6/recent/ticker-posts

MAALIM SEIF NA BALOZI SEIF WASHIRIKI UZINDUZI WA QUALITY CENTRE DAR

.Maalim Seif akiagana na waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga baada ya uzinduzi wa kituo cha Quality Center jijini Dar es salaam.(Picha; Salmin Said, OMKR)
Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga akikata utepe kuashiria kukizindua rasmi kituo cha Quality Center mjini Dar es Salaam
Maalim Seif na Balozi Seif Ali Iddi wakizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa kituo cha Quality Center jijini Dar es Salaam

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na makamu wa pili Balozi Seif Ali Iddi leo wameshiriki katika uzinduzi wa kituo cha biashara cha quality Center mjini Dar es Salaam linachomilikiwa na wafanyabishara wazalendo wa Tanzania.

Wakizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali mara baada ya uzinduzi rasmi uliofanywa na Waziri Mkuu wa Kenya Mhe. Raila Odinga, viongozi hao wamesema ni jambo la faraja kuona wafanyabishara wazalendo wanawekeza katika miradi mikubwa ya kichumi ambayo inasaidia mipango ya serikali ya kupunguza umaskini.


Wameitaka kampuni hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara mzalendo Bw. Yussuf Manji kuendelea na juhudi zake hizo ili iweze kuwekeza katika mikoa mengine ya Tanzania bara na visiwani kwa lengo la kurahisisha huduma za wananchi.

Akizindua kituo hicho cha biashara, Waziri Mkuu wa Kenya Mhe. Raila Odinga amezitaka nchi za Afrika Mashariki kuweka utaratibu mzuri katika maeneo ya mipaka ili kuruhusu wafanya biashara kutumia fursa za kibiashara zilizopo katika nchi hizo.

Amesema iwapo wafanyabiashara watapatiwa fursa hizo na kuondolewa vikwazo katika maeneo ya mipaka, wanaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kutimiza ndoto za EAC za kuwa na soko la pamoja.

Amefahamisha kuwa pamoja na mambo mengine nchi za Afrika Mashariki zinatakiwa kujipanga ili kukabiliana na maadui wa maendeleo wakiwemo ujinga, maradhi, njaa na uongozi mbaya kwa lengo la kufikia maendeleo ya kweli ya nchi za ukanda huu.

Ameelezea kufurahishwa na namna wafanyabiashara wa Tanzania walivyopata mwamko wa kuwekeza katika nchi yao jambo ambalo linaleta faraja kwa watanzania na nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla.

Amemkaribisha Bw. Manji kupekeleka miradi yake nchini Kenya na kumuahidi kumpatia eneo la kuwekeza iwapo ataamua kufanya hivyo.

“Tunataka kuwa ndugu wa kweli, sio wa kukutana kwenye vikao tu, tunakukaribisha sana Bw. Manji uje Kenya na nitakupatia eneo la kuweka mradi wao”, alisema Odinga.

Amesifu hatua hiyo ya kuanzishwa kwa kituo kikubwa cha biashara cha wazalendo na kwamba kimeonesha njia ya ushirikiano bora wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa vile kituo hicho kinaweza kutumiwa na wananchi mbali mbali wa nchi wananchama wa Jumuiya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo mwenyekiti wa kituo hicho Bw. Yussuf Manji amesema kituo kicho ambacho kitatoa huduma mbali mbali zikiwemo za kibenki na maduka ni cha aina yake na kwamba watajitahidi kutoa huduma zinazoendana na viwango vya kimataifa.

Hassan Hamad (OMKR).

Post a Comment

0 Comments