Abbas, Moroko kuifumua sehemu ya kiungo
Na Salum Vuai, Dar es Salaam
BAADA ya kuonja kipigo katika mchezo wa kwanza wa michuano ya Chalenji juzi, timu ya taifa ya Zanzibar ‘The Zanzibar Heroes’, leo inajaribu kufuta makosa yake itakapochuana na Burundi.
Mchezo kati ya timu hizo umepangwa kuanza wakati wa saa 8 :00 mchana katika uwanja wa Taifa jijini hapa.
Katika pambano lake dhidi ya Uganda Cranes siku ya kwanza ya mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia, Serengeti, Zanzibar Heroes ilichapwa mabao 2-1, huku Burundi ikiibomoa Somalia kwa magoli 4-1 ikiwa mechi za kundi ‘B’.
Kocha Abdelfatah Abbas, ameliambia gazeti hili jana kuwa, anakusudia kufanya mabadiliko katika sehemu ya kiungo, ambayo kwenye mechi ya juzi, ilionekana kupwaya na kukosa malengo.
Hata hivyo, hakueleza ni wachezaji gani atakaowapumzisha na ni akina nani watakaoanza leo, ingawa alionesha dhahiri kukosa raha kwa kutokuwepo Abdi Kassim ‘Babi’ kikosini ambaye amerudi Vietnam baada ya mechi za Taifa Stars na Chad kusaka tiketi ya Kombe la Dunia.
"Pamoja na kutokuwa na bahati tulipochyeza na Uganda, ninaamini kesho (leo) vijana hawatatuangusha na naiona wazi dalili ya ushindi", alisema.
Aidha alifahamisha kuwa ingawa mchezo wa mpira hautegemei ndoto, lakini anakiamini alichokiona usingizini usiku wa kuamkia jana, ambapo alisema alioneshwa magoli matatu yanatinga ndani ya nyavu za Warundi.
Bila shaka Zanzibar inahitaji kushinda leo, ili kufufua matumaini ya kusonga mbele, jambo ambalo linawezekana kwani Burundi iliyoishinda Somalia juzi, haikupata upinzani mkali kutokana na kiwango duni cha Somalia ambayo imezidiwa sana kisoka na Zanzibar.
Kocha Hemed Suleiman ‘Moroko’, hakuwa tayari kutaja wachezaji atakaowapanga leo, lakini alisema hatarajii kurejea makosa waliyofanya katika pambano la awali, na kuwahakikishia Wazanzibari kuwa bendera yao itapepea vyema leo.
Daktari wa timu hiyo Abdallah Said, amesema, Ali Badru ambaye aliumia kifundo baada ya kufunga goli nyavuni mwa Uganda, anaendelea vizuri na yapo matumaini makubwa atacheza leo.
0 Comments