Na
Benedict Liwenga, Dodoma.
BUNGE Maalum la Katiba limepitisha
marekebisho ya kanuni ili kuliwezesha kufikia hatua ya mwisho ya upigaji kura
kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 2 mwaka huu.
Hatua
hiyo ililenga kumaliza vikao vya Bunge hilo kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa sheria
wa Oktoba 4 mwaka huu.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta,
wakati alipokuwa akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu uwasilishwaji wa azimio la
kupitisha marekebisho ya kanuni za bunge hilo.
Alisema
inakadiriwa kuwa wajumbe wasiopungua 480 wanatarajiwa kupiga kura na kutokana
na kanuni zilivyokuwa kabla ya mapendekezo ya mabadiliko hayo ingechukua siku
nyingi kukamilisha zoezi la upigaji kura kwa kupitia kifungu kwa kifungu.
“Kanuni
zilivyo hivi sasa kama hatutafanya mabadiliko itachukua kwa wastani wa dakika
kama mbili kwa kila mjumbe kupiga kura kwa kila kifungu ambapo kwa siku tutamia
wastani wa dakika 960 kwa ibara moja, tunatarajia ibara zitakuwa 300,” alisema
na kuongeza “kwa ibara hizo tungehitaji siku 300 kukamilisha zoezi hilo
ambao muda huo utakuwa kinyume na utaratibu uliopangwa tutakuwa tunamaliza ibara
moja kwa siku moja,” alisema.
Alisisitiza
kuwa marekebisho yaliyofanyika yalilenga kuhakikisha kazi ya upigaji kura
inakuwa rahisi na inamalizika katika muda uliopangwa wa kisheria wa siku 60.
Awali
akiwasilisha maelezo ya marekebisho ya kanuni za bunge maalum kwa niaba ya
Mwenyekiti wa Kamati ya kanuni na haki za Bunge Maalum, Amon Mpanju, alisema kanuni
zilizofanyiwa mabadiliko ni ya 36 na 38.
Alisema
marekebisho hayo yatamwezesha mjumbe aliye nje ya maeneo ya Bunge kwa ruhusa ya
maandishi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba kupiga kura ya wazi na siri
kwa njia ya nukushi na mtandao.
Alisema
hatua nyingine ni kumwezesha mjumbe kupiga kura katika muda usiozidi siku saba
kwa urahisi na ufanisi.
Akitoa
ufafanuzi wa wajumbe walioko hijja, Sheikh Norman Jongo, alisema mjumbe
anayetekeleza ibada hiyo hakatazwi kupiga kura ili mradi hajafikia hatua za
mwisho wa ibada hiyo.
Wakati
huo huo rasimu ya katiba mpya
iliyopendekezwa inatarajiwa
kuwasilishwa katika Bunge Maalum
la Katiba Septemba 24, mwaka huu.
Mabadiliko
hayo yametangazwa na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahya Khamis Hamad,
wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema
uamuzi wa mabadiliko hayo umetokana na kufanyika kikao baina ya Kamati ya
Uongozi wa Bunge hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi.
Hata
hivyo, alisema kazi ya uandishi wa rasimu hiyo imeshakamilika na kazi
iliyobakia ni kuipitia kwa makini.
Aliongeza
kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, inatarajia kukabidhiwa rasimu ya katiba mpya
iliyopendekezwa Septemba 23, mwaka huu kutoka kwa Kamati ya Uandishi wa Bunge
hilo.
0 Comments