6/recent/ticker-posts

Taarifa ya Serikali kuhusu Baraza la Manispaa la Zanzibar

TAARIFA YA SERIKALI JUU YA HOJA ZILIZOTOLEWA KATIKA RIPOTI YA KAMATI TEULE YA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU BARAZA LA MANISPAA LA ZANZIBAR


1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa naomba kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Serikali kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi kwa jinsi unavyoliongoza Baraza letu hili kwa busara na hekima kubwa, jambo ambalo linaliwezesha Baraza kutekeleza Majukumu yake ya kikatiba kwa ufanisi mkubwa. Aidha, nalishukuru Baraza lako Tukufu kwa kuridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Kuchunguza Utendaji wa Baraza la Manispaa.


Mheshimiwa Spika, vile vile, nachukua fursa hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati Teule Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin Mwakilishi wa kuchaguliwa na Wananchi wa Jimbo la Magomeni pamoja na Wajumbe wake wote kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuibua hoja mbali mbali na kutoa mapendekezo yao juu ya hatua za kuchukuliwa ili kuimarisha utendaji wa Baraza la Manispaa. Kwa hakika hoja zilizoibuliwa ni muhimu na Serikali imepokea Ripoti ya Kamati Teule kwa moyo mkunjufu na kuzingatia kwa makini hoja na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati.


Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba, Serikali tayari imeanza kuchukua hatua katika kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yako Teule.


Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo, sasa naomba uniruhusu kutoa maelezo kuhusiana na hoja mbalimbali zilizotolewa na Kamati Teule ya Baraza kama ifuatavyo:


2.0 MAELEZO YA SERIKALI KUHUSU HOJA MBALIMBALI ZILIZOTOLEWA NA KAMATI TEULE YA BARAZA LA WAWAKILISHI


Hoja Nambari 1: Mheshimiwa Spika, hoja hii ina maeneo sita yanayohitaji kupatiwa maelezo kama ifuatavyo:


  1. Mikataba ya Baraza la Manispaa kusainiwa bila ya kufuatwa matakwa ya kifungu cha 20(2) cha Sheria Nam. 3 ya 1995.


  1. Watendaji wa Baraza la Manispaa wakiongozwa na Mkurugenzi hawafuati maadili ya kazi, Sheria na Kanuni za Baraza katika kuingia na kufunga mikataba.


  1. Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa amekuwa akitumia         madaraka yake vibaya kwa kuamua vile anavyoona inafaa.


  1. Mwanasheria wa Baraza hashirikishwi ipasavyo katika uandaaji wa mikataba mbali mbali.


  1.    Kifungu cha 20(2) cha Sheria Nambari 3 ya 1995 kinachoeleza kwamba mikataba yote itakayoingiwa na Baraza itatiwa muhuri wa Baraza mbele ya Meya au Naibu Meya na Mkurugenzi au Afisa mwengine wa Baraza atakaeidhinishwa kwa niaba ya Mkurugenzi kwa kibali au azimio la Baraza. Vile vile, Kanuni 55(b) ya Kanuni za Baraza la Manispaa inaeleza kwamba mikataba itakayofungwa na Baraza ambayo thamani yake itazidi shilingi 5,000,000 ni lazima ipate kibali cha Baraza zima.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hoja hizo Kamati yako Teule ilitoa mapendekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma na kulitaka Baraza la Manispaa kutekeleza majukumu yake kwa misingi ya Sheria na Kanuni za Nchi na mikataba yote ya Baraza inafungwa kwa kuzingatia Sheria. Aidha, Kamati Teule imeishauri Serikali kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa Madiwani na watendaji wa Baraza wanashirikiana ili kuleta tija inayokusudiwa.
   
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja ya kusaini mikataba bila kufuata matakwa ya kisheria, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kurekebisha hali hiyo na kuipeleka mikataba yote iliyofungwa na itakayofungwa kuanzia sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupata ushauri na maelekezo jambo ambalo tayari limeshatekelezwa. Aidha, hivi sasa kila mkataba unaofungwa na Baraza la Manispaa unashuhudiwa na Meya au Naibu Meya kwa kuweka saini yake katika mkataba huo.



Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja ya watendaji wa Baraza wakiongozwa na Mkurugenzi kutofuata Sheria na Kanuni za Baraza katika kuingia na kufunga mikataba, Serikali inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya kwamba ingawa Baraza la Manispaa ni taasisi inayojitegemea, bado taasisi hii inatakiwa kutekeleza majukumu waliyopewa kwa kufuata misingi ya Sheria na Kanuni za nchi. Tayari Serikali imeshaiagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa Baraza hilo ili litekeleze majukumu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo. Aidha, Serikali tayari imempa maelekezo Mkurugenzi mpya wa Manispaa kuhakikisha kuwepo kwa ushirikiano wa kutosha baina Madiwani na Watendaji wa Baraza la Manispaa kwa lengo la kuleta ufanisi.


Hoja Nambari 2: Baraza la Manispaa limefuta Mikataba ya walioshindwa kutekeleza masharti ya mikataba bila ya kuwapa nafasi ya kujitetea.


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule katika maelezo yake juu ya hoja hii ilianisha kuwa Masharti ya mikataba hayatekelezwi ipasavyo kwa mfano; kipengele cha 1.1 katika mikataba yote ya uwekaji mabango ambacho kinazungumzia kuhusu suala la muda kimekuwa kikitumika vibaya kwa upande mmoja kutoa maamuzi bila ya kuuhusisha upande wa pili. Hali ambayo imepelekea kutokezea kwa maingiliano ya mikataba na kupelekea migogoro baina ya Kampuni za matangazo na Baraza la Manispaa.


Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Kamati kuhusu hoja hii ni kwamba hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, Ndugu Rashid Ali Juma na kulitaka Baraza la Manispaa kuzingatia Sheria zinazoongoza mikataba.


Mheshimiwa Spika, Sheria za Mikataba zinataka kila upande ulioingia mikataba utekeleze majukumu yake, endapo upande mmoja wa mkataba utashindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya mkataba ni wajibu wa upande huo ulioshindwa kuupa taarifa ya kushindwa kutekeleza majukumu upande mwengine.  Kwa kuwa Kampuni zilizoingia mikataba ya kuweka mabango ya matangazo barabarani zilipewa muda maalumu wa utekelezaji, zilipaswa kufuata muda huo na endapo Kampuni yoyote ilishindwa kutekeleza masharti ya mkataba ndani ya muda waliokubaliana ilipaswa Kampuni hiyo kutoa taarifa kwa Baraza la Manispaa na kueleza sababu za kushindwa kutekeleza makubaliano hayo.  Hata hivyo, Serikali inakubaliana na mapendekezo ya Kamati kwamba Baraza la Manispaa lilipaswa kutoa notisi kwa Kampuni iliyoshindwa kutekeleza makubaliano kabla kuchukuliwa maamuzi ya kupewa kampuni nyengine. Serikali imeona ingawa Baraza la Manispaa wametumia kifungu ……. cha makubaliano, lakini kifungu …… kinalitaka Baraza kuuarifu upande mwengine wa makubaliano kuhusu maamuzi yake. Serikali tayari imeshaanza kuchukua hatua za kisheria kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa kutokana na vitendo vyake vya kushindwa kufuata Sheria na Kanuni zilizopo nchini.


Mheshimiwa Spika, Serikali imekubaliana na mapendekezo ya Kamati Teule ya kufuata Sheria na Kanuni katika uandaaji na utekelezaji wa mikataba na tayari imetoa maelekezo kwa Baraza la Manispaa kuipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mikataba yote kabla ya kusainiwa kwa ushauri na maelekezo zaidi.


