TAARIFA YA
MWENYEKITI WA KAMATI YA KUCHUNGUZA NA KUDHIBITI HESABU ZA SERIKALI NA MASHIRIKA
(P.A.C) KUHUSU UTEKELEZAJI WA RIPOTI YA KAMATI JUU YA SHIRIKA LA UMEME LA
ZANZIBAR (ZECO).
Mhe. Spika:
Jambo lolote linalohitaji Baraka na
rehema za Mweyezi Mungu huanzwa kwa jina lake Tukufu. Namimi nianze kumtaja
Mwenyezi Mungu (Subhannahu Wataaala), anaetupa uzima na afya njema, tukaweza
kufika katika Baraza hili na kujadili mambo mbali mbali kama tunavyotakiwa kufanya
hivyo na Katiba ya Zanzibar na Sheria za nchi.
Nikiwa mbele yako Mhe. Spika na mbele
ya macho ya wananchi wa nchi hii na nikisikika na habari hii kufika kwa
wananchi wa Mataifa mengine duniani, sina budi kutoa shukurani zangu kwako na
Wajumbe wa Baraza hili kwa moyo mmoja kuikubali ripoti ya Kamati yetu ya P.A.C,
iliyopewa kazi ya kufanya uchunguzi maalum wa utendaji na mambo mbali mbali ya
Shirika la Umeme la Zanzibar, kazi ambayo tuliifanya kwa ueledi mkubwa na ugumu
na changamoto nyingi zilizotukabili.
Mhe. Spika:
Shukurani zangu za dhati ziwe kwa Baraza
hili kwa kuipokea ripoti yetu ya Kamati baada ya kuiwasilisha kutokana na
Wajumbe hawa kuifahamu vizuri na ndipo kwa kauli moja, Baraza liliikubali
ripoti hiyo na kuiagiza Serikali iyatekeleze Mapendekezo ya Ripoti hiyo bila ya kuipa
ruhusa ya kufanya mapitio (kuchakachua) yaliyoelezwa na Ripoti hiyo.
Mhe. Spika:
Nataka kulikumbusha Baraza lako
Tukufu kwamba, wajibu wetu kama Kamati kuhusiana na kazi tuliyopewa na Baraza
hili kufuatia Hoja Binafsi ya Mhe. Hija Hassan Hija, ya Kuunda Kamati Teule
kulichunguza Shirika hilo, na hatimae Baraza kuamua kazi hiyo ifanywe na Kamati
ya P.A.C, wajibu huo umemalizika mara tu Kamati yetu ilipowasilisha Ripoti yake
mbele ya Baraza hili, na baada ya hapo Ripoti hiyo na kila kilichomo
kilibadilika na kuwa ni Ripoti ya Baraza na Maagizo yaliyomo, ambapo kabla ya
kuwasilishwa yalikuwa ni mapendekezo ya Kamati, yamegeuka na kuwa ni maagizo ya
Baraza.
Mhe. Spika:
Kwa udhati huu, hata leo nikisimama
na kuitwa jina lile lile la Mhe. Omar Ali Shehe, Mwenyekiti wa Kamati ya P.A.C,
na nikapewa tena hadhi na heshima ile ile ya Mwenyekiti wa Kamati, sitakuwa na
uwezo wa kusema lolote juu ya Ripoti hiyo dhidi ya maamuzi ya Baraza lako
Tukufu, kwani ninajua fika kwamba, maamuzi ya chombo hiki yana heshima kubwa.
Mhe. Spika:
Wajibu wa Baraza lako, pamoja na
majukumu mengine, ni kuisimamia Serikali. Wajibu huu unaoelezwa na kifungu cha 43(5)
cha Katiba ya Zanzibar, pia umeelezwa na kifungu cha 5A(2) cha Katiba hiyo,
kinachohusiana na Mgawanyiko wa Madaraka, na madaraka ya Baraza la Wawakilishi
ni kutunga Sheria na kusimamia Utekelezaji wa Shughuli za Umma.
