6/recent/ticker-posts

Taarifa ya Mwenyekiti wa PAC kuhusu utekelezaji wa Ripoti ya kamati inayohusu ZECO


TAARIFA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA KUCHUNGUZA NA KUDHIBITI HESABU ZA SERIKALI NA MASHIRIKA (P.A.C) KUHUSU UTEKELEZAJI WA RIPOTI YA KAMATI JUU YA SHIRIKA LA UMEME LA ZANZIBAR (ZECO).

Mhe. Spika:

Jambo lolote linalohitaji Baraka na rehema za Mweyezi Mungu huanzwa kwa jina lake Tukufu. Namimi nianze kumtaja Mwenyezi Mungu (Subhannahu Wataaala), anaetupa uzima na afya njema, tukaweza kufika katika Baraza hili na kujadili mambo mbali mbali kama tunavyotakiwa kufanya hivyo na Katiba ya Zanzibar na Sheria za nchi.

Nikiwa mbele yako Mhe. Spika na mbele ya macho ya wananchi wa nchi hii na nikisikika na habari hii kufika kwa wananchi wa Mataifa mengine duniani, sina budi kutoa shukurani zangu kwako na Wajumbe wa Baraza hili kwa moyo mmoja kuikubali ripoti ya Kamati yetu ya P.A.C, iliyopewa kazi ya kufanya uchunguzi maalum wa utendaji na mambo mbali mbali ya Shirika la Umeme la Zanzibar, kazi ambayo tuliifanya kwa ueledi mkubwa na ugumu na changamoto nyingi zilizotukabili.

Mhe. Spika:

Shukurani zangu za dhati ziwe kwa Baraza hili kwa kuipokea ripoti yetu ya Kamati baada ya kuiwasilisha kutokana na Wajumbe hawa kuifahamu vizuri na ndipo kwa kauli moja, Baraza liliikubali ripoti hiyo na kuiagiza Serikali iyatekeleze  Mapendekezo ya Ripoti hiyo bila ya kuipa ruhusa ya kufanya mapitio (kuchakachua) yaliyoelezwa na Ripoti hiyo.

Mhe. Spika:

Nataka kulikumbusha Baraza lako Tukufu kwamba, wajibu wetu kama Kamati kuhusiana na kazi tuliyopewa na Baraza hili kufuatia Hoja Binafsi ya Mhe. Hija Hassan Hija, ya Kuunda Kamati Teule kulichunguza Shirika hilo, na hatimae Baraza kuamua kazi hiyo ifanywe na Kamati ya P.A.C, wajibu huo umemalizika mara tu Kamati yetu ilipowasilisha Ripoti yake mbele ya Baraza hili, na baada ya hapo Ripoti hiyo na kila kilichomo kilibadilika na kuwa ni Ripoti ya Baraza na Maagizo yaliyomo, ambapo kabla ya kuwasilishwa yalikuwa ni mapendekezo ya Kamati, yamegeuka na kuwa ni maagizo ya Baraza.


 

 

Mhe. Spika:

Kwa udhati huu, hata leo nikisimama na kuitwa jina lile lile la Mhe. Omar Ali Shehe, Mwenyekiti wa Kamati ya P.A.C, na nikapewa tena hadhi na heshima ile ile ya Mwenyekiti wa Kamati, sitakuwa na uwezo wa kusema lolote juu ya Ripoti hiyo dhidi ya maamuzi ya Baraza lako Tukufu, kwani ninajua fika kwamba, maamuzi ya chombo hiki yana heshima kubwa.

Mhe. Spika:

Wajibu wa Baraza lako, pamoja na majukumu mengine, ni kuisimamia Serikali. Wajibu huu unaoelezwa na kifungu cha 43(5) cha Katiba ya Zanzibar, pia umeelezwa na kifungu cha 5A(2) cha Katiba hiyo, kinachohusiana na Mgawanyiko wa Madaraka, na madaraka ya Baraza la Wawakilishi ni kutunga Sheria na kusimamia Utekelezaji wa Shughuli za Umma.

