Na Husna Mohammed, Beijing
IDHAA ya Kiswahili ya radio China kimataifa (CRI), ina mpango wa kuongeza watangazaji na waandishi wa habari kutoka Zanzibar ili kukuza mahusiano ya vyombo vya habari vya nchi mbili hizo.
Akizungumza na ujumbe wa wanahabari kutoka vyombo vya habari Zanzibar vilivyotembelea radio hiyo mjini Shijingshan jijini Beijing, Mkurugenzi wa CRI, Han Mei, alikiri kuweko kwa uchache wa wafanyakazi kutoka Zanzibar lakini akasema hilo linafanyiwa kazi.
“Ni kweli kabisa wafanyakazi wa Zanzibar ni wachache ukilinganisha na Tanzania Bara na Kenya hivyo tukifanya uajiri tutaipa kipaumbele Zanzibar ili kukipa hadhi kiswahili kimataifa,” alisema.
Sambamba na hilo lMkurugenzi huyo, alisema Zanzibar ni kiini cha lugha ya kiswahili fasaha hivyo kupata wafanyakazi kutoka Zanzibar kwa kiasi kikubwa kutaimarisha matangazo ya redio hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema ili kuhakikisha idhaa hiyo inasikika nchi mbalimbali wameanzisha madarasa ya lugha ya kichina sambamba na kufungua vituo vya FM katika nchi 63 duniani ikiwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki katika miji ya Nairobi na Mombasa nchini Kenya, Kampala na Jinja Uganda, Bujumbura nchini Burundi na Zanzibar.
Hata hivyo, alisema wana mpango wa kutoa mafunzo kwa watendaji wa vyombo vya habari vya Zanzibar kupitia madarasa ya kichina yanayofundishwa mjini Zanzibar.
Vilevile aliishukuru Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi mbili hizo.
Nae kiongozi wa msafara wa waandishi wa habari, Nasima Haji Chum, alisema ziara hiyo ni ya mafanikio makubwa kwa kuwa wamejifunza mambo mengi yanayohusu historia ya watu wa China na maendeleo yao.
“Tumejifunza mambo mengi ni wazi kuwa China imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo ingawa inasema haijafika wanakotaka,” alisema.
Idhaa ya radio ya taifa ya China imeanzishwa mwaka 1941, inatangaza lugha 63 duniani ambapo watu wapatao milioni 100 wanasikiliza matangazo ya redio hiyo.
0 Comments