Mhe. Spika:
Baraza lako linapotunga Sheria,
Serikali hii ya Mapinduzi inalazimika itekeleze shughuli zake kwa mujibu wa
maelekezo ya Sheria husika, na ni sawa na kusema, tunapotunga Sheria, basi
jukumu la Serikali ni kuisimamia sheria hiyo kama ilivyotungwa na Baraza la
Wawakilishi.
Sambamba na hilo, Baraza lako
linapopitisha Bajeti ya Serikali, na kuruhusu kukusanywa kwa Mapato, kufanywa
Matumizi kwa kazi za Kawaida na Kazi za Maendeleo, Serikali hii hii inalazimika
kufanya makusanyo hayo na matumizi kama viile Baraza hili lilivyoamua.
Mhe. Spika:
Nataka nisisitize kwamba, Baraza lako
Tukufu linapoiridhia ripoti yoyote ya Kamati ya Baraza na likaagiza Mapendekezo
ya Kamati hiyo yatekelezwe kama ilivyopendekezwa na Kamati ama hata yakifanyiwa
marekebisho na kuamuliwa na Baraza, Serikali hii hii inalazimika kutekeleza
maamuzi na maagizo ya Baraza kama yalivyo, na sio kugeuka na Kuunda Tume ama
Kamati nyengine, ikapewa kazi ya kuichunguza ripoti ambayo tayari imeshaamuliwa
na Baraza.
Mhe. Spika:
Baraza kwa mantiki ninayoikusudia
hapa, linajumuisha Wajumbe wasiokuwa Mawaziri; Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mwanasheria Mkuu na hata wewe mwenyewe Mhe. Spika. Na kwa kufahamu haja ya
maagizo na maamuzi ya Baraza kutekelezwa ipasavyo, Wajumbe wote hao wa Baraza,
ikiwa ni pamoja na Serikali, wanapata
fursa na nafasi nzuri ya kutoa maoni yao na maelekezo, kabla ya maamuzi ya
Baraza kufikiwa wakati Ripoti za Kamati zetu zinapowasilishwa Barazani.
Mhe. Spika:
Kimsingi si sahihi utekelezaji wa
maamuzi ya Baraza kuundiwa Tume nyengine kwa ajili ya kuyachunguza maamuzi
hayo, na wajibu pekee unaobaki kwa Serikali ni KUYACHUKULIA HATUA maamuzi hayo
kwa kuzingatia Sheria, ikiwa ni pamoja na Hatua za Kinidhamu na Hatua za
Kijinai, na hatimae kutoa taarifa ya utekelezaji hapa Barazani, taarifa ambayo
itakuwa na vielelezo vya uthibitisho wa hatua walizozichukua, kama vile ambavyo
ripoti zetu zinavyofanya, na sio kuletewa (mere statements) zisizokuwa na
uthibitisho wowote.
Mhe. Spika:
Kamati yangu ilifanya kazi kwa
umakini mkubwa. Iliwahoji wahusika wote wa Shirika pamoja na Mashahidi ikiwa ni
pamoja na kukusanya vielelezo husika. Serikali katika kutekeleza Mapendekezo ya
Baraza haikufanya hivyo na badala yake ni sawa na iliyotoa Dudu Mchuzini.
Mhe. Spika:
Tokea kuanzishwa kwa Utaratibu wa
Kikanuni, wa kuitaka Serikali kuwasilisha utekelezaji wa Mapendekezo ya Kamati
mbali mbali za Kudumu za Baraza hili na kwa kuzingatia Mapendekezo ya Kamati
Teule na Maagizo ya Baraza ya kuitaka Serikali ilete tena Mrejesho wa
utekelezaji wa Maagizo hayo hapa Barazani, muda mwingi unatumika kutoa semina
kwa Serikali hii juu ya namna ya uwasilishaji huo unavyotakiwa.