Mhe. Spika:

Baraza lako linapotunga Sheria, Serikali hii ya Mapinduzi inalazimika itekeleze shughuli zake kwa mujibu wa maelekezo ya Sheria husika, na ni sawa na kusema, tunapotunga Sheria, basi jukumu la Serikali ni kuisimamia sheria hiyo kama ilivyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Sambamba na hilo, Baraza lako linapopitisha Bajeti ya Serikali, na kuruhusu kukusanywa kwa Mapato, kufanywa Matumizi kwa kazi za Kawaida na Kazi za Maendeleo, Serikali hii hii inalazimika kufanya makusanyo hayo na matumizi kama viile Baraza hili lilivyoamua.

Mhe. Spika:

Nataka nisisitize kwamba, Baraza lako Tukufu linapoiridhia ripoti yoyote ya Kamati ya Baraza na likaagiza Mapendekezo ya Kamati hiyo yatekelezwe kama ilivyopendekezwa na Kamati ama hata yakifanyiwa marekebisho na kuamuliwa na Baraza, Serikali hii hii inalazimika kutekeleza maamuzi na maagizo ya Baraza kama yalivyo, na sio kugeuka na Kuunda Tume ama Kamati nyengine, ikapewa kazi ya kuichunguza ripoti ambayo tayari imeshaamuliwa na Baraza.

Mhe. Spika:

Baraza kwa mantiki ninayoikusudia hapa, linajumuisha Wajumbe wasiokuwa Mawaziri; Mawaziri na Naibu Mawaziri; Mwanasheria Mkuu na hata wewe mwenyewe Mhe. Spika. Na kwa kufahamu haja ya maagizo na maamuzi ya Baraza kutekelezwa ipasavyo, Wajumbe wote hao wa Baraza, ikiwa ni pamoja na Serikali,  wanapata fursa na nafasi nzuri ya kutoa maoni yao na maelekezo, kabla ya maamuzi ya Baraza kufikiwa wakati Ripoti za Kamati zetu zinapowasilishwa Barazani.

Mhe. Spika:

Kimsingi si sahihi utekelezaji wa maamuzi ya Baraza kuundiwa Tume nyengine kwa ajili ya kuyachunguza maamuzi hayo, na wajibu pekee unaobaki kwa Serikali ni KUYACHUKULIA HATUA maamuzi hayo kwa kuzingatia Sheria, ikiwa ni pamoja na Hatua za Kinidhamu na Hatua za Kijinai, na hatimae kutoa taarifa ya utekelezaji hapa Barazani, taarifa ambayo itakuwa na vielelezo vya uthibitisho wa hatua walizozichukua, kama vile ambavyo ripoti zetu zinavyofanya, na sio kuletewa (mere statements) zisizokuwa na uthibitisho wowote.

Mhe. Spika:

Kamati yangu ilifanya kazi kwa umakini mkubwa. Iliwahoji wahusika wote wa Shirika pamoja na Mashahidi ikiwa ni pamoja na kukusanya vielelezo husika. Serikali katika kutekeleza Mapendekezo ya Baraza haikufanya hivyo na badala yake ni sawa na iliyotoa Dudu Mchuzini.

Mhe. Spika:

Tokea kuanzishwa kwa Utaratibu wa Kikanuni, wa kuitaka Serikali kuwasilisha utekelezaji wa Mapendekezo ya Kamati mbali mbali za Kudumu za Baraza hili na kwa kuzingatia Mapendekezo ya Kamati Teule na Maagizo ya Baraza ya kuitaka Serikali ilete tena Mrejesho wa utekelezaji wa Maagizo hayo hapa Barazani, muda mwingi unatumika kutoa semina kwa Serikali hii juu ya namna ya uwasilishaji huo unavyotakiwa.

