Na
Rajab Mkasaba, Ikulu
UONGOZI
wa Benki wa Taifa ya Biashara (NBC) umeeleza kuvutiwa kwake na hatua za
maendeleo ya kiuchumi zilizofikiwa Zanzibar na kuahidi kuendelea kuziunga mkono
ili ziweze kuimarika zaidi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki hiyo, Mizinga Melu, aliyasema hayo wakati alipofanya
mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk.
Ali Mohamed Shein, akiwa pamoja na uongozi wa benki hiyo kutoka Tanzania Bara
na Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, alimueleza Dk. Shein
kuwa NBC inathamini juhudi na mafanikio yaliofikiwa na kusisitiza kuwa benki
yao ina kila sababu ya kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa serikali pamoja na
wananchi wa Zanzibar.
Alisema
NBC imepata mafanikio makubwa Zanzibar hali ambayo imetokana na ushirikiano
uliopo ambao umeisaidia benki hiyo kupiga hatua kubwa na kuimarika zaidi.
Aliahidi
kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za maendeleo.
Nae
Dk. Shein aliueleza uongozi wa benki hiyo, kuwa juhudi za benki hiyo na
mafanikio yaliopatikana ipo haja ya kuyaimarisha zaidi kutokana na ushindani
mkubwa wa kibiashara uliopo.
Aliueleza
uongozi huo kuwa licha ya ushindani huo NBC imeweza kupiga hatua katika
kujiimarisha.
Alitoa
wito kwa uongozi huo wa NBC kuendelea kutoa huduma zaidi kwa jamii ikiwa ni
pamoja na kutoa ushirikiano na kujitangaza katika maeneo ya vijijini.
Aliuahidi
uongozi huo kuwa serikali itaendeleza ushirikiano na benki hiyo pamoja na benki
nyengine zote ambazo zinafanya shughuli zake Zanzibar kwa lengo kukuza uchumi
na kuimarisha maendeleo.
0 Comments