Na Masanja Mabula, Pemba
MTU mmoja amefariki dunia papo hapo na wengine watatu kunusurika, baada ya kula samaki aina ya bunju anayedaiwa kuwa na sumu.Tukio hilo limetokea katika kijiji cha Ukunjwi wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba.
Kamanda wa Polisi mkoa huo, Shekhan Mohammed Shekhan alimtaja marehemu kuwa Juma Abdalla Mmanga (15) na walionusurika na kulazwa hospitali ya Wete ni Suleiman Ali (9) , Abubakar Ali Suleiman (7) na Suleiman Issa Suleiman (11).
Alisema samaki huyo alivuliwa na marehemu Juma Abdalla Mmanga na Suleiman Issa Suleiman ambaye bado amelazwa hospitali.
"Tumepokea taarifa za mtoto kufariki dunia na wengine watatu kulazwa hospitali ya Wete baada ya kula samaki aina ya bunju ambaye ana sumu kali na inasemekana watoto hao ndio walikwenda kuvua wenyewe katika bahari ya Ukunjwi,” alisema.
Mwandishi wa habari hizi alifika wodi ya watoto ya hospitali ya Wete na kumkuta mtoto Suleiman Issa Suleiman akiendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, baba mdogo wa mtoto huyo, alisema hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri tofauti na alipofikishwa hospitali.
"Kwa kweli tunashukuru madaktari wameweza kutusaidia na sasa hali ya kijana wangu inaendelea vyema, kwani ni tofauti na tulivyokuja nae,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba, Mhe.Dadi Faki Dadi aliwataka wananchi kuacha kuvua na kula samaki wanaoweza kuua ili kunusuru maisha na afya zao.
0 Comments