Hoja Nambari 3: Suala la mabango, uendeshaji wake na mapato yake yanaamuliwa kibinafsi zaidi kutokana na kutowekwa chini ya Kamati yoyote kati ya Kamati za Baraza la Manispaa.


Mheshimiwa Spika, Kamati yako katika hoja hii, ilipendekeza kuimarishwa usimamizi wa fedha katika kazi za uwekaji wa mabango ya matangazo.


Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na mapendekezo ya Kamati Teule na tayari imelitaka Baraza la Manispaa kuandaa na kutekeleza mpango bora wa usimamizi wa miradi ya Baraza ikiwemo uwekaji wa mabango ya matangazo ili kuimarisha mapato ya Baraza la Manispaa. Aidha, Serikali imelitaka Baraza kuhakikisha kwamba biashara ya uwekaji wa mabango ya matangazo inafanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Serikali ya mwaka 2005 ikiwa ni pamoja na kutangaza zabuni.


Hoja Nambari 4: Mheshimiwa Spika, hoja hii ilikuwa na vipengele viwili ambavyo ni:


  1. Gharama walizotumia Kampuni ya SYSCORP haziendani na gharama halisi ya kazi ya ushushaji wa mabango, mbali ya kwamba, Kamati ilijiridhisha kwamba hakukuwa na mabango yaliyokuwa yanahitaji kushushwa kwa wakati ule.


  1. Mkataba wa Baraza na Kampuni ya SYSCORP ulifungwa wakati Baraza la Manispaa lilopita limemaliza muda wake na Baraza jipya halijazinduliwa na hivyo kushindwa kupata azimo la Baraza.


Mheshimiwa Spika, katika hoja hii, Kamati Teule pia lilipendekeza kuimarishwa kwa usimamizi wa uwekaji wa mabango ya matangazo.


Mheshimiwa Spika, Serikali imeona kuwa haikuwa sahihi kwa Baraza la Manispaa kuitoza Kampuni ya SYSCORP gharama kwa kazi ya ushushaji wa mabango kwa sababu kimsingi Kampuni hiyo ilipaswa ikabidhiwe eneo safi ambalo halina mabango ya matangazo.  Hata hivyo kwa kuwa Kampuni ya SYSCORP walikubali kulipa gharama hizo, kama sharti la kupatiwa eneo hilo, ni dhahiri kwamba yalikuwepo makubaliano ya pande mbili na hivyo Serikali inaona hili halikuwa tatizo.


Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo hayo, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kurekebisha mikataba yake na kampuni mbalimbali ili kuweka bayana kwamba kampuni yoyote itakayoweka mabango itakuwa na wajibu wa kuyashusha mara mkataba utapomalizika au endapo utakatishwa kwa sababu yoyote ile. Vilevile, Baraza limetakiwa kufuata kikamilifu Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma Nam. 9 ya 2005.  


Hoja Nambari 5: Baraza la Manispaa kujenga Bwawa la Michenzani kwa Sh.  19,000,000 bila ya kuwa na bajeti ya ujenzi wa Bwawa hilo.


Mheshimiwa Spika, maoni ya Kamati Teule kuhusu hoja hii ni kwamba Baraza la Manispaa lilipaswa kuwasilisha nyongeza ya makisio kama Kanuni ya 68 ya Baraza la Manispaa inavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali imeona kwamba matumizi yaliyofanyika ya Sh. 19,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Michenzani yalikuwa ndani ya Bajeti ya Mwaka iliyoidhinishwa na Baraza hili na hivyo hapakuwa na haja ya kuombwa bajeti ya ziada (supplementary budget). Hata hivyo, kutokana na hoja ya Kamati yako Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kufuata Sheria na Kanuni zilizizopo kuhusu matumizi ya fedha ikiwemo kufuata taratibu za uhaulishaji wa fedha kwa matumizi mengine ya vifungu vilivyoombewa bajeti hiyo.


Hoja Nambari 6: Mheshimiwa Spika, hoja hii ilikuwa na vipengele vinne kama ifuatavyo:


  1. Utaratibu wa Baraza la Manispaa kuwa ni lazima maombi ya matumizi yapitie kwa Afisa Utawala au Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ambae nae baada ya kuyaidhinisha lazima ampe nakala Afisa Utawala. Hali hii inaonesha kwamba Afisa Utawala ndio mwenye uwezo (Power) kuliko mtu yeyote katika kuidhinisha matumizi ya Baraza la Manispaa.


  1. Katika Baraza la Manispaa hakuna utaratibu maalum unaotumika wakati wa kuidhinisha matumizi, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za fedha.


  1. Kutokuundwa kwa Kamati ya kudumu ya kuratibu na kuthibitisha masuala ya fedha ndani ya Baraza la Manispaa, jambo ambalo ni matakwa ya Sheria Nambari 3 ya 1995 limekuwa ni jambo la kawaida kwa miaka mingi, hivyo hupelekea kutumika fedha za wananchi kinyume na masharti ya sheria.


  1. Maamuzi ya matumizi ya fedha na maamuzi mengine yanayotolewa na Kamati za Kudumu za Baraza la Manispaa hayawasilishwi mbele ya Baraza zima.
Mheshimiwa Spika, Katika kuzitafutia ufumbuzi hoja hizi, Kamati Teule ilipendekeza kuwa Afisa Utawala awe na hadhi sawa na Wakuu wengine wa Idara na kuwe na utaratibu maalum unaofuatwa wakati wa kuomba na kuidhinishwa matumizi ya fedha za Baraza. Aidha, Kamati ilipendekeza kuwa shughuli ya utawala na utumishi ziendelee kuwa chini ya Mkurugenzi isipokuwa ateuliwe Afisa Maalum wa kumsaidia Mkurugenzi katika masuala hayo ambaye hatokuwa na mamlaka sawa au zaidi ya wakuu wa Idara waliotajwa ndani ya Sheria.


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule pia ilipendekeza kwa kuwa Kamati za Kudumu hushughulikia zaidi masuala ya kisekta ni vyema maamuzi yanayotolewa na Kamati hizi yawasilishwe mbele ya Baraza zima ili kutekeleza dhana ya uwajibikaji wa pamoja na utawala bora. Aidha, Kamati ilipendekeza kuwepo na kanuni inayokidhi matakwa ya kifungu 23 cha Sheria namba 3 ya 1995 kuhusu kuundwa kamati ya kudumu ya kuratibu na kudhibiti masuala ya fedha.


Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na hoja na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule na tayari imeliagiza Baraza la Manispaa kufuata matakwa ya kisheria katika kutekeleza majukumu yake ikwemo kuundwa kwa Kamati ya Kudumu ya Mipango na Fedha ya Baraza. Aidha, tayari Baraza la Manispaa limesharekebisha mapungufu yaliyokuwepo na sasa Idara zote za Baraza zina hadhi sawa na umeandaliwa utaratibu wa kila Mkuu wa Idara kuwasilisha maombi ya Idara yake moja  kwa moja kwa Mkurugenzi na baada ya maombi hayo kuidhinishwa hupelekwa kwa Mhasibu kwa ajili ya malipo.



Mheshimiwa Spika, kuhusu pendekezo la Kamati la kuteuliwa kwa Afisa Maalum wa kumsaidia Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa katika shughuli za Utawala na Utumishi, suala hili litazingatiwa na kuchukuliwa hatua ipasavyo.



Hoja Nambari 7: Hakuna utaratibu maalum unaotumiwa na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa kuwasilisha Ripoti ya Fedha na Ripoti ya Utendaji kwa Waheshimiwa Madiwani wa Baraza hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja ya kuwepo na utaratibu maalum wakati wa kuomba na kuidhinisha matumizi, Serikali inakubaliana na Kamati Teule kwamba huko nyuma haukuwepo utaratibu mzuri wa Mkurugenzi wa Manispaa kuwasilisha ripoti za fedha na ripoti za utendaji. Naomba kuchukua fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwamba kasoro hiyo hivi sasa haipo tena na Baraza la Manispaa linafuata utaratibu wa kuwasilisha ripoti za fedha na utendaji kwa Waheshimiwa Madiwani kikamilifu.

Hoja Nambari 8: Mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule kuhusu kuoanisha vifungu 49(1) (c) na 51 ya Sheria ya Baraza la Manispaa.
Mheshimiwa Spika, upungufu ulionekana na Kamati Teule ya Baraza lako Tukufu katika hoja hii hauzuii utendaji kazi wa Baraza la Manispaa. Hata hivyo, Serikali imepokea ushauri wa Kamati na ushauri huo utazingatiwa wakati wa kufanya mapitio ya Sheria ya Serikali za Mitaa.


Hoja Nambari 9:  Mheshimiwa Spika, hoja hii ilihusisha maeneo matatu kama ifuatavyo:


  1. Watendaji wa Baraza la Manispaa wakiongozwa na Mkurugenzi hufanya manunuzi kwa kuwatumia watu binafsi badala ya kampuni jambo ambalo linaleta hisia kuwa na maslahi binafsi.


  1. Takriban Shughuli nyingi za manunuzi katika Baraza la Manispaa hufanywa bila ya kutolewa zabuni kinyume na  ilivyoelezwa na Kanuni ya 55, 56 na 57. Sharti la kutangaza zabuni pia linamfunga Mkurugenzi kwa mujibu wa Kifungu cha 11(2) cha Sheria Nambari 3 ya 1995 kinachomtaka azingatie sheria nyengine zote za nchi ambapo akiwa Afisa muwajibikaji mkuu wa masuala ya fedha anapaswa kuzingatia Sheria ya Manunuzi na Uuzaji wa Mali za Umma Nambari 9 ya 2005.


  1. Afisa ununuzi hashirikishwi katika kufanya ununuzi mbali mbali kwa ajili ya Baraza la Manispaa.



Mheshimwa Spika, Kamati Teule katika hoja hii ilipendekeza kuwa Baraza la Manispaa lifuate Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma na Kanuni zake wakati wa kununua na kuuza mali za Baraza la Manispaa. Vile vile, Kamati ilipendekeza kuwa Afisa Ununuzi wa Baraza la Manispaa ashirikishwe wakati wa ununuzi na asitumike kuziba mianya ya ukiukwaji wa sheria.


Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii, Serikali imelifuatilia kwa kina suala hili na kuona kwamba Baraza la Manispaa tayari limeanza kutekeleza Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma Nambari 9 ya 2005 kwa kuanzisha Kitengo cha Ununuzi (PMU). Hata hivyo, imeonekana kuwepo na utata wa kisheria kuhusu suala zima la uundwaji wa Bodi ya Zabuni kwa sababu taasisi zenye hadhi ya Shirika la Umma (body corporate) kama ilivyo kwa Baraza la Manispaa hutakiwa kuwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo ndiyo inayoteuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni. Kwa sasa Sheria ya Baraza la Manispaa haina kifungu kinachoruhusu kuwa na Bodi ya Wakurugenzi na Baraza la Madiwani liliopo haliwezi kuchukua nafasi hiyo kwa vile ni la wanasiasa.  


Mheshimiwa Spika, Serikali itazingatia suala hili wakati wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma, 2005 ili Sheria hiyo itakayofanyiwa marekebisho iweze kutumiwa na Serikali za mitaa katika kufanya manunuzi na kuuza mali za Baraza.  Kwa sasa Ofisi ya Mwanansheria Mkuu tayari imeshalishauri Baraza la Manispaa kuunda bodi yake ya zabuni kwa kuwatumia wakuu wa Idara kuwa ndiyo wajumbe wa bodi hiyo kama utaratibu unavyotumika kwa Idara zinazojitegemea.


Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ushiriki wa Afisa Ununuzi katika masuala ya ununuzi, naomba kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba hivi sasa Afisa huyo anashirikishwa kikamilifu katika kufanya kazi hiyo. Aidha, katika jitihada za kukiimarisha Kitengo cha Manunuzi cha Baraza la Manispaa (PMU), Baraza limepeleka masomoni wafanyakazi wake wawili ambao wanasomea Diploma ya Ununuzi na Ugavi na watapokamilisha mafunzo yao na kurudi kazini watasaidia sana katika kuimarisha huduma na usimamizi wa ununuzi katika Baraza la Manispaa.


Hoja Nambari 10: Mheshimiwa Spika, hoja hii ilikuwa na vipengele vinne kama ifuatavyo:


  1. Wafanyabiashara ambao wametoa pesa zao kujenga vibaraza kwenye Soko la Mwanakwerekwe, hawakufahamishwa kwa uwazi utaratibu wa jenga, endesha na haulisha (Build, Operate and Transfer- BOT) ambao ndio uliotumika kujenga vibaraza hivyo.


  1. Kamati ina wasiwasi juu thamani halisi (value for money) ya ujenzi wa vibaraza na meza katika soko la Mwanakwerekwe.


  1. Ingawa wafanyabiashara walilipa asilimia 80 ya fedha zote walizotakiwa kulipa (Shilingi 400,000 kati ya Shilingi 500,000) kwa Mkandarasi, jambo la kustaajabisha ni kwamba walitakiwa kufunga mkataba na Baraza la Manispaa badala ya Mkandarasi huyo.


  1. Ingawa Mkurugenzi na Mkandarasi walieleza kuwa wakodishwaji wa vibaraza na meza wamelipa baada ya vibaraza na meza kujengwa, Kamati imebaini kuwa kauli hizo sio sahihi na badala yake kauli za wakodishwaji ndio zenye ukweli. Kamati imetamka hivyo, baada ya kuangalia tarehe zilizotolewa risiti na tarehe ya kufungwa mikataba.


  1. Kutokana na kasoro mbali mbali zilizojitokeza kwenye mikataba inadhihirisha wazi kuwa Watendaji wa Baraza la Manispaa wakiongozwa na Mkurugenzi hawapo makini wakati wa kufunga mikataba.


  1. Kamati Teule imeona sio kweli kwamba Mkandarasi alipeleka barua ya kuomba kupewa vibaraza kwa wale wafanyabiashara walioshindwa kulipa fedha.


Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Mkurugenzi amemruhusu Mjenzi kujenga bila ya kufuata taratibu za kisheria, Kamati inapendekeza aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza, Ndugu Rashid Ali Juma achukuliwe hatua za kinidhamu. Pia Kamati imependekeza Mkurugenzi huyo pamoja na Ndugu Khamis Ali Khamis (Mjenzi wa vibaraza) wachukuliwe hatua za kisheria kwa kutoa ushahidi wa uongo mbele ya Kamati hii kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha Sheria namba 4 ya 2007.



Mheshimiwa Spika, vilevile, Kamati imependekeza Mkurugenzi na watumishi wa Baraza waliohusika katika makosa yaliyobainika katika mikataba wachukuliwe hatua za kisheria. Aidha, Kamati imetoa ushauri kwa viongozi wa Baraza kuwa makini wakati wa kufunga mikataba ili kulinda uhalali wa mikataba hiyo.