Mhe. Spika:
Serikali hii iliyojaa Wasomi na
Viongozi wazoefu, wenye uzoefu wa kusafiri mara kwa mara nchi za Ng’ambo kwa
kutumia fedha za Wananchi wavuja jasho, haipaswi kuendelea kupewa semina ya
namna ya utekelezaji wa Maagizo ya Baraza na Uwasilishaji wa Taarifa hizo za
Utekelezaji. Kwani tunaamini uwezo upo, ila uthubutu na utayari ni mbambo
yaliyokosekana kwa Serikali yetu, kwa kipindi cha miaka mingi sasa.
Mhe. Spika:
Nilidhani Serikali ingelichukua hatua
muafaka za kinidhamu kwa uzito wa makosa yaliyotendwa na watendaji wa Shirika
dhidi ya makosa ya kuhujumu uchumi. Aidha, kwa vile Kamati ilifanya uchunguzi
wa kina na kukusanya vielelezo vinavyojitosheleza, kwa hatua hii, nilidhani
Serikali itachukua hatua ya kuwasilisha vielelezo hivyo kwa Afisi ya Mkurugenzi
wa Mashtaka, ili Mkurugenzi huyu afuatilie taratibu za kufikishwa Mahakamani
kwa wahusika badala ya kuliacha shauri hili Polisi kwa kufanya uchunguzi ambao
tayari umeshafanywa na Kamati yangu.
Mhe. Spika:
Wananchi wetu wa Zanzibar pamoja na
Wajumbe wako wa Baraza hili wa Beck Benchers, tunaamini kwamba, Serikali hii
bado haijawa tayari juu ya suala zima la KUWAJIBIKA NA KUWAWAJIBISHA WALE WOTE
WALIOHUSIKA na Ripoti mbali mbali za Baraza, na matokeo yake kutafutwa namna
yoyote ya kusema, ili ionekane bado wana hamu ya kutekeleza maagizo hayo, huku
muda ukipotea bila ya Utekelezaji wa Maagizo ya Baraza kama yanavyotakiwa.
Mhe. Spika:
Kwa mnasaba wa Shirika hili la Umeme
na kwa kuzingatia Maamuzi ya Baraza baada ya Ripoti ya Kamati yetu, na kwa
kuzingatia maelezo ya utekelezaji yasiyo na ushahidi wowote na yanayokengeuka
masharti ya utekelezaji wa Maagizo hayo kama yalivyoagizwa na Baraza hili
Tukufu, ni wazi kwamba Serikali imeridhika kwa yale mapungufu yote
yaliyobainika na Kamati na kukubaliwa na Baraza.
Sio vyema sana kwa hali hii
inavyoendelea kusema kwamba, Serikali hii ni stahamilivu sana kwa maovu
yanayotendeka katika Shirika la Umeme na mama mwema sio tu asieweza kukikata
kiganja cha mwanawe bali hukiosha japo hakiosheki, lakini pia amejizuia
kumadhibu, hata kama mtoto huyo amefurutu katika utovu wa adabu na heshima kwa
wazazi wake.
Mhe. Spika:
Naendelea kukushukuru wewe na
kuwashukuru Wajumbe wote wa Baraza lako hili kwa usikivu wenu. Na Naomba
kuwasilisha.
……………………………..
Mhe. Omar
Ali Shehe,
Mwenyekiti,
Kamati ya
P.A.C,
Baraza la
Wawakilishi,
Zanzibar.
1 Comments
Hapo ndipo ulipo uzaifu wa smz, kulindana hata kwenye jambo kubwa kama hili la ufujaji wamali za wana nchi vingozi wana lindana kwa kujua kua hatua zakisheria zita wagusa hata wao ndani ya suk hakuna msafi wote walaji, znz, hakuna mtetezi wa wanyonge na wanajua kuwa wanaongoza watu wa kusadikika, uwezo wao wakufikiri mdogo,zeco, kuna ujambazi, wakutisha na tume ya barazala wakilshi inapigwa danadana, nani mwengine ataye weza kuhoji wajue 2015 haipo mbali tutapambana aumtasema ukweli
ReplyDelete