6/recent/ticker-posts

Dk Shein: CCM hakijahodhi mchakato wa Katiba

Na Said Ameir, Dodoma
 
Chama cha Mapinduzi CCM kimesema hakijahodhi wala hakina nia ya kuhodhi Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea hivi sasa kama baadhi ya vikundi vya watu vinavyodai.
 
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ilichofanya CCM katika mchakato huo ni kutoa maoni kama ilivyoelekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wala si vinginevyo.
 
Amewafananisha wanaosambaza maneno hayo ya uzushi kwa madai kuwa CCM inafanya hivyo kutokana na hofu ya kushindwa kwenye uchaguzi kuwa ni sawa na mfa maji ambaye haachi kutapatapa.
 
“Hayo ni mawazo ya wafa maji, na mfa maji haachi kutatapa. CCM haina nia hiyo wala hatuna hofu” Dk. Shein alieleza na kusisitiza kuwa Chama hicho kilitoa maoni yake kama ilivyoelekeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba na ilitarajiwa kuwa vyama vingine vingefanya hivyo hivyo.
 
Alifafanua kuwa katika mapendekezo ya chama hicho kilichoyawasilisha mbele ya Tume yamo yaliyotofautiana na yale yaliyomo kwenye rasimu lakini CCM imefanya hivyo kutokana na dhamira yake ya kweli ya kuhakikisha nchi inapata Katiba mpya yenye kukidhi mahitaji ya watanzania wote.
 
Katika hotuba yake leo akifungua mafunzo ya siku nne ya Makatibu wa CCM ngazi ya Mikoa na Wilaya pamoja na watendaji kutoka Makao Makuu ya chama hicho na wale kutoka Ofisi Kuu za Zanzibar na Dar es Salaam yanayofanyika huko mjini Dodoma Dk. Shein amesema chama hicho kitaheshimu maoni ya watanzania kupitia Kura ya Maoni wakati utakapofika.
 
Hata hivyo alisisitiza kuwa wao bado wataendelea kutoa maoni yao na kwamba”hatujawahi (wanaCCM) kutamka kuwa maoni yetu ndio yachukuliwe na Tume ya Katiba na kuyafanyia kazi na mengine yote yatupiliwe mbali” alisema Dk. Shein na kusisitiza kuwa wana CCM wameonyesha umakini mkubwa katika suala ya Katiba.  
 
Katika hotuba yake hiyo Makamu Mwenyekiti aliwataka watendaji hao kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ambayo karibu mada 12 zitawasilishwa zikiwemo juu ya maandalizi ya uchaguzi ili kuwajengea uwezo wa kiuongozi na kiutendaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kwa uweledi zaidi.
 
“Nawasihi kuwa muwe makini katika mada hizo na nyingine ili kuhakikisha kuwa matatizo na khitilafu zilizokuwa zikijitokeza kila wakati basi ukifika wakati huo hajizirudii” Dk Shein aliwaambia.
 
Awaeleza washiriki hao kuwa kwa weledi walionao haistahiki hata kidogo kunyooshewa vidole kulaumiwa kila uchaguzi ukifika kuwa wameigilia mchakato wa uchaguzi katika maeneo yao.
 
“Taratibu za kiutawala ni kuwa Makatibu kazi yenu ni utendaji na kutoa ushauri wa kitaalamu kwenye vikao vyenu. Haipendezi na haileti sura nzuri kwamba kila wakati shutuma za kuvuruga mchakato wa uchaguzi katika mikoa na wilaya ziwe zinaelekezwa kwa Makatibu” Dk. Shein alisema.
 
Aliwasihi Makatibu kujiepusha na wanachama wa chama hicho wanaojipitishapitisha na kuonyesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.
 
“Muwe nao kwa kuwa ni wanachama wenzetu katika chama lakini sio kushirikiana nao katika nia zao za kugombea kwa kuwa wakati haujafika” alisema Dk. Shein na kutoa wito kwa wanachama wa aina hiyo wawape fursa wanaoshika nafasi hizo na kushirikiana nao katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi.
 
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kusisitiza suala la maadili katika uongozi na utumishi wa chama na kueleza kuwa kiongozi wa CCM ni lazima awe kioo cha uadilifu mbele ya umma.
 
“Kiongozi wa CCM popote alipo lazima awe mfano wa mtu mwema mwenye kufuata maadili na uadlifu kufuatana na maelekezo ya Sera za Chama chetu na kwa kuzingatia sheria za nchi, silka na utamaduni wa jamii kwa jumla” Dk. Shein alisisitiza.
 
Kwa hiyo alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa CCM ambao wamekuwa wakifanya vitendo kinyume na maadili na uadilifu kuwa wakati ndio huu wa kujirekebisha vinginevyo waachie ngazi.
 
Alisisitiza kuwa uadilifu, uaminifu na nidhamu ni mambo muhimu katika kufanikisha ushindi wa chama hivyo chama hakitawavumilia watu wanaoharibu taswira ya chama mbele ya jamii.
 
Awali akimkaribisha Makamu Mwenyekiti kuyafungua mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana alieleza  kuwa miongoni mwa malengo ya mafunzo hayo ni kuimarisha chama hasa ngazi ya wilaya, matawi na mashina.
 
Lengo jingine ni kuwajengea uwezo wa kiuongozi na kiutendaji watendaji hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi zaidi na kwamba mafunzo hayo yatawapa fursa watendaji hao kujadiliana na kushauriana namna uendeshaji wa shughuli za chama katika mazingira ya sasa.

Post a Comment

4 Comments

  1. kama mwadilifu ndugu sheni tunataka kura ya maoni hapa znz kujua wanaotaka muungano na wasiotaka , fanya hima kabla ya kukutana na mola wako ukashindwa cha kumjibu

    ReplyDelete
  2. mkisha pewa nchi yenu mtaanza kubaguana huyu mpemba huyu muunguja na hili lipo usikatae

    ReplyDelete
  3. Zanzibar kukabidhiwa kwa wazanzibar inahitaji miaka 100 na ushei sio saivi.

    ReplyDelete
  4. Hatuna historia ya kubaguana usituletee unyerere wako. Kwanini nyie hamubaguani mpaka mutuahutumu sisi kubaguana. Wenye kuhubiri siasa za kibaguzi ZANZIBAR ni watu wakuhesabika. Kama fitina munaileta nyie Zanzibar. Sisi ni ndugu wa damu sio wa kuungana kwa kuchanganya udongo kwenye vibuyu.

    ReplyDelete