni kuanza kutelezwa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, amepongeza jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu na uendeshaji zinazoendelea katika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Naibu Waziri Chumi amebainisha hayo wakati wa ziara yake ya kikazi aliyofanya katika kituo hicho cha mikutano tarehe 14 Agosti 2025 ambapo pia alipata fursa ya kutembelea eneo la ujenzi wa mradi wa ukumbi mpya wa kisasa uliopo mbioni kuanza kutelezwa.
Ziara hiyo iliyolenga kujionea hatua iliyofikiwa katika maboresho ya kituo hicho katika nyanja mbalimbali ikiwemo marekebisho ya miundombinu ya msingi ikiwemo kumbi za mikutano, maeneo ya mapokezi ya wageni, ujenzi wa lifti mpya za kisasa, pamoja na vifaa vya kisasa vinavyotumika katika mikutano ya kimataifa.
“Nimefurahishwa sana na hatua kubwa ambayo AICC
imefikia katika maboresho ya huduma na miundombinu
yake. Mageuzi haya yaliyofanyika katika kituo hiki muhimu
kwa Taifa na Afrika Mashariki yanaakisi maono na dhamira
ya dhati ya Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha
taasisi zake zinatoa huduma bora zinazokidhi viwango vya
kimataifa” alisema Mhe. Chumi.
Vilevile Mhe. Chumi alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya
utendaji na weledi wa Menejimenti ya kituo hicho ikiongozwa
Mkurugenzi Mtendaji Bi. Christine G. Mwakatobe, katika
utekelezaji wa maboresho hayo ambayo yana lengo la
kuimarisha uwezo wa AICC katika kuhudumia mikutano ya
kitaifa na kimataifa kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Aidha, Naibu Waziri alisisitiza kuhusu umuhimu wa AICC
kwenye utekelezaji wa dhana ya diplomasia ya uchumi na
nafasi yake kama lango la kukuza ushirikiano wa kikanda
kupitia mikutano ya kimataifa na shughuli za kidiplomasia.
Aliendelea kubainisha kuwa uboreshaji wa miundombinu hiyo
unakwenda sambamba na mkakati wa serikali wa kuvutia
wawekezaji na watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AICC
Bi. Christine G. Mwakatobe alieleza kuwa maboresho hayo
yanajumuisha ukarabati wa ukumbi wa Simba, matumizi ya
teknolojia ya kisasa katika mifumo ya mawasiliano na
uendeshaji wa mikutano, ulinzi na usalama, maboresho ya
huduma za afya katika hospitali ya AICC, pamoja
na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.
“Tumejipanga kuwa kituo kinachoongoza kwa ubora wa huduma Afrika Mashariki. Tunawashukuru viongozi wetu kwa kutupa msukumo wa maendeleo na kutufuatilia kwa karibu,” alisema Bi. Mwakatobe.
Ziara ya hiyo ya Mhe. Chumi imekuja wakati ambapo AICC imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maboresho, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindani wa kimataifa kama kituo bora cha mikutano barani Afrika.
Mbali na hayo, Mhe. Chumi akizungumza na menejimenti ya AICC, amewahimiza kuendelea kubuni mikakati ya kuvutia matukio makubwa ya kimataifa na kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kuongeza tija na mchango wa kituo hicho katika pato la taifa na maendeleo ya mkoa wa Arusha kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment