6/recent/ticker-posts

Maalim Seif awaasa wagombea uongozi CUF: Msikubali kununuliwa

 BAADHI wajumbe wa mkutano mkuu wa chama cha wananchi CUF wilaya ya Mkoani Pemba wakimsikiliza Katibu mkuu wa chama hicho, Mhe: Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akizungumza nao kwenye mkutano huo uliambatana na uchaguzi mkuu wa wilaya, uliofanyika Jimbo la Mtambile jana (picha na Haji Nassor, Pemba)
 
KATIBU mkuu wa CUF Mhe: maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya ya Mkoani Pemba wa chama hicho, ambao uliambatana na uchaguzi mkuu wa wilaya, uliofanyika Jimbo la Mtambile jana (picha na Haji Nassor, Pemba)

 
MWAKILISHI wa CUF Jimbo la Kiwani Mhe: Hija Hassan Hija akitoa neno la shukuran, mara baada ya Katibu mkuu wa CUF Mhe: maalim Seif Sharif Hamad, kufungua mkutano mkuu wa chama hicho wilaya ya Mkoani, ulioambatana na uchaguzi (picha na Haji Nassor, Pemba)

KATIBU wa CUF wilaya ya Mkoani Pemba, Tahir Awesu akiwasilisha utekelezaji wa chama hicho,  kwenye mkutano mkuu wa wilaya ya Mkoani uliofunguliwa na Katibu mkuu wa CUF Mhe: Maalim Seif Sharif Hamad, ambao mkutano huo uliambatana na uchaguzi (picha na Haji Nassor, Pemba)

Na Haji Nassor, PEMBA
KATIBU mkuu wa Chama cha wananchi CUF Zanzibar Mhe: maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya ya Mkoani wa chama hicho, wasikubali kununuliwa na wagombea nafasi mbali mbali, na badala yake wawachague viongozi kwa kuwaona wanafaa.
Alisema ni kweli wapo baadhi ya wagombea wa nafasi zinazogombewa wamekuwa wakimwaga pesa kwa wajumbe hao, na endapo watazichukua na kisha kuwapa kura kutokana na fedha hizo, waelewa kuwa chama kitaanza kudhoofika.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo jana Mtambile wilaya ya Mkoani Pemba, wakati alipokua akifungua mkutano mkuu wa wilaya, ulioambatana na uchaguzi wa kuwachagua viongozi mbali mbali akiwemo Katibu, Mwenyekiti na wajumbe wa mkutano kuu taifa CUF taifa.
Alisema ni vyema wajumbe hao kuwa makini na kujitenga mbali na wagombea wenye nia ya kusambaaza fedha, kwao kwa ajili ya kuwapigia kura wakijua kuwa viongozi wa aina hiyo hawana nia thabiti na chama.

Alieleza kuwa ni vyema kuwachagua viongozi ambao ni wapiganaji wa kweli na ambao wataweza mapambano na vyama vyengine katika uchaguzi mkuu ujao, ili kuendelea kushika hatamu wa nafasi mbali mbali ikiwa ni pamoja udiwani, uwakilishi na ubunge.
‘’Mimi niwanasihi sana ndugu wajumbe wa mkutano huu, ambao ndio wapiga kura wa kuwachagua viongozi, lakini muelewa kuwa mkiwachagua viongozi legeleg ndio mnakidhoofisha chama, na mkiwa makini ndio kusema CUF inaweza kushinda hata ngazi ya raisi’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine Katibu mkuu huyo wa CUF, amewataka viongozi ambao watachaguliwa kuvunja makundi mara moja, wakijua kama wakiyaendeleza yanaweza kuleta mpasuko ndani ya chama.
Alisema wapo, baadhi yao hata baada ya kuchaguliwa huendelea na vikao haramu na makundi kwa wajumbe waliodhani wamewapigia kura, ambapo ni vyema wakaelewa mwisho wa makundi ni mara baada ya kutangaazwa mshindi.
Mapema akiwasilisha utekeleza wa kazi za chama kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, katibu wa CUF wilaya ya Mkoani Tahiri Awesu alisema pamoja na mafanikio yaliopatikana, zipo changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi.
Katika hatua nyengine alisema taarifa ambazo chama wanazo, kuna vitambulisho vya uzanzibari ukaazi zaidi ya 4000 katika wilaya ya mkoani havijachukuliwa, hivyo ametoa wito kwa wananchi kuvifuatilia.
Mapema mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Mhe: Hija Hassan amemuomba katibu mkuu huyo wa CUF akiwa pia Makamu wa kwanza wa rais kufuatilia kwa karibu taarifa za kutaga kupunguzwa tena majimbo kisiwani Pemba.
‘’Mimi kama mwakilishi nnazo taarifa kwamba tume ya uchaguzi ya Zanzibar, inataka kuyapunguza tena majimbo Pemba kutoka 18 ya sasa na kuwa 15, hili makamu wa kwanza tunaomba lisifanyike, maana sisi CUF wilaya wala hatutoliridhia’’,alifafanua.
Mkutano huo mkuu wa wilaya, unatarajia kuwachagua katibu, mwenyekiti pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu taifa ambapo awali viongozi waliochaguliwa miaka mitano iliopita walijiuzulu.

Post a Comment

2 Comments

  1. maalim nimeskia unagombea tena ukatibu mkuu mm ushauri wangu waandae watu wakuvaa viatu vyako mapema bila hivo kuna vita vya uongozi vinakuja ukija kuwa hupo tena maana sisi ni binaadam

    ReplyDelete
  2. Anonymous1 Nafikiri ushauri wako ni Mzuri sana lakini naona Wazanzibari wenyewe sio wajinga tena.. hawatachagua Mtu ambae ana onyesha kuwa na Dalili za Unafiki na Kuwagawa wazanzibari..Maalim Amechukua tena nafasi hiyo kwakuona kwamba kuna njama kubwa zakutaka kuwagawa wazanzibari katika dhama zilizopita.. Wazanzibari wanafaa kushukuriwa na hao viongozi wanaoipinga GNU, baada yakupiga kura za Ndio kwa asilimia 66% kukuba Umoja .Sasa Wazanzibari tumeweza kuwajua wale waliokua wapinzani wa umoja huo.. wanakusanyana kwa makundi kwenda mikutanoni ati wanasema Wawakilishi wanakwenda kuratibu Ilani za CCM.. Na wanatumia magari na hela za walipa kodi kwa mikutano hiyo..

    ReplyDelete