Na Mwandishi Wetu.
Serekali imeshauriwa kulipa kipaumbele suala la uazishwaji
wa mitaala ya Kodi kufundishwa katika
skuli ili kuweza kutoa fursa kwa wanafunzi hao kuwa na uelewa wa mapema juu ya
umuhimu wa kulipa kodi.
Hayo yameelezwa na Afisa wa Elimu kwa Walipa Kodi kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ndg Saleh Haji wakati alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari huko Ofisini kwake Mlandege mjini Zanzibar .
Alisema hatua hiyo pia itaweza kupunguza migogoro kwa
wanajamii, kutokana na kuelewa maana ya kulipa kodi kwa wanafunzi hao.
Aidha alisema tofauti iliopo sasa ni miongoni mwa
wafanyabiashara na Mamlaka za ukusanyaji wa mapato imetokana na kutokuwa na
uelewa wa mapema juu ya haki hiyo kama raia wa nchi badala yake kuona Serekali
ina lengo la kuwaharibia biashara zao, wakati wanapofuatilia kodi hizo.
’’Tutahakikisha tunaelimisha wanafunzi wote ili kila mmoja
ajue umuhimu na maana ya ulipaji kodi ili hapo baadae isijekuwa ni tatizo ndani
ya jamii,’’alisema ofisa huyo.
Aidha alifahamisha katika kuhakikisha wanafunzi hao wanaweza
kutambua maana ya ulipaji kod, wamefanikiwa kuazisha klabu za kodi katika skuli
ya Haile Ssalase pamoja na Skuli ya
Mombasa Biashara kwa lengo la kuwapa elimu ya kodi.
Ofisa huyo alisema kuwa endapo fursa hiyo itatolewa kwa
skuli zote za Unguja na Pemba wataweza
kuwajengea uelewa kwa haraka zaidi.
Alisema itakuwa vyema zoezi hilo kuendelezwa ili jamii iwe
na elimu ya kutosha juu ya suala zima la ulipaji ili hapo baadae kusijekuwa na
vikwazo ambavyo vinaweza kuleta mgogoro kati ya mlipa kodi na Mamlaka hiyo.
0 Comments