6/recent/ticker-posts

Buriani Ali Khatib

Shemsia Khamis na Haji Nassor, Pemba
 
ALIEKUWA mpiga picha wa kujitegema ‘the best photo studio’ ya mjini Chake Chake, Ali Khatib, amefariki dunia baada ya kuigonga gari eneo la benki ya watu wa Zanzibar mjini Chake Chake kisiwani Pemba, wakati akiendesha vespa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa kabla ya kifo cha marehemu huyo, aliwapita kilomita chache akiendesha chombo hicho kwa mwendo wa kasi.

Walisema marehemu huyo Ali Khatib Haji (28) aliivamia gari hiyo kwa pembeni ilipokuwa ikikatisha kuelekea eneo la Tibirinzi, ambapo baada ya muda mfupi mashuhuda hao, walisikia mshindo mkubwa na kukimbilia na baadae kumchukua hadi hospitali ya Chake Chake.

Mashuhuda wa ajali hiyo, walieleza kuwa ajali hiyo ambayo ilitokea majira ya saa 2:40 usiku wakati mpatwa na ajali hiyo, akitokea mjini Chake Chake na kuelekea Machomane, na alipofika eneo la benki ndipo alipokumbwa na ajali hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi daktari dhamana wa hospitali ya Chake Chake, Yussuf Hamad Iddi, alisema kuwa marehemu huyo alifikishwa hospitalini hapo majira ya saa 2:50 usiku huo, akiwa katika hali mbaya.

Alisema kuwa chanzo cha kifo chake ni kuumia kichwa na kuvuja damu sehemu zake za masikio na mdomoni, jambo ambalo lilisababisha kupoteza uhai wake muda mfupi tu baada ya kufikishwa hospitalini hapo.

Alisema kuwa pia marehemu huyo, alipata michubuko sehemu mbali mbali za mwilini mwake, ikiwa ni pamoja na mguu na mkono wa upande wake wa kulia na kusababisha kutokwa na damu na kisha kukumbwa na mauti hayo.

Alifahamisha kuwa marehemu huyo baada ya kufikishwa hospitalini hapo, hakuchukuwa muda mkubwa alifariki dunia kutokana na sababu hizo na alikabidhiwa kwa ndugu na jamaa zake kwa ajili ya shughuli za mazishi.

Mkuu wa upelelezi wa makosa jinai, Mkoa kusini Pemba Suleiman Hassan Suleiman, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja dereva aliekuwa akiendesha gari hiyo kuwa ni Said Saleh Ali, mkaazi wa Pondeani Chake chake, wakati akiwa na gari yenye namba za usajili Z 823 BQ.

Alieleza kuwa dereva wa gari hiyo yenye ‘route’ namba 136 Chake chake - Vitongoji, alikuwa akitokea upande wa Michakani na ndipo alipofika eneo la benki ya watu Zanzibar na kupinda kwenda eneo la Tibirinzi ndipo alipotoekezea muendesha vespa na kugonga gari hiyo.

Alisema marehemu huyo ambae alikuwa akiendesha vespa yenye namba za usahili Z 558 BH, chanzo za ajali hiyo ni kutokana mwendo wa kasi wa kijana, jambo ambalo lilisbabaisha mgongano huo kuwa mkubwa na kuvukwa na gozi la kichwa na kupoteza damu nyingi.

Hivyo Mkuu huyo wa upelelezi wa makosa ya jinai, aliwataka madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kuepukika.

Hata hivyo Mkuu huyo wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa wa Kusini Pemba, ameendelea kuwataka madereva wa gari na waendesha vyombo vya magurudumu mawili kuwa makini wanapokuwa barabarani.

Hii ni ajali ya 10 ya barabarani kutokezea kwa mwaka huu, kwa mkoa wa Kusini Pemba, kuanzia kipindi cha mwezi Januari hadi Septamba mwaka huu, kutokezea ambapo kati ya hizo saba zikihusisha vyombo vya maringi mawili.

Post a Comment

1 Comments

  1. Inna lillah wainna ilayhi rajioun. Allah amsamehe makosa yake

    ReplyDelete