6/recent/ticker-posts

Mwanamke Mjamzito Auawa Kikatili

Mwanajuma Mmanga na Khamisuu Abdallah
MWANAMKE mmoja mjamzito wa miezi miwili ameuawa kikatili baada ya kushambuliwa kwa mapanga na mumewe wakati akiswali sala ya alfajiri.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea alfajiri ya jana katika kijiji cha Donge Mtambile, wilaya ya Kaskazini ‘B’mkoa wa Kaskazini Unguja.

Marehemu ametambuliwa kwa jina la Msikitu Juma Ali (30).
Waandishi wa habari hizi walishuhudia mwili wa mwanamke huyo ukiwa na majeraha ya mapanga sehemu mbali mbali za mwili, ikiwemo usoni, kichwani na tumboni ukiwa umehifadhiwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Akisimulia mkasa huo, kaka wa marehemu, Shaame Ali Machano, alisema mtuhumiwa alikuwa akimshutumu mkewe kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mtoto wa mpangaji wake, wakati marehemu na mumewe wakiishi Mkele wilaya mjini Unguja.

Alisema hali hiyo ilisababisha mzozo mkubwa, ndipo familia ya marehemu ilimtaka mtoto wao ahame kwenye nyumba ya kupanga na kurejea nyumbani Donge, ambako walipewa nyumba ya kuishi.

Alisema mauaji ya ndugu yake yametokea siku nne tu tokea ahamie kijijini huko.
Alisema alfajiri ya kuamkia leo (jana), mtuhumiwa alimuamsha mkewe afanye ibada (swala ya alfajir) na wakati akiwa kwenye kitako cha shahada (tahiyattu) mtuhumiwa alianza kumshambulia kwa mapanga.

Alisema marehemu alijitetea kwa kupiga kelele lakini alimdhibiti kwa kumtia nguo mdomoni.
“Baada ya kupata taarifa za kuwepo vurugu, tulikwenda nyumbani kwake na kumkuta marehemu akiwa kwenye msala huku akiwa amefunikiwa kanga na mtuhumiwa hatukumkuta,” alisema kwa huzuni.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Kheri Mussa Haji amethibitisha mauaji hayo.
Aidha alisema baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa aliemtaja kwa jina la Abdalla Mohammed Kagomba (38) alijisalimisha kituo cha polisi Mahonda.

Alisema polisi walifika katika eneo la tukio walimkuta marehemu akiwa ameshafariki huku akiwa na majeraha ya kukatwa kwa panga.

Alisema baada ya kumuhoji mtuhumiwa, polisi waligundua kwamba chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi.
Kamanda Haji alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi mwao.

Daktari Dhamana wa hospitali ya Mnazimmoja, Dk. Msafiri Marijani, alisema chanzo cha kifo chake ni kupoteza damu nyingi.

Aidha alisema baada ya kumchunguza marehemu aligundulika kuwa na ujauzito wa miezi miwili.

Post a Comment

0 Comments