Mheshimiwa Spika, Kuhusu suala la kumchukulia hatua za kinidhamu aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, Ndugu Rashid Ali Juma, hatua hizo hazitoweza kuchukuliwa kwa vile mhusika amelazimika kujiuzulu wadhifa wake huo, kutokana na uamuzi wake wa kuchukua nafasi ya uongozi katika Chama cha Siasa. Aidha, Serikali imelishauri Baraza la Wawakilishi kuwasilisha shauri linalohusu wahusika kutoa ushahidi wa uongo mbele ya Kamati kwa Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la wafanyabiashara kufunga mkataba na Baraza la Manispaa badala ya Mkandarasi, Serikali imeamua kulifikisha suala hili Polisi kwa uchunguzi zaidi na endapo itabainika kuna Sheria zilizokiukwa wahusika wachukuliwe hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria. Vile vile, Baraza la Manispaa limetakiwa kuwasilisha rasimu za mikataba yote katika Ofisi ya Mawanasheria Mkuu kwa kupitiwa na kushauriwa ipasavyo.



Hoja Nambari 11: Mheshimiwa Spika, hoja hii, ilikuwa na vipengele viwili kama ifuatavyo:
  1. Kutokufuatwa utaratibu wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa vibaraza katika soko la Mwanakwerekwe na kutotangazwa kwa zabuni ya ujenzi huo jambo ambalo ni kinyume na kifungu 55(b) cha Kanuni za Baraza la Manispaa pamoja na Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma ya 2005.

  1. Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa amehusika na mgogoro baina ya Baraza la Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi kutokana na kitendo chake cha kukusanya ada ya leseni kwa wafanyabiashara wa ndani wa soko la Mwakwerekwe. Jambo lililopelekea Mheshimiwa Waziri wa Wizara husika kutoa agizo la kumtaka Mkurugenzi huyo kurejesha fedha hizo ambazo ni Shilingi 10,000,000. Hadi taarifa hii inakamilika fedha hizo zilikuwa hazijarejeshwa.


Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Kamati Teule imependekeza kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma, kwa kitendo chake cha kuruhusu ujenzi kufanyika bila ya kufuata utaratibu wa kisheria. Serikali imeona umuhimu wa pendekezo la Kamati Teule na tayari imeliandikia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi juu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma.
Aidha, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kuilipa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi fedha za leseni ilizozikusanya kutoka kwa wafanyabiashara waliopo katika soko la Mwanakwerekwe ili kuondosha mzozo uliopo baina ya Baraza la Manispaa na Halmashauri ya Wilaya Magharibi. Aidha, Serikali imeelekeza kwamba wafanyabiashara wanaotumia masoko yaliyopo katika Wilaya ya Magharibi wakate leseni zao za biashara katika Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi na Baraza la Manispaa liwatoze kodi ya matumizi ya eneo.  


Hoja Nambari 12: Mheshimiwa Spika, katika hoja hii Kamati Teule iliibua maeneo matano yenye mapungufu kama ifuatavyo:


  1. Baadhi ya Madiwani walijichukulia maeneo ya maduka katika Soko la Mwanakwerekwe kinyume cha utaratibu na kuwakodisha wafanyabiashara kwa maslahi yao binafsi.


  1. Baadhi ya Madiwani huzitumia Kamati za Kudumu za Baraza la Manispaa kuwa ni vitega uchumi vyao.


  1. Kitendo cha Madiwani kutafuta wateja wa kukodi maduka hayo kinaashiria kuwa Madiwani huchangia kwa asilimia kubwa ukiukwaji wa Sheria kwa maslahi yao binafsi.


  1. Kuna ukiukwaji mkubwa wa maadili ya kazi na utumiaji mbaya wa madaraka.  


  1. Kamati ya Kudumu ya Kazi za Ujenzi na Mazingira ya Baraza la Manispaa hutumiwa vibaya na Madiwani kama ni sehemu ya kujipatia maslahi yao.


Mheshimiwa Spika, katika kulishughulikia suala hili, Kamati imependekeza kwamba Madiwani hao wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa makosa ya kujipatia fedha kinyume na sheria. Aidha, kwa kuwa mikataba iliyowekwa imekiuka masharti ya kifungu cha 20(2) cha Sheria nambari 3 ya 1995, Kamati imependekeza kufungwa upya mikataba hiyo kama ilivyoelekezwa na kifungu hicho cha Sheria. Vilevile, kamati imependekeza kuwa watendaji wa Baraza waliohusika na ufungaji wa mikataba kinyume na sheria wachukuliwe hatua za kisheria.


Mheshimiwa Spika, kuhusu pendekezo la kuwachukulia hatua za kisheria Madiwani waliohusika na uchukuaji wa maduka na kukodisha kinyume na taratibu, Serikali haina mamlaka ya moja kwa moja ya kuwachukulia hatua za kinidhamu madiwani hao. Ni vyema ikafahamika kwamba Suala hili limechangiwa zaidi na kutokuwepo kwa Sheria ya Maadili. Hata hivyo, Serikali hivi sasa imo katika hatua za matayarisho ya Sheria ya Maadili ambayo itatumika kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wanaokiuka maadili ya uongozi.
 


Mheshimiwa Spika, Suala hili vilevile litazingatiwa wakati wa utayarishaji wa Sheria mpya ya Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali imemuagiza Waziri mwenye mamlaka ya Tawala za Mikoa kukutana na Waheshimiwa Madiwani na kuwaelimisha juu ya njia sahihi za kutekeleza majukumu yao. Pia, Serikali itaviarifu vyama vya siasa vya madiwani hao kuvitaka kuzungumza na madiwani wao juu ya haja ya kuheshimu sheria zilizopo nchini.


Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza awali kwamba Serikali imeliagiza Baraza la Manispaa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kufanya mapitio ya mikataba yote na kasoro zozote zitakazobainika zirekebishwe kwa mujibu wa sheria zilizopo.


Hoja Nambari 13: Baraza la Manispaa halikuwapatia risiti baadhi ya wakodishwaji baada ya kufanya malipo mbali mbali yakiwemo ya leseni.  Kitendo hicho ni kinyume na kifungu Nambari 3 cha Mkataba wa ukodishaji.


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule imebaini kwamba wapo baadhi ya wafanyabiashara waliolipa pesa zao kwa ajili ya kukodishwa maduka ila hawakupatiwa risiti. Kutokana na kasoro hii, Kamati Teule imependekeza kuchukuliwa hatua kwa wale wote waliobainika kutofuata Sheria na Kanuni za Baraza la Manispaa.
Mheshimiwa Spika, ingawa suala hili halijawekwa wazi, Serikali inawataka wale wote ambao walilipa fedha zao na hawakupatiwa risiti wajitokeze ili hatua za kisheria na kinidhamu ziweze kuchukuliwa.


Hoja Nambari 14: Mheshimiwa Spika, hoja hii ina vipengele viwili ambavyo ni:


  1. Kitendo cha kuwatoza ada ya usafi wafanyabishara wanaopanga biashara zao ndani na nje ya maduka ni cha dhulma. Hii ni kutokana na kuwa ndani ya duka Baraza la Manispaa halitoi huduma ya usafi.


  1. Pamoja na kuwepo Mikataba kwa wafanyabiashara waliokodishwa milango ya maduka, Kamati imebaini kuwa Mikataba hiyo ina mapungufu kadhaa.


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule katika hoja hii imelitaka Baraza la Manispaa liache kuwatoza mara mbili ada ya usafi wafanyabiashara wanaoweka biashara zao nje na ndani ya duka. Aidha, Kamati imependekaza kuwa Serikali ichukuwe hatua kwa wale wote waliobainika kutofuata sheria na kanuni za Baraza la Manispaa pamoja na Sheria nyengine zinazohusiana na manunuzi. Kamati pia imependekeza kuwa Baraza la Manispaa lipitie upya mikataba yote iliyofungwa kipindi kilichopita ili ijiridhishe na utaratibu uliotumika.




Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali tayari imeliagiza Baraza la Manispaa pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuipitia mikataba iliyoingia Baraza la Manispaa na Wafanyabiashara mbalimbali na kuchukua hatua zinazofaa.


Aidha, Serikali kupitia Wizara husika itaandaa utaratibu wa kuwahoji wakodishwaji na kuwatambua watendaji waliohusika na tatizo hili na ikithibitika kuwa wamefanya makosa hayo, wahusika wote watachukuliwa hatua za kisheria.  Nachukua fursa hii pia kueleza kwamba Serikali inawashauri wafanyabiashara wanaohisi wamedhulumiwa kwa kutozwa ada ya usafi bila ya kupata huduma hiyo, wafuate utaratibu wa kisheria kwa kupeleka malalamiko yao Mahakamani kwani Baraza lina hadhi ya Shirika na linaweza kushitaki na kushitakiwa.


Hoja nambari 15: Kipengele cha 3 cha Mkataba kimemtaka Mkodishwaji kulipia ada ya huduma ya usafi ya Shilingi 90,000 kwa mwezi wakati hali halisi analipia Shilingi 40,000.


Mheshimiwa Spika, katika hoja hii, Kamati Teule imependekeza kuwa watendaji wa Baraza waliohusika na suala hili wachukuliwe hatua za kisheria.


Mheshimiwa Spika, Serikali imebaini kwamba Mkataba wa Baraza la Manispaa una vifungu viwili tofauti ambapo kimoja kinahusiana na ukodishwaji wa mlango na chengine kinahusu usafi. Hivyo, Serikali haikurudhika na maelezo yaliyotolewa na  Baraza la Manispaa na inaendelea kulifanyia kazi suala hili ili kupata ukweli wake. Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu na kisheria wale wote watakaobainika kuwa na makosa katika hoja hii.  


Hoja Nambari 16: Mheshimiwa Spika, hoja hii ilikuwa na vipengele vinne ambavyo ni:
  1. Bw. Rashid Khalfan Ali ameshindwa kulipa asilimia 20 ya kodi ya milango miwili kwa kipindi chote alichokodishwa na Baraza la Manispaa. Kwa upande mwengine Baraza la Manispaa limeshindwa kulipa gharama za ujenzi wa mlango mmoja hadi sasa.


  1. Bw. Suleiman Msellem Nassor ameshindwa kulipa asilimia 20 ya kodi ya milango miwili kwa kipindi chote alichokodishwa na Baraza la Manispaa. Kwa upande mwengine Baraza la Manispaa limeshindwa kulipa gharama za ujenzi wa milango minane.


  1. Wajenzi hawakulipwa gharama za fedha ambazo wamezitumia katika ujenzi.


  1. Wajenzi wametumia gharama kubwa (zaidi ya walichokubaliana na Baraza la Manispaa) kinyume na makubaliano kutokana na maelekezo mabaya ya Mshauri wa Ujenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu Abdulkadir.
Mheshimiwa Spika, katika hoja hii, Kamati imependekeza kuwa Watendaji wa Baraza la Manispaa wachukuliwe hatua za kisheria.


Mheshimiwa Spika, kutokana na hoja hii, Serikali imebaini kwamba Baraza la Manispaa limeshindwa kulipa gharama za maduka tisa (9) na hivyo kuwashauri wajenzi wa maduka hayo Ndugu Rashid Khalfan Ali na Ndugu Suleiman Msellem Nassor kuyapeleka mashauri yao Mahakamani kulishtaki Baraza la Manispaa. Vyenginevyo, Baraza hilo lifikirie kuwalipa wajenzi hao fedha wanazodai.


Mheshimiwa Spika, Hoja Nambari 17 ina vipengele mbalimbali kama ifuatavyo:


  1. Baraza la Manispaa limefunga mkataba wa ujenzi na watu mbali mbali ambao ni Kampuni ya F&K Enterprises Limited, Ndugu Rashid Khalfan Ali na Ndugu Suleiman Msellem Nassor pamoja na waliokodishwa maduka. Hivyo, Kamati ilishindwa kujua mjenzi halisi wa maduka hayo.

  1. Kampuni ya F&K imesajiliwa kisheria isipokuwa kwa mujibu wa kipengele cha 3(a)-(r) cha “Memorundum of Association” Kampuni hii haina jukumu la kufanya shughuli za usafi pamoja na shughuli za ujenzi.


  1. Baraza la Manispaa kutokuwa na mikataba ya kimaandishi    na Bw. Suleiman Msellem Nassor kuhusu ujenzi wa maduka yote kumi.


  1. Wakodishwaji wamejazishwa mikataba kama wao ni   wajenzi wa maduka hayo na wanalipa asilimia sawa na waliojenga.


  1. Baraza la Manispaa limeshindwa kutimiza ahadi ya kuwapatia milango wafanyabiashara waliokuwa wanatumia eneo hilo (wauza ndizi).


  1. Ujenzi wa maduka haya umekosesha baadhi ya wananchi ajira jambo ambalo limepelekea hali zao za maisha kuwa ngumu.


Mheshimiwa Spika, Serikali katika kulifuatilia suala hili imeona kuna utata mkubwa katika suala zima la ujenzi wa maduka katika eneo la Darajani kama ilivyobainishwa na Kamati Teule. Miongoni mwa mambo yaliyoleta utata ni kutokuwepo kwa mkataba halali baina ya Baraza la Manispaa na F&K Enterprises Limited. Serikali imeiagiza Wizara husika ichukue hatua za kisheria dhidi ya Ndugu Ramadhan Abdalla Songa kwa kukodisha maduka na kuchukua fedha za wafanyabiashara wakati akijua fika kuwa siyo yeye aliyejenga maduka hayo.


Kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya 2007, Serikali inalishauri Baraza la Wawakilishi kuwasilisha Polisi na kwa Mkurugenzi wa Mashtaka suala la kumchukulia hatua za kisheria Ndugu Vuai Ame Vuai kwa kutoa maelezo yanayotofautiana mbele ya Kamati kwa lengo la kuipotosha Kamati. Kama ilivyoelezwa hapo awali, Serikali pia imeona haja ya kuchukuliwa hatua za kisheria aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma kutokana na sababu za kukiuka Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma pamoja na Kanuni zake. Aidha, Serikali itazingatia ushauri uliotolewa na Kamati Teule juu ya kuwawezesha walioathirika. Hii itafanyika baada ya kujua idadi kamili na mahitaji ya waathirika hao. Baraza la Manispaa tayari limeagizwa kuanza kulifanyia kazi suala hili.


Hoja Nambari 19, 20 na 21: Baraza la Manispaa halikuingia Mkataba na Kampuni ya F & K Enterprises Limited kuhusu ujenzi wa maduka 13 katika Soko la Darajani na Shughuli za ujenzi wa maduka 13 katika Soko la Darajani ilifanywa bila ya kutangazwa zabuni jambo ambalo ni kinyume na Kanuni ya 55(b) ya Kanuni za Baraza la Manispaa na Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma nambari 9 ya 2005. Aidha, Wakodishwaji wengine ambao sio wajenzi (mbali na Rashid na Suleiman) wamejazishwa mikataba sawa na wengine ya kujilipa asilimia 80 na kulilipa Baraza asilimia 20 wakati wao sio wajenzi.


Mheshimiwa Spika, katika hoja hizi, Serikali imeona utata mkubwa katika ujenzi wa maduka ya Soko la Darajani na tayari Serikali imeanza kuchukua hatua kwa kuliwasilisha suala hili katika Jeshi la Polisi dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma kwa uchunguzi zaidi. Na iwapo itathibika kwamba Mkurugezi huyo alifanya makosa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


Hoja Nambari 22: Ugawaji wa maduka ya kufidia wajenzi haukuzingatia idadi ya ujenzi wa maduka (wajenzi wote wamepewa maduka mawili) jambo ambalo ni kinyume na makubaliano yao. (Mjenzi aliojenga maduka matatu amepewa mawili na aliojenga maduka kumi kapewa mawili).


Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na hoja ya Kamati Teule na kuona kuwa hakukua na utaratibu mzuri katika ugawaji wa maduka ya kufidia wajenzi wa maduka hayo. Baraza la Manispaa limetakiwa kuwa makini katika kufuata Sheria na Kanuni katika utendaji wa shughuli zake.


Hoja Nambari 23: Mheshimiwa Spika hoja hii ilihusisha vipengele nane (8) kama ifuatavyo:


  1. Baraza la Manispaa kutotangaza Zabuni ya Ujenzi wa Maduka 16 katika Soko la mbogamboga Darajani.


  1. Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa alishindwa kutekeleza matakwa ya Kifungu cha 29(2) cha Sheria Nambari 3 ya 1995 kinachomtaka aendeleze mikataba halali aliyoirithi.


  1. Maeneo yaliyokuwa na masoko hujengwa majengo ya kudumu (maduka) jambo ambalo huondosha dhamira ya kuwa na masoko.


  1. Baadhi ya vipengele vya mkataba havikujazwa.


  1. Kipengele cha 14(c) cha mkataba kinachoeleza kwamba mkodishwaji (mjenzi) akodishe maduka kwa watu wengine kwa makubaliano na mkodishaji (Manispaa) hakifuatwi. Hii ni kutokana na kuwa mkodishwaji amewakodisha watu bila ya kutoa taarifa kwa mkodishaji.


  1. Shughuli za ujenzi imetolewa bila ya kufuatwa taratibu za zabuni jambo ambalo ni kinyume na Kanuni ya 55(b) ya Baraza la Manispaa pamoja na Sheria ya Manunuzi na Uuzaji wa Mali za Umma.


  1. Ujenzi wa maduka haya umewakosesha ajira wananchi na baadhi yao kubakia kutangatanga mitaani na wengine kujibana kwa wenzao na kupelekea kushuka kwa shughuli za biashara.


  1. Baraza lilishindwa kutimiza ahadi lililoitoa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakitumia eneo lile.


Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii, Kamati Teule imependekeza kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kutofuata sheria za nchi na imelitaka Baraza la Manispaa kulipa gharama alizotumia Ndugu Ussi Ame Pandu wa SLP 318 kwa mujibu wa thamani ya soko. Sambamba na hilo, Baraza la Manispaa limlipe fidia Ndugu Ussi kwa usumbufu alioupata.


Mheshimiwa Spika, tayari nimeshatoa maelezo ya Serikali kuhusu hoja hii. Kimsingi Serikali inakubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule ikiwa ni pamoja na kulitaka Baraza la Manispaa kufuata Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma katika masuala yote ya manunuzi hata kama inatumia utaratibu wa BOT.  Aidha, Serikali haioni haja ya kulipwa Ndugu Ussi Ame Pandu kwa sababu taratibu za kisheria hazikufuatwa katika kufikia makubaliano.


Hoja Nambari 24: Mheshimiwa Spika hoja hii ina vipengele vinne (4) kama ifuatavyo:
  1. Mkodishwaji wa Bustani ya Jamhuri (Bi Asya Moh’d Bafadhil) anatumia gharama kubwa kinyume na alivyotarajia na kwamba kipato kinachopatikana ni kidogo.


  1. Kuna utata kuhusu tarehe ya kuanza kwa mkataba wa ukodishwaji wa Bustani ya Jamhuri ambapo risiti zinaonesha kwamba wameanza kulipa tokea tarehe 1 Aprili, 2010 wakati Mkataba umeanza tarehe 1 Novemba, 2010.
  2. Shughuli za ujenzi katika Bustani ya Jamhuri imetolewa bila ya kufuatwa taratibu za zabuni jambo ambalo ni kinyume na Kanuni ya 55(b) ya Baraza la Manispaa pamoja na Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali za Umma.


  1. Kitendo cha Mkurugenzi kutamka kuwa mali za Serikali hazikodishwi zaidi ya miaka kumi ni kinyume na Kifungu cha 47 cha Sheria ya Ardhi Nambari 12 ya 1992 kama ilivyorekebishwa na Kifungu cha 6 cha Sheria Nambari 11 ya 2010. Hii ni kutokana na kuwa kifungu hicho kinaruhusu mali ya Serikali kukodishwa si zaidi ya miaka 99.


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule katika hoja hii imependekeza kwamba Watendaji wa Baraza la Manispaa wakiongozwa na Mkurugenzi wafuate Sheria na Kanuni mbali mbali za nchi pamoja na kumtaka Mkurugenzi huyo awe mwangalifu na kauli zake anazozitoa. Aidha, kwa kuwa Mkodishwaji alishindwa kutoa maelekezo ya kina mbele ya Kamati kuhusiana na malipo aliyofanya ya tarehe 1 Aprili, 2010 Kamati inashauri kuwa mkataba huo uanze mwezi huo. Vilevile Kamati imependekeza kuwa Baraza la Manispaa kuwa makini wakati linapoingia na kufunga mikataba ili kuleta tija


Mheshimiwa Spika, katika hoja hii, Serikali imeona kwamba ingawa kwa mujibu wa Kamati Teule Mkodishwaji anatumia gharama kubwa na kipato anachokipata ni kidogo bado anasisitiza kuendelea na mkataba huo. Hii inaonesha wazi kuwa Mkodishwaji huyo anapata faida vyenginevyo asingesisitiza kuendelea na mkataba huo. Mheshimiwa Spika pamoja na mtizamo huu, Serikali inakubaliana na pendekezo la Kamati Teule kwamba Baraza la Manispaa kutakiwa kufuata Sheria na Kanuni na imelitaka Baraza kufanya hivyo. Aidha, Serikali imemtanabahisha Mkurugenzi aliyekuwepo hivi sasa kuwa makini na kuzingatia ipasavyo Sheria na Kanuni zake na kwamba kwa wakati wote Baraza liwe makini na hasa wakati wa kuingia na kufunga mikataba ili kuleta tija kwa Baraza la Manispaa. Kuhusu hoja kwa Mkodishwaji kutoa malipo kabla ya kuanza kwa mkataba, Serikali haikuona tatizo kwa jambo hilo kwani Mkataba uliotiwa saini ndio msingi mkuu na unapaswa kuheshimiwa.


Hoja Nambari 25: Kamati imeona kwamba mkataba wa ukodishwaji wa Bustani ya Jamhuri hauna tija kwa Baraza la Manispaa


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ya Baraza lako Tukufu, imependekeza kuwa Baraza la Manispaa liwe makini wakati linapoingia na kufunga mikataba ili kuleta tija.


Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na hoja hii ya Kamati Teule na imeona ni kweli Mkataba wa Ukodishwaji wa Bustani ya Jamhuri hauna maslahi kwa Baraza. Mkataba huo ni miongoni mwa mikataba itakayoangaliwa upya kwa msaada wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, Baraza la Manispaa kwa mara nyengine tena limetakiwa kuwa makini wakati linapoingia na kufunga mikataba.


Hoja Nambari 26: Mheshimiwa Spika, katika hoja hii, Kamati Teule imebainisha kasoro sita (6) kama ifuatavyo:


  1. Kampuni binafsi mbali mbali zinapewa kazi na Baraza la Manispaa lakini bado mafundi wa Baraza hutumika kwenye kazi hizo walizopewa Kampuni binafsi kinyume na utaratibu.


