Joseph Ngilisho,Arusha
KATIKA hali isiyo ya kawaida baadhi ya walinzi wa Shirika la Nyumba la Taifa jijini Arusha (NHC), kitalu namba 50
E mtaa wa Joel Maeda,wanadaiwa kuigeuza nyumba hiyo danguro na kujipatia fedha, kutokana na kuendesha biashara haramu ya ngono.
Hali hiyo inasababisha adha kwa wapangaji ndani ya nyumba hiyo.
Nyumba hiyo ipo mkabala na eneo la mzunguko wa mnara wa saa katikati ya jiji,ambapo hutumika kama jengo la ofisi mbalimbali za wapangaji huku eneo hilo likitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayosifika kwa biashara ya ngono.
Uchunguzi wa uhakika uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini baadhi ya walinzi katika jengo hilo wamekuwa wakipokea ujira wa shilingi 1,000 hadi 2,000 kwa watu wanaohitaji kufanya ngono.
Uchunguzi huo umebaini walinzi hao wamekuwa wakipokea fedha hizo kwa watu wanaohitaji kujisitiri ndani ya jengo hilo.
“Kila changudoa anayekuja na mteja wake hulazimika kumlipa mlinzi shilingi 1,000 hadi 2,000,” alisema mtoa habari.
Hali hiyo imesababisha wapangaji ndani ya jengo hilo kulalamikia tabia hiyo kuwa nyakati za asubuhi wanapokwenda kufungua ofisi hukutana na rundo la kondomu.
Mmoja wa wapangaji hao,Wilfred Mirambo ambaye anaendesha ofisi ya sheria ndani ya jengo hilo alithibitisha madai hayo na kusema kuna wakati aliwahi kuwafumania watu wakifanya ngono.
“Kuna siku nilikuwa nimesahau nyaraka muhimu ofisini ikanibidi nirejee usiku kuichukua ghafla nafungua mlango wa kupanda ngazi kuelekea ofisini nikawakuta watu wanafanya ngono waliponiona wakakimbia,”alisema.
Wapangaji wengine bila kutaja majina yao walisema walishawahi kufikisha taarifa zao polisi na shirika la nyumba la taifa mkoani Arusha lakini hakuna jitihada zilizochukuliwa.
Baadhi ya walinzi walipotafutwa ili kuzungumzia madai hayo walikataa lakini alipotafutwa Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoani Arusha,James Kisarika alioneshwa kushtushwa na taarifa hizo na kusema ofisi yake haijawahi kupokea malalamiko.
Alisema wanaopaswa kuchukua hatua ni wapangaji sio wao kwa kuwa wao ndio waliowaajiri walinzi hao huku akisisitiza jukumu lao ni kuhakikisha wanasimamia sheria za mikataba ya upangaji.
0 Comments