Mhe. Spika:

Serikali hii iliyojaa Wasomi na Viongozi wazoefu, wenye uzoefu wa kusafiri mara kwa mara nchi za Ng’ambo kwa kutumia fedha za Wananchi wavuja jasho, haipaswi kuendelea kupewa semina ya namna ya utekelezaji wa Maagizo ya Baraza na Uwasilishaji wa Taarifa hizo za Utekelezaji. Kwani tunaamini uwezo upo, ila uthubutu na utayari ni mbambo yaliyokosekana kwa Serikali yetu, kwa kipindi cha miaka mingi sasa.

 

Mhe. Spika:

Nilidhani Serikali ingelichukua hatua muafaka za kinidhamu kwa uzito wa makosa yaliyotendwa na watendaji wa Shirika dhidi ya makosa ya kuhujumu uchumi. Aidha, kwa vile Kamati ilifanya uchunguzi wa kina na kukusanya vielelezo vinavyojitosheleza, kwa hatua hii, nilidhani Serikali itachukua hatua ya kuwasilisha vielelezo hivyo kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, ili Mkurugenzi huyu afuatilie taratibu za kufikishwa Mahakamani kwa wahusika badala ya kuliacha shauri hili Polisi kwa kufanya uchunguzi ambao tayari umeshafanywa na Kamati yangu.

Mhe. Spika:

Wananchi wetu wa Zanzibar pamoja na Wajumbe wako wa Baraza hili wa Beck Benchers, tunaamini kwamba, Serikali hii bado haijawa tayari juu ya suala zima la KUWAJIBIKA NA KUWAWAJIBISHA WALE WOTE WALIOHUSIKA na Ripoti mbali mbali za Baraza, na matokeo yake kutafutwa namna yoyote ya kusema, ili ionekane bado wana hamu ya kutekeleza maagizo hayo, huku muda ukipotea bila ya Utekelezaji wa Maagizo ya Baraza kama yanavyotakiwa.

Mhe. Spika:

Kwa mnasaba wa Shirika hili la Umeme na kwa kuzingatia Maamuzi ya Baraza baada ya Ripoti ya Kamati yetu, na kwa kuzingatia maelezo ya utekelezaji yasiyo na ushahidi wowote na yanayokengeuka masharti ya utekelezaji wa Maagizo hayo kama yalivyoagizwa na Baraza hili Tukufu, ni wazi kwamba Serikali imeridhika kwa yale mapungufu yote yaliyobainika na Kamati na kukubaliwa na Baraza.

Sio vyema sana kwa hali hii inavyoendelea kusema kwamba, Serikali hii ni stahamilivu sana kwa maovu yanayotendeka katika Shirika la Umeme na mama mwema sio tu asieweza kukikata kiganja cha mwanawe bali hukiosha japo hakiosheki, lakini pia amejizuia kumadhibu, hata kama mtoto huyo amefurutu katika utovu wa adabu na heshima kwa wazazi wake.

Mhe. Spika:

Naendelea kukushukuru wewe na kuwashukuru Wajumbe wote wa Baraza lako hili kwa usikivu wenu. Na Naomba kuwasilisha.

 

 

 

……………………………..

Mhe. Omar Ali Shehe,

Mwenyekiti,

Kamati ya P.A.C,

Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.

 

 

Post a Comment

1 Comments

  1. Hapo ndipo ulipo uzaifu wa smz, kulindana hata kwenye jambo kubwa kama hili la ufujaji wamali za wana nchi vingozi wana lindana kwa kujua kua hatua zakisheria zita wagusa hata wao ndani ya suk hakuna msafi wote walaji, znz, hakuna mtetezi wa wanyonge na wanajua kuwa wanaongoza watu wa kusadikika, uwezo wao wakufikiri mdogo,zeco, kuna ujambazi, wakutisha na tume ya barazala wakilshi inapigwa danadana, nani mwengine ataye weza kuhoji wajue 2015 haipo mbali tutapambana aumtasema ukweli

    ReplyDelete