  1. Shughuli za ujenzi katika maeneo mengine aliyojenga Ndugu Ali Abdalla Ali zimetolewa bila ya kufuatwa utaratibu wa zabuni kwa zile kazi zenye gharama zinazohitaji hivyo.


  1. Mjenzi alipewa fedha za kununulia miti kinyume na taratibu za manunuzi.


  1. Baraza linanunua vifaa kama vile “bollard”, “paving stone” kwa mtu binafsi wakati lina uwezo wa kutengeneza vifaa hivyo. Pia vifaa vinavyonunuliwa havina ubora ukilinganisha na vile vilivyotengenezwa na Baraza siku za nyuma.


  1. Ingawa ziko barua 3 tofauti zinazoonesha Ndugu Ali Abdalla Ali kulipa gharama alizotumia kwa awamu, hata hivyo, Kamati imebaini kuwa kwa mujibu wa barua hizo malipo yalifanywa ndani ya mwezi mmoja kutokana na tarehe za barua hizo. Jambo ambalo liliitia mashaka kamati. Sambamba na hilo hundi nambari 990385 inaonesha kwamba malipo hayo yalifanywa kwa pamoja. Kutokana na mashaka hayo Kamati ilimtaka aeleze ukweli wa jambo hilo ambapo Ndugu Ali Abdalla Ali alikiri kwamba alilipwa fedha zile kwa pamoja kimakosa na katika kutatua hilo alitakiwa na Baraza kuandika barua zile.


  1. Hakuna mkataba baina ya Baraza la Manispaa na Ndugu Ali Abdalla Ali wa ujenzi katika eneo la Darajani.


Mheshimiwa Spika, katika hoja hii, Kamati Teule imependekeza kuwa Baraza liache tabia ya kukwepa masharti ya Sheria na Kanuni zilizopo na lifuate matakwa ya Sheria na Kanuni hizo. Aidha, Kamati imependekeza kuwa Wafanyakazi wa Baraza la Manispaa wasishirikishwe au wasitumike kwenye kazi zilizopewa Kampuni hata kama kazi hiyo inatakiwa haraka (yaani Kampuni iachiwe itafute mbinu za kumaliza kazi zake kwa wakati). Vilevile, Kamati ilishauri Baraza kukabidhi kazi kwa wataalamu wake ili kuepuka kutumika vibaya fedha za walipa kodi wa nchi hii.


Mheshimiwa Spika, kimsingi Serikali inakubaliana na hoja na mapendekezo ya Kamati Teule na tayari Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kuacha tabia ya kukwepa kufuata masharti ya Sheria na Kanuni. Vile vile, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kutowashirikisha wafanyakazi wake katika kazi zilizopewa Kampuni kwa namna yoyote ile. Baraza la Manispaa pia limeagizwa kutumia wataalamu wake wa fani mbalimbali kufanya kazi za Baraza ili kupunguza kutumika fedha kulipa wataalam wa nje kwa kazi zinazoweza kufanywa na wataalam wa ndani.


Hoja Nambari 27:  Ndugu Ali Abdalla Ali alikuwa Mfanyakazi wa Baraza la Manispaa wakati huo huo alipewa majukumu na kazi binafsi na Baraza la Manispaa kupitia Kampuni yake.


Mheshimiwa Spika, kama ilivyokuwa kwa hoja Nambari 26, Kamati Teule imelishauri Baraza kukabidhi kazi kwa wataalamu wake hao ili kuepuka kutumika vibaya fedha za walipa kodi wa nchi hii.


Mheshimiwa Spika, Serikali imeshangazwa sana na uamuzi wa Baraza la Manispaa wa kumpa mtu kazi ambaye Baraza hilo hilo limemfukuza kazi. Hivyo, Serikali inakubaliana na hoja ya Kamati Teule na kukubali pendekezo lake. Baraza la Manispaa tayari limetakiwa kuachana kabisa na tabia ya kutumia wataalamu wa nje kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa na wataaamu wake wa ndani.
Hoja Nambari 28: Mheshimiwa Spika, katika Hoja hii Kamati Teule imeibua mambo makubwa matatu (3) ambayo yameonekana kuwa ni kasoro katika utendaji wa Baraza la Manispaa. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:


i)     Baraza la Manispaa limenunua basi kwa ajili ya wafanyakazi, kwa njia ya ununuzi     wa     moja kwa moja (direct procurement) kwa kutumia kifungu cha 38(1) cha Sheria Nam. 5     ya 2005 na haikutangaza zabuni. Kamati haikubaliani na     uamuzi wa Mkurugenzi kutumia kifungu hicho kwani ununuzi wa gari haukuhitaji uharaka huo.


ii) Baraza kwa makusudi limekiuka kifungu cha 55 cha  Kanuni ya Baraza ambayo     inamtaka Mkurugenzi kutoa tangazo la kuitisha zabuni katika ununuzi wa basi hilo.


iii) Kauli ya Ndugu Abdalla (muuzaji wa basi) aliyotoa mbele ya Kamati ya kuwa aliliuzia gari mbili Baraza kwa maombi tofauti (katika miezi tofauti) inapingana na     barua ya tarehe 12 Mei, 2010 iliyotumwa na Baraza la Manispaa.


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule katika hoja hii imependekeza kuwa watendaji wa Baraza la Manispaa wakiongozwa na Mkurugenzi wafuate matakwa ya Sheria kikamilifu na sio kuyafumbia macho baadhi ya masharti kwa maslahi yao binafsi. Vilevile, Kamati imependekeza kuwa maamuzi yote ya Kamati za Kudumu za Baraza la Manispaa yawasilishwe kwenye Baraza kwa kuidhinishwa, jambo hili litasaidia kila Diwani kujua kinachoendelea kwenye Baraza la Manispaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na hoja ilizotoa Kamati Teule. Kitendo cha baadhi ya Wafanyakazi wa Baraza kukwepa kufuata Sheria na Kanuni zinazoongoza Baraza hakikubaliki na hivyo Serikali imeshalifikisha suala hili katika Jeshi la Polisi kwa uchunguzi na hatua za kisheria dhidi ya wahusika wote. Aidha, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kuwasilisha maamuzi yote ya Kamati za Kudumu za Baraza kwenye Baraza kwa kuidhinishwa. Hatua hii itasaidia kila Diwani kujua kinachoendelea kwenye Baraza la Manispaa.


Hoja Nambari 29: Mheshimiwa Spika, hoja hii ina vipengele saba (7) kama ifuatavyo:
  1. Sheria na Kanuni za uajiri na upandishwaji vyeo katika Baraza la Manispaa hazifuatwi kwa baadhi ya watendaji.


  1. Ingawa uajiri wa wafanyakazi 83 ulifanywa kinyume na utaratibu lakini uajiri huo ulikuwa sahihi.


  1. Kwa kuzingatia Dokezo la tarehe 30 Septemba, 2009 inadhihirisha wazi kwamba Ndugu Khamis ameteuliwa na Mkurugenzi Rashid kushika wadhifa huo kwa kuwa yeye ndiye aliyetia saini Dokezo hilo.


  1. Utaratibu wa upandishwaji vyeo katika Baraza la Manispaa hauzingatii sifa kwa nafasi husika bali hufanywa kwa upendeleo.


  1. Mkurugenzi anatumia madaraka aliyokuwa nayo kwa maslahi yake binafsi.


  1. Watumishi wa Baraza la Manispaa hawapewi “Job Description” kitu ambacho ni kinyume na taratibu za kazi.


  1. Mkuu wa Idara ya Utawala na Sheria anafanya shughuli zaidi za Afisa Utumishi.


Mheshimiwa Spika, Kamati Teule imetoa mapendekezo mbali mbali katika kusaidia kurekebisha kasoro zilionekana katika Baraza la Manispaa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuwajibishwa na kuchukuliwa hatua aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa Ndg. Rashid Ali Juma kwa mujibu wa Sheria za nchi, Serikali kuiagiza Wizara husika na masuala ya utumishi kuupitia upya muundo wa utumishi wa Baraza la Manispaa kwa lengo la kuweka utaratibu maalum wa upandishaji vyeo pamoja na kuandaliwa sifa za watumishi na watendaji waliopandishwa vyeo bila ya kuwa na sifa husika waondolewe mara moja na kuwekwa wale wanaostahiki. Aidha, pendekezo jengine ni kwamba watendaji wa Baraza watakiwe kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taaluma na maadili yao ya kazi na kuachana na tabia ya kufuata amri za Mkurugenzi.


Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kamati imekiri kuwa uajiri uliofanyika ulikuwa sahihi na kwa kuwa kipindi kilichofanyika ajira hizo Sheria ya utumishi wa Umma ilikuwa bado haijaanza, hivyo Serikali imeona si busara kumchukulia hatua Mkurugenzi. Hata hivyo, Baraza la Manispaa limetakiwa kufuata Sheria za Nchi na Kanuni ilizojiwekea kikamilifu.


Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria namba 4 ya 2007, Baraza la Wawakilishi iliwasilishe Polisi na kwa Mkurugenzi wa Mashtaka suala la kumchukulia hatua za kisheria kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Maanispaa kwa kutoa taarifa za uongo mbele ya Kamati.


Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja ya baadhi ya watendaji wa Baraza la Manispaa kupandishwa vyeo bila ya kuwa na sifa, Serikali imeiona kasoro iliyoibuliwa na Kamati Teule. Ingawa watendaji hao watatu wanazo sifa za kielimu lakini imegundulika kwamba uzoefu wao ni mdogo. Hivyo katika kuliletea ufanisi Baraza la Manispaa, Serikali imeamua kuwaondoa wafanyakazi hao katika nyadhifa zao hizo na nafasi zao kupewa wafanyakazi wengine wenye sifa za kielimu na uzoefu wa kutosha katika kazi.


Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na pendekezo la Kamati Teule la kuwataka watendaji wa Baraza kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taaluma na maadili yao ya kazi. Hata hivyo, watendaji hao ni lazima kufuata amri halali za Mkurugenzi.


Hoja Nambari 31: Mheshimiwa Spika, katika Hoja hii Kamati Teule imeainisha kasoro katika maeneo matano (5). Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:


  1. Maamuzi ya Waziri ya kuliandikia barua Baraza la Manispaa ya kusitisha zoezi la kumhamisha mkodishwaji wa duka la Diplomatic Supermarket ni kinyume na masharti ya kifungu cha 62 cha Sheria Nambari 3 ya 1995. Hii ni kutokana na kuwa kifungu hiki kinamtaka kwanza Waziri afanye uchunguzi wa jambo husika na endapo atagundua kuwa Baraza la Manispaa linatekeleza majukumu yake kinyume na utaratibu basi atoe taarifa kupitia Gazeti Rasmi la Serikali na hatua nyengine ziendelee. Kwa msingi huo kitendo cha Waziri cha kumuongezea muda mkodishwaji hakina uhalali.


  1. Kamati ina wasiwasi juu ya baadhi ya Viongozi akiwemo Mheshimiwa Waziri na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa kupokea fedha kwa ajili ya kutoa maamuzi ya upendeleo.


  1. Baraza na Kamati ya Fedha na Uchumi zilipitisha Azimio la kujengwa au kuimarishwa eneo la Mazizini liliopo duka la Diplomatic.


  1. Hakuna tangazo lolote lililotolewa kuhusiana na uimarishaji wa eneo la Diplomatic Super Market.
  2. Kumbukumbu za Vikao vya Baraza Kuu zinaonesha kuwa kumbukumbu zimeandikwa mwanzo na vikao ndio vikafuata. Kwa mfano Kikao namba 1/2012 kilifanyika tarehe 6 Machi, 2012 wakati kumbukumbu zimeandikwa tarehe 12 Machi, 2011. Aidha, Kikao namba 3/2012 kilifanyika tarehe 6 Juni, 2012 wakati kumbukumbu zimeandikwa tarehe 11 Juni, 2011.


Mheshimiwa Spika, katika hoja hizi, Kamati ilitoa mapendekezo yake kama ifuatavyo:


  • Waziri kabla ya kuchukua hatua azingatie zaidi matakwa ya Sheria mbali mbali kuliko utashi ili kuepuka mvutano usio wa lazima.
  • Serikali kwa kupitia Makamu wa Pili wa Rais ichunguze tuhuma zilizotolewa dhidi ya viongozi hawa na endapo itathibitika hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika.
  • Baraza la Manispaa kuitisha zabuni kwa ajili ya ujenzi wa eneo hilo
  • Kwa kuwa kuna mgongano wa tarehe katika kumbukumbu za vikao, kamati inawashauri Watendaji wa Baraza wawe makini wakati wa kuandaa kumbu kumbu mbalimbali za vikao.



Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na pendekezo la Kamati la kumtaka Waziri kuzingatia matakwa ya sheria kabla ya kuchukua hatua. Aidha, Serikali imechunguza tuhuma kwamba Waziri na Mkurugenzi wamepatiwa fedha kwa ajili ya kutoa maamuzi ya upendeleo na haikupata ushahidi wowote juu ya tuhuma hizi.


Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kumalizana na mkodishwaji wa duka hilo kwa kukubaliana kuendelea na mkataba nae kwa masharti mapya au kusitisha mkataba huo. Aidha, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuona utaratibu gani wa kumaliza mkataba na mkodishwaji huyo ili kutoa fursa kwa Baraza la Manispaa kuliendeleza eneo hilo. Vilevile, Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kuwa makini katika uandaaji na uwekaji wa kumbukumbu za vikao ili kusitokee utata juu ya taarifa za kumbukumbu hizo.


Hoja Nambari 32: Maeneo ya Masoko hujengwa majengo ya maduka na kudhoofisha dhamira ya kuwa na masoko.


Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Kamati Teule imependekeza kuwa Baraza la Manispaa liachane na tabia ya kujenga maduka ya kudumu katika masoko na badala yake ibakie na dhana ya kuwa na masoko.


Mheshimiwa Spika, Ushauri uliotolewa na Kamati Teule ni wa busara na kimsingi Serikali inakubaliana na mapendekezo yao. Hata hivyo, mtazamo wa Baraza la Manispaa wa kuchanganya maduka na soko ni wa kisasa zaidi na unatumika katika nchi mbalimbali duniani. Serikali imelitaka Baraza la Manispaa kuweka dhamira ya kuchanganya maduka na soko tangu inapoandaliwa michoro na sio kuongeza mambo ambayo mwanzo hayakuwepo.


3. HITIMISHO


Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo na ufafanuzi huo wa Serikali, naomba nichukue fursa hii kwa mara nyingine tena kukushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kutoa maelezo haya. Vile vile nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Teule wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin kwa kazi yao nzuri yenye mustakbali mwema kwa nchi yetu.  Nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao kupitia Kamati zao mbalimbali. Nawashukuru pia viongozi na watendaji wa Baraza la Manispaa kwa kusaidia kutoa maelezo yaliyoweza kufafanua hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Teule.


Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza kuyafanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na kamati yako Teule na ni imani yangu kuwa kila taasisi inayohusika na utekelezaji wa mapendekezo hayo itafanya kazi zake kwa umakini na uadilifu mkubwa kwa lengo la kuliwezesha Baraza letu la Manispaa kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Post a Comment

0 Comments